Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Burhani, amesema kuwa vijana wa Tanzania ni watu wenye akili timamu, jambo linalowasaidia kutumia maarifa yao kwa wivu mkubwa katika kuilinda amani ya taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya KIJANI FIRST TIME VOTERS uliofanyika katika makao makuu ya nchi jijini Dodoma, Faris alieleza kuwa kuna baadhi ya wanaharakati kutoka nchi jirani ambao wameanza kuleta chokochoko na kutoa maneno ya dhihaka dhidi ya Serikali ya Tanzania.
"Vijana makini wa Tanzania hawatakubali hata siku moja kuona wanaharakati hao, ambao tayari wamekuwa chimbuko la machafuko katika nchi zao, wakijaribu kuhamishia chokochoko zao hapa nchini. Hatutavumilia kuona watu wakisababisha vurugu, majeraha, na hata vifo kupitia harakati zisizojali amani," alisisitiza Faris.
Kauli hiyo aliitoa kwa niaba ya vijana wa CCM Mkoa wa Kagera, katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyoongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Comrade Mohamed Ali Kawaida, pamoja na Baraza lake la Vijana Taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED