KATIBA ya Tanzania mwaka 1977, imeshafanyiwa mabadiliko mbalimbali au kupigwa viraka zaidi ya mara 10 kwa lengo la kuiboresha ili iendane na mahitaji ya sasa lakini hata hivyo mambo hayajakaa sawa, inalalamikiwa.
Japo lengo ni kukidhi matakwa na mahitaji ya wananchi kwa ujumla, baadhi ya Watanzania wamekuwa wakitamani kuwapo kwa katiba mpya inayoendana na mazingira ya sasa.
Wakati hali ikiwa hivyo, mgombea urais wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Justas Rwamugira, anasema akipata ridhaa ya kuongoza taifa ataendelea kuweka viraka zaidi katika katiba ya sasa.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, anasema haoni umuhimu wa kuwa na katiba mpya, bali ni kuiwekea viraka iliyopo, akitaja sababu kuwa ni jambo hilo halitaki haraka bali ni la kwenda nalo taratibu na kuwa makini, sio la kukimbilia na kujikuta hali ikiwa mbaya zaidi.
Anafafanua kuwa katika utawala wao, watakuwa wanaifanyia mabadiliko kila baada ya miaka mitano kwa kushirikisha wananchi ili watoe maoni yao. Hawaoni sababu ya msingi ya kuleta nyingine.
"Ndani ya katiba, yapo mambo makubwa na madogo, tutasikiliza wananchi wanataka nini, na kupeleka maoni yao bungeni ili yafanyiwe marekebishe. Suala katiba tutakwenda nalo taratibu," anasema.
Anaongeza kusema; " Katiba ya sasa haina matatizo makubwa kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakidai, ni marekebisho madogo tu, ndio maana hadi sasa ina viraka kama 15 tu. Maana yake ni kwamba inafaa, kwa hiyo tutaendelea kuweka viraka," anasema.
HUDUMA ZA JAMII
Mgombea huyo anasema serikali ya TLP itajenga nyumba za kutosha kwa ajili ya askari wa majeshi yote ili wasihangaike na maisha ya mtaani hali inayosababisha waonekane wa kawaida.
"Wakiwa kambini sio rahisi kuzoeleka kama ilivyo sasa, lakini pia wataweza kufanya kazi yao kwa haraka inapotokea dharura, kwa sababu watakuwa eneo moja la kuishi," anasema.
Aidha, chini ya serikali ya TLP, huduma za afya zitakuwa bure kwa Watanzania wote na pia hakutakuwa na mtindo wa kulipisha maiti fedha kama ilivyo kwa serikali ya sasa.
"Chama chetu kinataka kurudisha enzi ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere za kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wote siyo kwa makundi machache," anasema.
Anafafanua kuwa serikali iliopo madarakani inatoa huduma za afya bure kwa wazee, wajawazito na watoto, na kwamba wao hawatabagua. Kila Mtanzania atatibiwa bure na pia hakuna kutoza maiti, kwa maelezo kuwa uwezekano wa kutoa huduma hizo bure upo
"Ukweli ni kwamba bunge limekuwa likipitisha fedha nyingi, kwa ajili ya uboreshaji huduma za afya, lakini usimamizi wake umekuwa ni mdogo na kusababisha jamii kuingua kwenye gharama ambazo zingelipwa na serikali," anasema.
Anasema kukosekana kwa usimamizi wa fedha za umma kunasababisha zahanati, vituo vya afya na hospitali kutokuwa na dawa za kutosha, kwani hata wazee, wajawazito na watoto wanakosa dawa au kutozwa fedha, na kwamba TLP itakuwa makini afya za Watanzania.
Rwamugira anasema TLP inaamini kuwa utoaji huduma ya afya bure kwa Watanzania wote inawezekana, kwa maelezo kuwa fedha za kulipia gharama zote zipo, ila nyingi zinaishia mikononi mwa wajanja wachache.
Anataja mikakati mingine ya TLP kuwa ni kukomesha mikopo ya kausha damu na kuweka yenye riba nafuu ambayo kila Mtanzania atakuwa na uwezo wa kukopa na kurejesha bila maumivu.
"Lakini pia kwa upande wa wamachinga na madereva wa bodaboda na bajaji, tutawawekea mazingira mazuri ya biashara zao ili wasionekane kero kwa jamii kama ilivyo sasa," anasema.
Mgombea urais huyo anasema bodaboda na bajaji watakuwa na vituo maalum vya kufanyia kazi, huku wamachinga nao wakiwa na masoko yenye miundimbinu ya kutosha, sheria na miongozo ya kusimamia kazi zao.
VITUO MAALUM
Mbali na hayo, anasema kwa sasa kuna makundi ya wazee, walemavu na watoto wanaozagaa na kulala mitaani, kwamba wakiingia madarakani watachukulia tatizo hilo kwa uzito kwa kuwajengea vituo maalum
"Wananchi wakitupa ridhaa ya kuongoza nchi, tutajenga vituo vya kulelea makundi hayo kila mkoani ili wawe sehemu maalum na kuwahudumia kila kitu badala ya kuzagaa kama ilivyo sasa," anasema.
Katika ufafanuzi wake, anasema kwa upande wa watoto, vituo vyao vitakuwa na shule ili nao wapate elimu wajiandae kulitumikia taifa lao la baadaye badala kuwa watoto wa mitaani.
Anasema kuna bomu kubwa linalonyemelea taifa la kuwapo kwa watoto wengi wa mitaani ambao wasiposaidiwa mapema, wanaweza kuwa majambazi wasio na tija kwa taifa.
"Kwa sasa watoto na vijana wadogo wanalala mitaani katika vituo vya mabasi, chini ya madaraja na wengine nje ya baraza za maduka, hao wanaweza kujikuta wakiwa wahalifu wakubwa baadaye," anasema.
Anaeleza kuwa wengi wao wanatakiwa kuwa shule wakisoma, lakini badala yake wanazurura mitaani na ili kuwanusuru, TLP itaanzisha vituo vyao kila mkoa na kuweka shule ili wasome na mafunzo ya ufundi ili kuwaongezea ujuzi zaidi..
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED