Mbunifu wa kitanzania, Yvonne Baldwin, ameweka historia kwa kushinda tuzo mbili kubwa za kimataifa katika mashindano ya AI for Good Innovation Factory 2025, ya Jukwaa la Umoja wa Mataifa linalosaidia kuongeza kasi ya miradi ya teknolojia kwa maendeleo ya dunia (AI for Good).
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo imefanyika wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Jamii ya Habari unaoendelea mjini Geneva.
Akiwa mmoja wa washiriki kutoka jumla ya bunifu 650 duniani, Baldwin ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa Kampuni ya Elevate AI Africa, ameibuka mshindi wa kwanza katika Mashindano ya Women’s Innovation Factory Pitching Competition 2025 kupitia mradi wake wa MamaMate, unaolenga kuwasaidia wanawake waishio vijijini kupitia huduma za afya na ustawi zinazotumia teknolojia ya AI.
Mbali na ushindi huo, Yvonne pia ametangazwa kuwa Mshindi Mkuu wa Mashindano ya AI for Good Innovation Factory 2025, akijishindia cheti, tuzo, na zawadi ya dola 20,000 za Kimarekani.
Mashindano hayo ni sehemu ya mpango wa kimataifa wa AI for Good unaosimamiwa na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU), yakilenga kuibua, kuendeleza na kuongeza athari ya miradi ya akili bandia yenye suluhisho kwa changamoto za maendeleo endelevu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED