MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, amewatangazia kiama wananchi wanaohujumu miundombinu ya maji kwa kuiba dira zake na kwenda kuuza kama chuma chakavu.
Amesema vitendo hivyo vinasababishia hasara kubwa ya upotevu wa mapato Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA).
Mhita ametoa kauli hii, leo, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji tangu mwaka 2020 mpaka hivi sasa kutoka kwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usambazaji na Usimamizi wa Mazingira KUWASA, Mhandishi Magige Marwa, iliyofanyika ukumbi wa mamlaka hiyo.
Amesema serikali haiwezi kuendelea kuvumilia kuona baadhi ya wananchi wasiokuwa wadilifu wakiendelea kuhujumu miundombinu ya maji, iliyogharimu fedha nyingi za umma,kwani fedha za ukarabati wake zilipaswa kuongeza mtandao wa maji maeneo mengine.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usambazaji na Usimamizi wa Mazingira KUWASA, Mhandishi Magige Marwa amesema, baadhi ya wananchi wamekuwa wakihujumu mamlaka kwa kuiba dira za maji na kwenda kuuza kama chuma chakavu huku wengine wakijiunganishia huduma kinyemela.
Pia amesema,wengine wanatoboa bomba za maji na kumwagilia mashamba yao ya zao la mpunga kutokana na kukosekana kwa mvua ya uhakika na wamekuwa wakipata hasara kubwa kwasababu pia huduma hiyo nao wanailipitia kupitia kwa wazalishaji wao KASHUWASA.
“Tumekuwa tukiwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wote wanaobainika kuhujumu miundombinu yetu, tunapoteza mapato mengi kutokana na maji yanayomwagiza ovyo ikiwa ni pamoja na fedha za marekebisho ya miundombinu,” amesema Marwa.
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Mhandisi, Allen Marwa amesema, wamepokea zaidi ya Sh. bilioni tisa kutoka Wizara ya Maji, kwa ajili ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi inayoendelea na ifikapo mwakani watakuwa na asilimia 96 ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED