Wahandisi watatu, mwongoza watalii kusomewa hati mpya

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 03:10 PM Oct 01 2025
Nyundo ya mahakamani
Picha: Mtandao
Nyundo ya mahakamani

WAHANDISI watatu na mwongoza watalii mmoja wanatarajiwa kusomewa hati mpya ya mashtaka ya uhujumu uchumi Oktoba 9, 2025, wakikabiliwa na tuhuma za kuhujumu zaidi ya Sh. milioni 300 kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi.

Watuhumiwa hao ni Faustine Malya (44), mkazi wa Salasala; Emiliani Kimaro (35), mkazi wa Kibaha; Nelson Jacob (32), mkazi wa Kimara Mwisho — wote wakiwa ni wahandisi — pamoja na Tumaini Mollel (30), mwongoza watalii mkazi wa Kiseke, Mwanza.

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa taasisi tano, ambazo ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tawi la Mtwara, Halmashauri ya Jiji la Tanga, Skyline Properties Ltd, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kampuni ya Mafuta ya Camel.

Wakati kesi hiyo ilipotarajiwa kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, iliahirishwa kutokana na hakimu huyo kupata udhuru. 

Wakili wa Serikali Janeth Kimambo aliomba mahakama ipange tarehe nyingine, ambapo Hakimu Kemilembe Josiah aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, 2025.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kubadilisha namba za akaunti za benki za Kampuni ya Sec East African Ltd, ambayo husimamia miradi ya ufungaji lifti katika majengo mbalimbali, na kuweka namba zao binafsi, kisha kuwasilisha taarifa hizo kwa taasisi husika ili kulipwa fedha kwa njia ya udanganyifu.

Ili kufanikisha mpango huo, inadaiwa walighushi saini za Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Tian Chun, Mkurugenzi wa Masoko, Ntuli Mwankusye, pamoja na Mhasibu, Gabriel Makundi.

Makosa hayo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu yanadaiwa kutendwa kati ya Novemba 5, 2021 na Aprili 14, 2023, ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Endapo wakipatikana na hatia, washtakiwa hao watakabiliwa na adhabu kali kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi.