WAKALA wa Huduma za Misitu (TFS) pamoja na Halmashauri za mkoa wa Pwani, zimetakiwa kutumia mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini kupanda miti katika maeneo ya mkoa huo kufikia lengo lililowekwa.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wakati wa uzinduzi wa siku ya upandaji miti katika Halmashauri ya Chalinze shule ya Msingi Chalinze Mzee ambapo miti 560 ilipandwa.
Amesema Mkoa huo unatakiwa kupanda miti milioni 13.5 kwa mwaka, kila halmashauri itapanda miti milioni 1.5.
Pia amezitaka halmashauri kufuatilia miti inayopandwa iwe endelevu badala ya kutumia rasilimali nyingi kwenye upandaji miti ambayo haiendelei.
Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, PCO Mathew Ntilicha, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi Prof. Dos Santos Silayo, amesema lengo la upandaji miti ni kuhamasisha jamii kuhifadhi misitu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Ofisa Misitu Mkoa wa Pwani, Pierre Protas amesema pamoja na mchango mkubwa wa misitu kwa jamii, bado kuna changamoto zinazoikabili rasilimali hiyo ambazo ni pamoja na uanzishwaji wa mashamba na makazi.
Pierre ametaja changamoto nyingine kuwa ni utegemezi kwenye nishati ya kuni na mkaa kama chanzo cha nishati na kipato kwa jamii ndani na nje ya mkoa wa Pwani, pamoja na uhaba wa watumishi katika sekta ya maliasili.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, ambaye pia ni Ofisa Elimu Msingi, Miriam Kihiyo naye amewaagiza walimu wakuu kuhakikishq kila mwanafunzi anapanda mti na kuitunza zaidi ya wanafunzi 61,000 huku akiomba TFS kuwasaidia dawa kwa ajili ya mchwa wanaohatibu miti.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED