Akili unde injini inayoendesha kufanikisha kila unachofanya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:06 PM Sep 23 2025
Akili unde injini inayoendesha kufanikisha kila unachofanya
Picha: AI
Akili unde injini inayoendesha kufanikisha kila unachofanya

KWA Kiingereza ni Artificial Intelligency-AI na kwa Kiswahili ni akili unde ‘AU’, ikimaanisha kuwa imeundwa na binadamu ili aitumie kutatua changamoto mbalimbali zinazomkabili ikifanya jukumu hilo kwa ufanisi na weledi tena kwa gharama nafuu.

Watalaamu wanaichambua AU kuwa ni zao la akili ya binadamu na hakuna tatizo inapotumiwa kwa sababu ni zana inayohitajika zaidi kwa maendeleo ya dunia na Tanzania pia.

Akili unde ni kazi ya binadamu anayeunda mashine kuanzia kompyuta, simu, vifaa kama GPS, ndege sisizo rubani, CCTV kamera za ulinzi, saa,magari yasiyohitaji dereva, roboti za kuzalisha viwandani vyote vyenye uwezo, ufanisi na kasi kubwa ya ufahamu na utambuzi mithili ya akili za watu.

Itakumbukwa AI au AU ni nadharia zilizoelezwa kwa mara ya kwanza na John McCarthy, mwanasayansi wa kompyuta wa Marekani miaka ya 1950 ambazo leo zinatikisa dunia.

AI ikitumika ipasavyo kwa malengo ya kiufanisi haina tatizo, lakini inapotumiwa kuhadaa na kudhalilisha haipendezi. Japo kuna baadhi hutumia kuonesha viongozi au watu fulani wakizungumza jambo ukadhani ni kweli wakati ni uongo, kadhalika ikamwonesha mtu mwenye hadhi yake anacheza midundo ukafikiri ni ukweli lakini ni udanganyifu.

Teknolojia hii inahitajika ili itumike kusaidia mazingira magumu yanayomkabili binadamu. AI isionekana kuwa ni kitu kibaya ni zana ya uchambuzi ujuzi na maarifa kwa ajili ya maendeleo.

Taarifa za mitandaoni zinaitaja teknolojia ya Artificial Intelligence, imekuwa gumzo duniani na sasa inatumika kama silaha ya mapambano kwa kila kitu, kuanzia shuleni darasani, angani kwenye vita na kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.

Kwenye biashara wataalamu wanadokeza kuwa AI inaweza kusaidia kupunguza gharama, kuongeza tija na hata kuleta wateja wapya endapo itatumika kwa njia sahihi.

Kwanza, AI hutoa nafasi ya kuelewa mahitaji ya wateja. Programu zake zinaweza kuchanganua taarifa kutoka kwa mauzo ya awali na mitandao ya kijamii ili kubaini bidhaa au huduma zinazopendwa zaidi.

Hatua hiyo humsaidia mfanyabiashara kuhakikisha duka, genge, hoteli, nyumba za kupanga hakosi kila kitu huduma au bidhaa zinazohitajika na pia kuepuka hasara ya kuhifadhi bidhaa zisizo na soko hasa madukani.

Halikadhalika kwenye biashara AI ni nadharia ya muhimu na yenye nguvu katika masoko na matangazo ya kidijitali. Kupitia zana maalum, mfanyabiashara anaweza kufahamu ni kundi gani la wateja linavutiwa zaidi na bidhaa zake, saa zipi matangazo yanafaa kuwekwa mtandaoni, na hata lugha bora ya kutumia kuwavutia, kuwasaka na kuwafikia wateja.

Kujua lugha tamu kunakuwezesha kuandaa matangazo yenye ushawishi mkubwa mitandaoni ikiwamo kwenye simu yako na kuyasambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Zama hizi kwenye biashara mbinu za kuwafikia na kuwahudumia wateja zimebadilika sana kupitia program mbalimbali kama za 

rogramu ya kompyuta zilizoundwa zenye mazungumzo ya kusisimua na kuhamasisha watu kupitia mtandao ya kompyuta mfano ‘chatbots’.

Programu hizo hufanya kazi saa 24 na kwa mfanyabiashara huwezesha kujibu maswali ya wateja haraka haraka bila kuhitaji mhudumu au msaidizi.

Huduma za papo kwa hapo huimarisha uaminifu wa wateja na kuwafanya warudi tena na kuendelea kuhitaji na kununua bidhaa zako.

Zama hizi AI ni msaada mkubwa katika kusimamia mapato na matumizi na masuala yote yanayohusu fedha na hesabu.

Akili unde inatumiwa kuandaa programu za kisasa zinazoweza kufuatilia kila senti inayotumika au kuingia, hivyo kuzuia hasara na udanganyifu. 

Pia, inaweza kutabiri changamoto za kifedha kabla hazijatokea na kumpa mfanyabiashara nafasi ya kupanga na kukabiliana nazo kabla ya kuumizwa.

Hata hivyo, wataalamu wanakumbusha kuwa AI haipaswi kuchukua nafasi ya ubunifu na maamuzi ya binadamu na la muhimu wafanyabiashara wajifunze kutumia teknolojia hii kwa uangalifu, kuwekeza katika mafunzo ya wafanyakazi na kuendelea kudumisha huduma bora za kibinadamu.

AU ambayo ni mifumo ya kompyuta inayofanyakazi ambazo zinahitaji akili ya binadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha, inatumika karibu kila mahali leo na hata wewe mmachinga una nafasi ya kuitumia pia.

Ukweli kuwa ndizo roboti, ndege zisizo na rubani au droni, magari yanayojiendesha bila dereva, kamera za CCTV, malipo ya kielektroniki mfano ya kutumia ‘kontroli namba’ madaktari wa kiroboti, si hivyo pekee hata mjasiriamali anaweza kuwa na program zake za kubadilisha mambo.

Akili unde pia ipo ndani ya kompyuta na kwa kila eneo zipo injini za kutafuta taarifa zake mfano tovuti ya Google, YouTube, Tiktok na Netflix, Google Assistant, Siri na kwenye roboti za mazungumzo zipo ChatGPT na Gemini.

Kwa hivyo, iwe unamiliki baa, mashine za kutoa fotokopi, hoteli, kioski, bodaboda, bajaji, biashara mtandaoni au kampuni kubwa, zama hizi ni za kuangalia jinsi AI inavyoweza kukusaidia.

Ikitumika vyema, teknolojia hii inaweza kukuza biashara yako, kuongeza mapato na kukuwezesha kushindana kwenye masoko ya ndani na nje na kukupaisha kimafanikio.