Wazee 1,008 wakatiwa bima kwa mil 24.4/-

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:35 PM Apr 16 2025
Katibu wa Baraza la Wazee Taifa Mzee Anderson Lymo akizungumza katika baraza la madiwani la Manispaa ya Kahama wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa bima za afya kwa wazee wa kahama leo
Picha: Shaban Njia
Katibu wa Baraza la Wazee Taifa Mzee Anderson Lymo akizungumza katika baraza la madiwani la Manispaa ya Kahama wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa bima za afya kwa wazee wa kahama leo

MANISPAA ya Kahama mkoani Shinyanga, imetenga na kutoa Sh. mil 24.4 na kuwakatia Bima za Afya ya Jamii-CHF, iliyoboreshwa kwa wazee wanaishi katika mazingira magumu.

Hatua hiyo, inalenga kurahisisha upatikanaji wa matibabu wanapofika vituo vya afya kupata tiba.

Katibu wa Baraza la Wazee Taifa, Anderson Lymo, ameyabainisha haya leo, katika Kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri, kilichojadili masuala mbalimbali, ikiwamo kuwasilisha taarifa za maendeleo inayotekelezwa kila kata.

Amesema, manispaa ya Kahama kila mwaka wa fedha, imekuwa ikitenga fedha na kuwakatia CHF iliyoboreshwa wazee wanaotoka katika mazingira magumu na wasiokuwa na ndugu wa kuwahudumia na mwaka huu, zaidi ya wazee 1,080 wanakwenda kupata bima hizo.

Lymo amesema, jumla ya Sh.milioni 24.4 zimetolewa kati yake Sh.milioni 5 zilitolewa mwaka 2021, Sh.milioni 6 mwaka 2022, Sh.milioni 3 mwaka 2023, Sh.milioni 5 mwaka 2024 na mwaka huu zinatolewa Sh.milioni 5.4 kwa wazee 1,080 kutoka kata 20.

 “Nchi nzima ni Manispaa ya Kahama pekee inayotenga fedha kwa ajili ya kuwajali wazee wasiojiweza na kuwakatia bima za afya ya CHF iliyoboreshwa, bima hizi zinawawezesha kupata matibabu na mwaka huu jumla ya wazee 1,080 sawa na wazee 50 kila kata watapata bima”Ameongeza Lymo.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa hiyo Laurent Nkwambi amesema, utaratibu wa kuwapata wazee hao unaanzia kwenye baraza ya wazee wa mitaa na vijijini, kwani wao ndio wanaowafahamu na kuwasilisha majina na kuwakatia bima hizo.

Amesema, vigezo wanavyovizingatia ni wasiokuwa na uwezo yaani wanaishi mazingira magumu pamoja na wale wasiokuwa na familia za kuwalea na kila mwaka fedha zinapopatikana wanazihuhisha bima hizo ili wasije kukosa matibabu wanapofika vituo vya afya au hospitalini kwenye matibabu.

Makamu Mwenyekiti wa Manispaa ya Kahama Machumu Sindano amesema, wataendelea kutenga bajeti ya bima za wazee kulingana na wanavyokusanya mapato ya ndani, na watahakikisha wazee wote wanafikiwa na kuhudumiwa na kila mwaka idadi imekuwa ikiongezeka.