SIKU ya Mazingira Duniani, ambayo ni Juni 5 ya kila mwaka, inatumika kusafisha mazingira na kutoa elimu na faida za kuyatunza, kitu kilichofanyika hata mwaka huu.
Siku hiyo, taasisi na wadau wanaohusika na utunzaji mazingira wanaingia mtaani kusafisha mazingira na hata kutoa elimu ya namna ya kugeuza taka kuwa fursa.
Mwaka huu katika Mkoa wa Dar es Salaam, ukaja na mbinu mpya, ikinadiwa maeneo ya Mbweni na Kunduchi.
Hapo ulifanyika usafi uliosaidia kupatikana kwa taka ngumu zinazojumuisha chupa za maji, nguo zilizochakaa, rambo za plastiki pamoja na taka hatarishi.
Ofisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mkoani Dar es Salaam, Eston Waliha ni miongoni wa waliohudhuria shughuli hiyo.
Akawaalika wadau kutumia fursa iliyopo kwa chupa za plastiki ili kusaidia kuweka mazingira safi. Eston akafafanaua:
“Kuna viwanda vinavyosindika taka za plastiki, hivyo hakuna sababu ya kutafuta taka za plastiki kwenye fukwe zetu kuna fursa nyingi kwenye taka hizo ambazo, zinaweza kuchakatwa na kuwa bidhaa.
"Kuna kiwanda huko Kibaha kinasindika plastiki hadi kuzalisha pamba bandia, jambo ambalo halikuwapo zamani. Ni suala la wananchi kukusanya na kutenganisha taka hizi."
Anatoa takwimu za taka walizokusanya katika ufukwe wa Silversands Dar es Salaam, Joshua Mkoma kiongozi wa timu rasmi ya wazoa taka inayojishughulisha na utunzaji mazingira, anasema walikusanya zaidi ya mifuko 350 ya taka yenye uzito wa kilo 2835, ni sawa na takriban tani tatu zilizolewa.
"Tulikusanya mifuko ya taka 350 yenye uzito wa kilo 2,835, ambayo ni sawa na karibu tani tatu. Hii ni sawa na kuzuia zaidi ya tani nane za uzalishaji wa ‘carbon dioxide’ (hewa ya kaboni).
"Hatua hii ni uthibitisho wa kile kinachotokea wakati vijana, jumuiya, na mashirika yanapoungana. Asante sana kwa washirika wetu wote, wafanyakazi wa kujitolea, na wanafunzi ambao wamewezesha hili.
"Siku ya Usafishaji Duniani ni ukumbusho kwamba mabadiliko ya mazingira huanza na hatua za pamoja. Kwa kuungana katika ufukwe wa Silversands, tunathibitisha kwamba hata hatua ndogo, zikizidishwa na mamilioni, zinaweza kubadilisha sayari yetu.
"Ni zaidi ya shughuli ya siku moja; ni sehemu ya harakati zinazokua za kulinda rasilimali za bahari ya Tanzania kupitia uongozi wa vijana, ushirikishwaji wa jamii, na elimu ya ubunifu," anasema Joshua
Carlos Mdemu, kutoka shirika lingine la kutetea mazingira, anasema kuwa bila ya ushirikishaji jamii, usimamizi wa taka utakuwa mgumu kwa sababu ya kukosekana maelewano ya pamoja katika utunzaji mazingira
Hapo mahsusi, anagusa maeneo ya pwani, ambako yanaonekana kutokuwa na wamiliki,hivyo kukosekana watu wa kuzisafisha.
“Tunahimiza jamii kuelewa suala la usafi wa mazingira, hasa katika maeneo ambayo yanaonekana hayana wamiliki kama vile fukwe, mito, maeneo ya wazi.
“Leo tunaangalia hasa maeneo hayo, ndiyo maana tunawashirikisha wanafunzi, kwa sababu tunajua kupitia kwao, elimu itaenea kwa jamii na watajifunza umuhimu wa mazingira tangu wakiwa shuleni,” anasema Carlos
MFUMO TAKA SIFURI
Nadharia ya ‘mfumo wa taka sifuri’ safari ikagonga hodi katika kitongoji cha Mbweni ambako taasisi zinazojihusisha na utunzaji mazingira, zinafika eneo hilo kuadhimisha kwa kusafisha mazingira.
Mfumo huo wa ‘taka sifuri’ unahusisha kuzigawa taka katika makundi kuanzia nyumbani, ili iwe rahisi kuzirejeleza na kupata kitu kingine kitakachokuwa na thamani. Kama vile mbolea na chakula cha kuku.
Ofisa Hamasa wa asasi hiyo, Marco Doto, anasema kutumia mfumo wa ‘taka sifuri’ kudhibiti taka, kunasaidia jamii kuepeuka magonjwa ya mlipuko.
"Hii ni sehemu ya kuikumbusha jamii juu ya utunzaji wa mazingira na kufanya mfumo wa ‘taka sifuri’, lakini tunawaelimisha wananchi waweze kutenganisha taka vizuri kuanzia nyumbani.
“Halafu baada ya hapo zitakuwa zinachukuliwa na kupelekwa katika kituo Cha uchakataji taka tunachotarajia kukijenga hapa Mbweni," anasema Doto
Anaeleza kuwa mfumo huo wa taka sifuri utaleta manufaa kwa kuwa utasaidia kufanya mazingira yabaki safi, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.
WASIMAMIZI WA MAZINGIRA
Mwamini Mkunda, Ofisa Afya Kata ya Mbweni, anasema kutofanya usafi kila mara, hatari yake ni kuhatarisha ongezeko la magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Hivyo, anatoa wito kwa wakazi wa Mbweni, kufanya usafi kila siku na sio kusubiri siku maalum tu.
Mkaguzi wa Mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aban Mngebusa, anawataka wakazi hao kujitahidi kila nyumba iwe na chombo cha kutunzia taka ili iwe rahisi kubebwa na kwenda kutupwa dampo.
WASEMAVYO WAKAZI
Mkazi wa Maputo Mbweni, Juma Zakaria, ni miongoni mwa walioshiriki katika usafi huo, anautaja kuwa mzuri, kuungana na taasisi hiyo kufanya usafi pamoja kwa kuwa wamepatiwa, pia elimu ya namna ya kutenganisha taka katika makundi manne.
Zakaria anasema kitendo kilichofanywa na taasisi hiyo, ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine zinazohusika na mazingira kwa kuwa bado wapo wasiofahamu umuhimu wa kufanya usafi.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Mariam Mwakibete, anasema kwa kufanya usafi pamoja na taasisi hiyo inayojihusisha na usafi wa mazingira, amepata elimu kwamba kumbe inawezekana taka kuwa fursa au chanzo cha kupata fedha.
"Nimejua kuwa kumbe kupitia taka unaweza kupata fedha! Nilikuwa sijui kabisa hili, kumbe ninaweza kutengeneza mbolea na chakula cha kuku na nikapata fedha imekuwa jambo kubwa sana kwangu" anasema Mwakibete
Katika maeneo mengi ya Dar es Salaam, Nipashe imeshuhudia watu wanaofanya usafi kwenye mifereji iliyo kando ya barabara na hata katika fukwe za bahari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED