CHAMA cha ACT Wazalendo, kimezindua ilani ya uchaguzi inayobeba vipaumbele saba ikiwamo cha kuwalipa wananchi wote pensheni pale wanapofikia umri wa kustaafu.
Uzinduzi wa ilani hiyo ukifanyika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Dar es Salaamu na kuhudhuriwa na wafuasi wa chama hicho na viongozi wakuu unaendelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kuandaa Ilani, Emmanuel Mvula, anayesema chama hicho kitatimiza ahadi zote zilizopo katika andiko hilo.
Miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kujenga uchumi wa watu binafsi na wakujitegemea utakaozalisha ajira milioni 12, chama kikilenga
kufufua, kujenga na kuwezesha ujenzi wa viwanda vipya vinavyomilikiwa na wazalishaji vijijini na kitahakikisha angalau asilimia 85 ya malighafi ya viwanda vya ndani inatokana na wazawa.
"Tutalinda haki za wafanyabiashara wadogo kwa kuruhusu kufanya biashara mijini na maeneo yenye mikusanyiko.Tutaanzisha na kuimarisha masoko maalum kwa siku, saa au mwezi, mahususi kwaajili ya wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali.
"Tutajenga nyumba 500,000 katika maeneo mbalimbali, za watumishi wa umma, wazee, watu wenye ulemavu pamoja na wenye hali duni ili Watanzania waishi kwenye nyumba za staha na ujenzi unakuwa nafuu," anasema Mvula.
Anaendelea na ufafanuzi kwamba watapunguza kodi ya wafanyakazi ili kuwaongezea wafanyakazi kipato waweze kumudu mahitaji katika maisha, kujiwekea akiba au kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji kipato cha ziada.
Kipaumbele cha pili katika ilani hiyo ni kutoa huduma bora na zenye staha kwa jamii yote ambayo ni upatikanaji na ubora wa, elimu, tiba, maji, umeme, nishati, mawasiliano na uhuru wa habari.
"Tutashusha bei ya kununua umeme kwa uniti kwa asilimia 50 na kuhakikisha umeme unapatikana kila nyumba.Tutapunguza gharama ya kuunganisha umeme kwa matumizi ya nyumbani hadi Sh 25,000 mijini na vijijini.
"Tutahakikisha uunganishaji wa umeme unafanyika ndani ya siku 10, baada ya kufanya malipo na kuziunganisha kaya masikini na huduma hiyo bila malipo, kuongeza matumizi ya gesi asilia (LNG) kwenye magari, kwa kuunganisha magari yote ya serikali, mabasi ya mwendokasi, malori na mabasi ya mikoani pamoja na kuongeza kiasi cha umeme kinachozalishwa kutoka megawati 4,031 hadi megawati 9,365 kufikia mwaka 2030," anasema Mvula.
Eneo la tatu linaloguswa na ilani hiyo ni usimamizi wa haki, usawa na demokrasia kwa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani na ustawi.
Pia ilani hiyo inaeleza zaidi kuwa haijasahau madhila ya utekaji, kupotea kwa raia, rushwa na ufisadi na kwamba serikali ya chama itajenga taifa lenye haki, usawa na demokrasia.
Eneo jingine lililogusiwa ni kuimarisha muungano na uhusiano wa kimataifa katika eneo hilo ilani hiyo inaeleza itaimarisha muungano na kuhakikisha kunakuwa na muungano wa haki, usawa na Kuheshimiana.
Pia inaeleza itautambua muungano kama ni ishara ya udugu na mshikamano, na ni tunu ya taifa, ambayo hata hivyo inapaswa kudumu kwa heshima na manufaa ya pande zote mbili pamoja na kuirejesha heshima, jina, ukuu na nafasi ya Tanzania katika kilele cha diplomasia barani Afrika na katika nchi za Ukanda.
Kipaumbele kingine ni kulinda na kusimamia ardhi na rasilimali za taifa, hapo mwasilishaji anafafanua:"Tutahakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya umiliki katika miradi na shughuli za uwekezaji katika ardhi, wananchi hawaondolewi kwenye ardhi yao bila kushirikishwa na kulipwa fidia na ya haki, kabla ya kuondolewa na kuhamishwa.”
"Tutaharakisha utekelezaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa, mkoani Njombe, na mradi wa Kabanga Nickel wilayani Ngara, mkoani Kagera na kuhakikisha utekelezaji unaanza ndani ya mwaka mmoja.
"Tutaweka mikataba yote ya ardhi na rasilimali wazi kwa wananchi, iliyoingiwa na itakayoingiwa kwa ajili ya kukuza na kuongeza uwazi na uwajibikaji. Na tutachukua hatua kali dhidi ya watumishi wote waliohusika katika mikataba yote iliyoingiwa na inayoliingizia taifa hasara, kutokana na uzembe na ufisadi" anasema Mwenyekiti Mvula.
Kipaumbele kingine ni kuboresha miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi katika hilo, chama hicho kinasema kitaongeza treni za SGR na safari zake kwa kutoa huduma ya usafiri wa treni kwa saa 24 ili itumike kikamilifu kusafirisha shehena na kupunguza msongamano, uharibifu wa barabara na gharama za usafirishaji.
"Tutajenga reli ya SGR ya Kusini Dar- Lindi–Mtwara-Ruvuma, kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo na itakayounganisha maeneo ya migodi ya Mchuchuma, Liganga na Kabanga Nickel hadi bandari za Mtwara, Dar es Salaam na Bagamoyo.
"Tutajenga na kuhakikisha barabara zote za mikoa na barabara kuu zinakuwa za kiwango bora cha lami na tutapandisha barabara zote za wilaya kuwa kiwango cha changarawe au lami. Tutanunua vivuko vikubwa vipya 15 na kukarabati vivuko vyote vilivyopo ili kutoa huduma bora za usafiri za uhakika, haraka na nafuu," anasema Mvula.
Kipaumbele cha mwisho ni kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, katika hilo ilani hiyo inafafanua itadhibiti biashara ya kaboni na kupitia upya mikataba ya biashara ya kaboni iliyopo na kuiweka wazi.
"Tutaanzisha vituo vya utabiri wa hali ya hewa katika ngazi ya kila wilaya na kujenga mifumo ya kisasa ya kutoa tahadhari na taarifa ya hali ya hewa, kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na kupunguza kodi na ushuru kwenye magari na vyombo vya moto vinavyotumia nishati safi, vinavyoingizwa nchini.
Baada ya kuwasilishwa kwa ilani hiyo, kiongozi wa chama Dorothy Semu anasema hivi sasa umasikini umekuwa jambo la kawaida na serikali iliyopo madarakani haishtuki.
Anapigilia msumari kwamba kwa miaka 64 ya uhuru bado huduma za afya ni mbovu, na hivyo kuna kila sababu ya kupambana kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya amani na kuiondoa katika genge la watu wachache.
"Nchi imegeuka kuwa ya mikopo isiyo na tija, miaka 64 baadaye nchi yetu inashuhudia wafanyabiashara, wasanii, wakulima na watumishi wana chuki na hofu ikitamalaki CCM wametudhihirishia hawana tofauti na misingi ya wakoloni weupe na hatuna budi kutangaza vita dhidi yao " anasema Dorothy.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED