MAJALIO KYARA NA TANZANIA NEXT LEVEL' Katiba mpya ndani ya mwaka mmoja,

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 05:00 PM Sep 17 2025
Majalio Kyara, mgombea urais wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU)
Picha: Maktaba
Majalio Kyara, mgombea urais wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU)

WAGOMBEA Urais kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wanaendelea kunadi sera na ilani za vyama vyao, katika kampeni, huku wakitoa ahadi kemkem kwa wapigakura ili wawachague.

Majalio Kyara, ni mgombea urais kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), ambaye naye anamwaga sera za chama chake kwa kufafanua kuwa ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake madarakani, serikali itaanzisha mchakato wa katiba mpya na kuukamilisha.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili jijini Dar es Salaam wiki hii, anasema Watanzania watapata katiba mpya ambayo mchakato wake ulikwamishwa na baadhi ya vyama vya siasa mwaka 2014.

"Suala la katiba mpya halina kizuizi, kinachotakiwa ni usimamizi tu, hivyo ndani ya wiki 40 au miezi 10 mwaka 2026, sisi tuhakikisha tunaipata kwani ndio mkataba kati ya mtawala na raia anayewaongoza ni muhimu ipatikane," anasema Kyara.

Anafafanua kuwa kila jambo watalifanya kwa kuzingatia sheria, uwazi na uwajibikaji na pia wataboresha sheria na ruzuku kwa vyama vyote vya siasa ili kutengeneza usawa na haki katika malezi ya vyama na demokrasia.

"Tunakusudia kupambana na rushwa na kukuza uongozi wenye maadili, kuleta fursa sawa kwa raia wote, bila kujali jinsi, kabila, dini, kulinda uhuru wa kitaifa na kupinga kuingiliwa na mataifa ya kigeni," anasema.

Mbali na hayo, anasema wakiingia madarakani watawezesha vijana wa kiume na wa kike kutengeneza fursa katika shughuli za uongozi na kiuchumi, kukuza kwa umakini usawa wa kijinsia kwa kuzingatia kundi la vijana wa kiume, kutoa ufadhili wa elimu na ushauri kwa wajasiriamali wachanga wanaotokana na makundi maaalum.

"Hilo litakwenda sambamba na ushiriki wao katika mipango na elimu ya mazingira, sera zinazowajumuisha wote, wa mijini na vijijini, kutoa vivutio na misamaha ya kodi kwa makundi haya," anasema.

Katika mwendelezo huo, anasema chama hicho kinakusudia kupanua wigo wa usawa wa kijinsia kwa kukuza haki, uwakilishi wa wanawake katika siasa, wawe wengi kwenye ngazi za maamuzi.

Kyara anasema katika ilani ya SAU , wameahidi kupanua wigo kwa kukuza haki za kijinsia ili wanawake wawe wengi kwenye ngazi za maamuzi na uongozi wa serikali kuu na za mitaa na katika mashirika na taasisi binafsi na za umma kwa kushika nafasi nyingi za uongozi.

"Tumeahidi kukomesha ukatili wa kijinsia kwa kuimarisha sheria ili kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia iwe nyumbani, kuondoa mila kandamizi zenye madhara hasa ndoa za utotoni na ukeketaji. Kaulimbiu yetu ni amani, uadilifu na maendeleo."

MIUNDOMBINU, UCHUKUZI

Anasema kila dola moja inayowekezwa katika miundombinu hususan ya msingi kama barabara, bandari, umeme na skimu za umwagiliaji tunahakikisha inazalisha dola tano katika ukuaji wa uchumi na kwamba kuweka kipaumbele kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali, usafirishaji na uchukuzi, kutaimarisha uchumi wa wananchi.

"SAU tunataka kuijenga Tanzania ya siku zijazo ambayo kila mwananchi atapata makazi bora na nafuu, usafiri bora kwa wananchi na bidhaa zao, kujenga barabara zinazopitika kipindi chote hasa vijijini," anasema Kyara.

Anaahidi kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa katika zabuni mbalimbali na kuweka ulazima wa ushirikishwaji wa wazawa katika zabuni ambazo amepewa mkandarasi mgeni katika utawala watalipa madeni kwa wakati kwa wakandarasi wazawa, kuboresha reli zilizopo na kuanzisha mpya, ikiwamo zinazounganisha nchi jirani kama ilivyo ya TAZARA.

"Tunataka kuhamasisha matumizi ya reli hasa katika kusafirisha shehena ili kuboresha uchumi, kupunguza msongamano, matumizi ya mafuta, matumizi ya fedha za kigeni na ajali za barabarani kutumia malighafi zilizopo nchini kufungua viwanda vya chuma kutengeneza vyuma vya reli na vifaa vingine vya ujenzi na kilimo kama matrekta," anasema.

Kyara  anasema serikali ya SAU itaanzisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutokea Bandari ya Dar es Salaam kuelekea mikoa mingine na mipakani has nchi jirani ili kuendelea kulinda na kutunza barabara na pia kupanua zaidi wigo wa kibiashara na nchi jirani.

VIPI KUHUSU ELIMU?

Mgombea Kyara anasema SAU inaamini kuwa elimu bora ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, na kwamba watawekeza katika elimu bora ili kupata wataalam bora watakaosaidia kukamilisha mipango mbalimbali ya maendeleo ya taifa.

"Uhaba wa walimu na vifaa vya kujifunzia ni kati ya vikwazo vikuu katika elimu, lakini pia mazingira mazuri ya kujifunzia kama maabara, madarasa, madawati na vyoo, hayo yote tutayashughulikia," anasema.

Anaongeza kuwa watakuza ushirikiano kati ya vyuo vikuu na viwanda ili kuoanisha mitaala na mahitaji ya soko la ajira na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali wakiwa shuleni. Ili kuongeza ujuzi na kuweza kufanya kazi kwa vitendo shughuli mbalimbali walizojifunza shuleni.

Jambo jingine wanalokusudia kulifanya ni kuhamasisha na kufadhili zaidi wanafunzi wa kozi za programu mbalimbali na pia kwa kutambua kwamba kuwa na uwiano mzuri kati ya wanafunzi na mwalimu ni kiashiria cha kupata elimu bora, wanakusdia kutoa ajira mpya kwa walimu, lengo likiwa ni kupata walimu wa kutosha ambao ni mahiri.

"Tunataka kufikia uwiano wa wanafunzi 20 hadi 29 kwa mwalimu kutoka kiwango cha sasa cha wanafunzi 53 kwa mwalimu. Kwa kuwa elimu ya awali ndio msingi wa elimu tutahakikisha elimu hiyo inaboreshwa na kuzingatiwa," anasema.

Aidha, anasema masomo ya hisabati, sayansi na TEHAMA yatapewa kipaumbele zaidi kwa lengo la kupata wataalam wengi wa baadaye ambao watakuwa na fani mbalimbali.

"Ilani hii ni mtiririko wa ahadi za chama kwa wapigakura na Watanzania wote. Inaonesha dira, maadili, sera na mipango ya chama katika kipindi cha miaka mitano ya utawala na kwa jinsi gani tutaweza kuwatumikia watu, kuboresha ubora wa maisha yao na kutatua changamoto zinazowakabili kwa miaka mingi kama umaskini, maradhi, ukosefu wa ajira, ukosefu wa miundombinu na nyingine nyingi,"anasema.

Anasema  SAU imekusudia kujenga taifa ambalo linafanya kazi kwa ajili ya wote, taifa ambalo hakuna mtu aliyeachwa nyuma na kwamba kwa pamoja tutafika mbali katika uongozi wao.