Wana-CHADEMA sita wakamatwa Songea

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:11 PM Apr 21 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Marco Chilya.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Marco Chilya.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Kusini kimesemea viongozi wake watatu, mwimbaji nyimbo za chama na wanachama wawili wameshikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Songea Mjini.

Taarifa ya awali iliyotolewa leo Aprili 21,2025 na CHADEMA makao makuu, imewataja viongozi hao kuwa ni  Christian Komba, Mwenyekit wa Jimbo la Songea, Esau Chiza Mwenyekiti wa BAVICHA Jimbo la Songea, Zubery Tindwa Mjumbe wa Kamati Tendaji Jimbo la Songea, George Mwingira  mwimbaji wa nyimbo za Chama,Abubakar Swalehe na Erick Wolfrem.

Akizungumza na Nipashe Digital, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kusini, Masoud Malimusi, amesema viongozi hao walikamatwa kwa nyakati tofauti na wapo katika Kituo cha Polisi Songea Mjini, ikiwamo wanne waliokuwa wamekutana Baa kujadili mambo yao wakiwa na sare za chama zenye maneno ya ‘No Reforms No Election”

Amesema Mwenyekiti alikamatwa baada ya mkewe na mtoto wake kuchukuliwa na polisi ambao walikwenda dukani na kukuta limefungwa kwa kuwa alikwenda kituo cha polisi kuwapelekea chakula wenzake waliokamatwa.

Malimusi amesema akiwa kituoni alipigiwa simu na mkewe ambaye alimtaka kwenda dukani na alipofika aliwakuta polisi ambao walimkamata na kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake.

George Mwingira

Amesema viongozi na wanachama hao wamepekuliwa kila mmoja nyumbani kwake na kurudishwa kituoni humo na kwamba wamejulishwa kuwa wanashitakiwa kwa sababu walikuwa wanaandaa ajenda ya kufanya maandamano kupinga kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu.

“Tulichoelekwa ni kuwa walifanya mkusanyiko usio halali, tusichoelewa hawa watu walikuwa wamekaa watatu wanaongea, sasa sijui ni kwasababu wamevaa sare za chama za ‘No Reforms No Election’ au vipi, tumeambiwa tutafute barua za kuwadhamini, na wamehojiwa asubuhi hii. Tukirudi kituoni tutajua nini kinaendelea,”amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Marco Chilya alipoulizwa amesema: “Nachojua tumeshikilia waalifu si wanachama. Nitafute baada ya saa mbili nitakuwa na ufafanuzi zaidi,”Si kila anayeshikiliwa ni mwanachama sisi tunashikilia waalifu.