JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu tuliona kwamba, uwapo wa wanawake katika vyombo vya maamuzi pekee hautoshi kuwawezesha kufanya ushawishi wa mabadiliko yenye tija. Tuliangalia pia mazingira yanayohitajika ili ushiriki wao kwenye uongozi uweze kuzaa matokeo ya kweli. Katika safu yetu leo, tutaangalia nguzo imara kwa wanawake viongozi ili waweze kuwa chachu ya mabadiliko yenye maana na endelevu kwa jamii nzima. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira.
Uthubutu, maono na mshikamano nguzo imara kwa wanawake viongozi kufanya mageuzi ya kweli kwenye jamii.
Wote tunafahamu kuwa idadi ya wanawake nchini Tanzania walioko katika nafasi za uongozi wa kisiasa bado ni ndogo. Lakini taarifa njema ni kwamba licha ya uchache wao bado wana uwezo mkubwa wa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa iwapo wataongozwa na nguzo imara za uthubutu, maono, mshikamano, sauti moja, kujiamini na utayari wa kujifunza.
Ngoja tuanze kwa kufafanua kidogo neno uthubutu. Kwa maneno mepesi uthubutu ni hali ya kuwa na ujasiri wa kufanya jambo gumu hasa pale ambapo wengine wanaogopa au wanasita kwa sababu mbalimbali. Ni msukumo wa ndani unaomwezesha mtu kuchukua hatua bila uoga, hata kama kuna vikwazo, upinzani, mashaka au kukatishwa tamaa na watu wengine. Uthubutu ni sifa moja kubwa kwa mtu yeyote anayetaka kufanya mabadiliko ya kweli.
Ngoja tuangalie neno uthubutu kulingana na mada yetu ya wanawake katika uongozi wa kisiasa. Wote tunafahamu kwamba jitihada za wanawake katika uongozi wa kisiasa zinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za kiutamaduni, kiuchumi na kimfumo. Wanawake wanatakiwa kuwa na uelewa wa kutosha juu ya uhalisia wa mazingira yanayowazunguka na kutafuta namna bora ya kufanya kile walichopanga kukitekeleza bila kuogopa hoja za kuwakatisha tamaa na zenye mitazamo hasi dhidi yao.
Nguzo nyingine imara kuwasaidia wanawake kuleta mabadiliko yenye tija ni kuwa na maono. Tunaposema maono tunamaanisha uwezo wa mtu kuona au kutambua mambo makubwa, ya mbele na ya baadaye kwa mtazamo wa matumaini, mabadiliko au maendeleo. Ni dira au mwelekeo wa fikra unaomwongoza mtu kuelekea kwenye lengo fulani la muda mrefu. Maono hutokana na ndoto, imani, maarifa, au dhamira ya ndani ya kuona hali bora kuliko uliyonayo kwa wakati huo.
Kwa muktadha wa wanawake viongozi, licha ya idadi yao kwenye nafasi mbalimbali za maamuzi ni ndogo, kama wana maono, watafanikiwa kuchochea mabadiliko. Tukumbuke kuwa kiongozi mwenye maono ni yule mwenye malengo yenye mwelekeo wa maendeleo na anayeweza kujitolea kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kutimiza malengo yake. Wanawake wengi viongozi, hizo sifa wanazo na tumeshuhudia waadhi yao waibua changamoto na kusimama kidete kuhakikisha zinatatuliwa hata kama walikuwa na rasilimali kidogo.
Kuwa na mshikamano ni jambo lingine linaloweza kuwasaidia wanawake kufanya ushawishi wa kuleta maendeleo yenye tija, licha ya uchache wao. Watu wanaposhikamana, wanakuwa hawana ushindani usio na tija na hujenga usaidizi wa pamoja. Wakiwa na sauti moja katika ushawishi, huwa na uzito zaidi kuliko sauti ya mtu mmoja mmoja. Kadhalika kuwa na sauti moja, huonesha mshikamano wa kweli na huleta shinikizo la mabadiliko kwenye mifumo ya kijamii na kisiasa.
Suala lingine ambalo ni muhimu zaidi ni kujiamini. Ili kuweza kufanya ushawishi wenye tija, wanawake wanatakiwa kujiamini pale wanapotoa hoja zao na wanapofanya maamuzi magumu kwa faida ya muda mrefu kwa jamii. Inawezekana kabisa maamuzi hayo yasipokelewe vizuri na wengi. Mwanamke anayejiamini hatakiwi kuyumbishwa na hilo na badala yake anatakiwa kuendelea kuonesha ujasiri na msimamo ili mradi kile alichokifanya ni kwa maslahi ya jamii.
Kujifunza ni nguzo nyingine muhimu kwa viongozi wanawake. Ingawa kujifunza kunaonekana kama jambo jepesi, utekelezaji wake huwa si rahisi sana kwani ili kujifunza, mhusika anatakiwa akubali kuwa hujui kila kitu, awe tayari kupokea maoni, kusikiliza wakosoaji, na kurekebisha pale anapobaini mapungufu yake. Zaidi ya hayo, anatakiwa ajiweke katika mazingira ama nafasi ya kutafuta maarifa mapya na sahihi ili kuongeza thamani yake kama kiongozi lakini pia ufanisi katika majukumu yake.
Kuwa na maarifa yanayoendana na mabadiliko yanayoendelea katika jamii, ni silaha muhimu sana kwa wanawake viongozi kwani licha ya kuwajengea uwezo wa kufahamu mambo yanayowazunguka, huwapa nguvu ya kujiamini, ujasiri wa kutoa hoja na kuzisimamia, kufanya maamuzi bila hofu na kuzungumza kwa mamlaka na bila kuogopa kukoselewa. kuondoa hofu.
Kadhalika, maarifa mapya huwawezesha wanawake kuwa na uwezo wa kuchambua masuala muhimu yanayoendelea katika jamii zao, kutafuta njia sahihi za kuyatafutia ufumbuzi na mbinu za kushirikisha wadau katika kutatua kero sugu za wananchi kwa njia endelevu. Kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine waliofanikiwa katika uongozi ni sifa nyingine ya mtu mwenye maarifa.
Kila mwanadamu hukosea lakini kiongozi bora ni yule anayekubali ukosoaji na kufanyia marekebisho maeneo yenye udhaifu. Kutetea kila kitu hata pale unapojua fika kwamba unachokisema hakina mantiki, huo siyo usimamiaji wa hoja ninaousema mimi.
Bado naamini kuwa wanawake walioko kwenye nafasi za uongozi wa kisiasa japo idadi yao ni ndogo, lakini wana nafasi kubwa ya kuwa nguzo ya mageuzi ya kweli ya kijamii na kisiasa iwapo watakuwa na uthubutu, maono, mshikamano, kujiamini pamoja na moyo wa kujifunza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED