Wawili washikiliwa wakijaribu kumteka Jonathan Ayo

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:39 PM Apr 15 2025
Wawili washikiliwa wakijaribu kumteka Jonathan Ayo
Pi
Wawili washikiliwa wakijaribu kumteka Jonathan Ayo

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limetoa ufafanuzi kuhusu picha mjongeo, iliyoonekana kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikihusisha watu waliokuwa wanatumia gari lenye namba za usajili T 540 EHF aina ya Toyota Noah, ikidaiwa wakijaribu kumteka Jonathan Ayo (37), mkazi wa KCMC Moshi eneo la Mbuyuni Wilaya ya Moshi Manispaa Aprili 12, 2025.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, lilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watu wawili ambao ni Kelvin Temu (39), mkazi wa KCMC Moshi na Samson Magere (30), mkazi wa Soweto Moshi wakiwa na gari T.540 EHF aina ya Toyota Noah, inayodaiwa kuhusika katika tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (SACP) Simon Maigwa, amesema uchunguzi wa tukio hilo umebaini kwamba halikuwa la utekaji bali watuhumiwa hao walikuwa wamemwajiri Jonathan Ayo, anayedaiwa kutekwa kama mtaalam wa mifumo wa kampuni yao.

Amefafanua kuwa Aprili 6, 2025, Ayo alikwenda ofisini kwao mtaa wa Soweto kuchukuwa kompyuta mpakato ya ofisi akieleza kuwa, anataka kufanyia kazi za ofisi akiwa nyumbani kwake na angeirudisha kesho yake.

Ameeleza kuwa baada ya Ayo kuondoka na laptop hiyo, hakuirudisha ndipo waajiri wake walipata mashaka na walianza kumtafuta kwa siku tano bila mafanikio na ilipofika  Aprili 12, 2025 walimpata akiwa ‘Bar’ mtaa wa Rau, akinywa pombe na alikubali kwenda kuwakabidhi laptop hiyo.

“Watu hao walitumia gari T.540 EHF aina ya Noah baada ya kuipata laptop yao waliamua wampeleke Polisi kwa hatua zaidi na walipofika eneo la Mbuyuni majira ya saa moja usiku, Ayo alifungua mlango wa gari ikiwa imesimama kwenye foleni na kujaribu kukimbia akiwa anapiga kelele za wezi.

Ilisababisha wananchi, kuwashambulia watu hao askari mgambo aliyekuwa eneo hilo, alifanikiwa kuzuia vurugu hizo na kumfikisha kituo cha Polisi Moshi,” ameeleza Maigwa.

Ameongeza kuwa kulingana na uchunguzi uliyofanyika hadi sasa hakukuwa na mazingira au tukio la utekaji kama inavyoenezwa katika mitandao ya kijamii bali ni mazingira yaliyotokana na Ayo ya kujaribu kukimbia huku akipiga kelele za wezi ili kukwepa kufikishwa Polisi.