Watumishi wa afya wapanda miti 500

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 03:49 PM Apr 30 2025
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, akipanda mti kuboresha mazingira ya hospitali hiyo
Picha: Marco Maduhu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, akipanda mti kuboresha mazingira ya hospitali hiyo

WATUMISHI wa afya katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, wameadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), kwa kupanda miti 500 katika maeneo ya hospitali hiyo.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira na kuhimiza utunzaji wa afya, kwa njia ya mazoezi.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo, Aprili 30, 2025, pamoja na upandaji miti, watumishi hao walishiriki mbio za kilomita 7.8 kama njia ya kuimarisha afya zao.

Watumishi wahamasisha wananchi kufanya mazoezi
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Luzila John, amesema wameamua kupanda miti hiyo, ili kuboresha mazingira ya hospitali, pamoja na kukimbia mbio hizo, ili kuimarisha afya za watumishi na kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi.

"Kesho ndiyo kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi, ambayo Kitaifa yatafanyika Singida, lakini na sisi kama watumishi wa afya katika Hospitali ya Rufani hapa Shinyanga.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira
“Tumeamua kupanda miti pamoja na kukimbia Mbio kilomita 7.8, ili kuimarisha Afya zetu," amesema Dk. Luzila.

Amesema wameweka pia mabanda katika Uwanja wa CCM Kambarage, kwa ajili ya wananchi kupima afya zao, huku akitoa wito kwa wananchi ni kwamba wapende kupima afya zao, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, ili wajikinge na magonjwa yasiyoambukiza.

“Tunatarajia pia kuanzisha Shinyanga RS Fitines Club, ili watumishi wawe wanafanya mazoezi na hata kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kuimarisha afya zao, ili wajikinge na magonjwa yasiyoambukiza," ameongeza.

Ofisa Afya Mazingira katika hospitali hiyo, Emiliana Charles, amesema katika zoezi hilo wamepanda miti 500, ambayo itasaidia pia wagonjwa kupata kivuli, matunda na kuzuia pia mmomonyoko wa udongo.