Wasira: CCM sio sawa na vyama vingine kina historia nzuri

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:17 PM Apr 16 2025
Makamu Mwenyekiti wa CCM Stephen Wasira akiongea na wana CCM Tabora, leo.
Picha: Maulid Mmbaga
Makamu Mwenyekiti wa CCM Stephen Wasira akiongea na wana CCM Tabora, leo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema chama cha mapinduzi sio sawa na vingine kwasababu kina historia nzuri, na niwalinzi wa mapindunzi ya Zanzibar na ndio wanaojua siri ya uhuru na faida ya umoja kwakuwa imetokana na juhudi zao.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho leo Urambo mkoani Tabora, Wasira amesema licha ya historia ya kuleta maendeleo na mabadiliko lakini kuna vijana wamesoma na kulala kwenye vitanda walivyovijenga wao huku wakisema CCM hawajafanya kitu.

Amesema wazazi wao zamani walikuwa hawajui kliniki walikuwa hawajifungui ila walikuwa wanazaa, "Anaenda shamba analina na ujauzito anajifungua hakuna anaejua wakisikia mtoto analia ndo wanajua kuna mtoto kazaliwa hapo, lakini Tabora ya sasa huwezi kuifananisha na miaka 60 iliyopita".

"Kwa sasa vifo vya mama wajawazito na watoto vimepungua kwasababu hospitali na vituo vya afya vimeongezeka, barabara zimejengwa kila mahali, kila mkoa umeunganishwa na lani, lakini wanasema hatujafanya lolote muwasamehe," amesema Wasira.

Baadhi ya wananchi na wanachama wa CCM.

Akizungumzia suala la tumbaku Wasira amesema, zao hilo pia limeendelea, wakulima wanauza kwa dola, na kwamba maendeleo ni hatua kwa hatua akieleza kuwa kwa kawaida yake unaondoa tatizo moja linakuja lingine ukitengeneza barabara magari yanaongezeka watu wanagongwa linageuka kuwa tatizo lingine, hayo ndio maendeleo.

Amesema tatizo jipya wanalitafutia ufumbuzi kama kwa upande wa elimu wanawasomesha watoto wawe na ufundi ili wakienda wajue cha kufanya, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo kazi ya chama cha mapinduzi. Na mapinduzi yenyewe ni maendeleo ya watu.

"Sisi hatuna mtaji wa pesa mtaji wetu ni watu, wakiendelea kutuunga mkono tunaendelea kuwepo, tutaendelea kutetea maslahi ya wananchi na hakuna mtu atakaekuwa na mamlaka ya kutuhoji kwanini tumeongezo miaka yote kwasababu wakati tunadai uhuru hatukuingia makubaliano kuwa tutaongoza kwa muda gani," amesema Wasira.