OKTOBA mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ambao utakuwa ni uchaguzi wa saba tangu kuanza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mwaka 1995 ambayo sasa imebadilishwa kisheria na kuitwa Tume Huru ya Taifa Uchaguzi (INEC).
Aidha, Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania hufanyika kila baada ya miaka mitano kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu wa Rais, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Diwani kwa upande wa Tanzania Bara.
Uchaguzi huo hufanyika kwa kuzingatia Ibara ya 38 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977, imeweka taratibu na masharti yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeratibu na kusimamia uchaguzi mkuu mara sita ambao ni wa mwaka 1995, 2000, 2005,2010, 2015, 2020.
Tanzania inatumia Mfumo wa Uchaguzi ambao mgombea anayepata kura nyingi halali kuliko mgombea mwingine yeyote hutangazwa kuwa mshindi ambayo ni kwa mujibu wa Ibara ya 41 (6) ya Katiba.
Mfumo mwingine unaotumika ni wa uwiano wa kura unaotumika kupata wabunge wanawake wa viti maalum ambao umetajwa kwenye Ibara ya 78 (1) ya Katiba, ambao pia hutumika kuwapa madiwani wanawake wa viti maalum kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 112 na 113 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.
Aprili 12, 2025 vyama vya siasa vitaakvyoshiriki uchaguzi mkuu mwaka huu vitasaini Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024 ambazo ziliwekwa kwenye tovuti ya INEC Mei 20,2025, za Tangazo la Serikali Na 390 la Mei 17,2024.
Kanuni hizo ni za Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi No 2 ya mwaka 2024, zenye sehemu tis ana vipengele 24 ambavyo ni masharti ya utangulizi, masharti kuhusu INEC, kamati ya usaili, sekretarieti ya kamati ya uchunguzi, ugawaji majimbo, maadili ya utendaji ya tume, watumishi na watendaji wa tume, wajibu wa kutoa elimu ya mpigakura kwa wananchi, na masharti mengineyo.
Uchaguzi hufanyika kila baada ya miaka mitano na shughuli zake ambazo hufanywa na INEC hugawanyika katika sehemu tatu ambazo ni kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Shughuli zinazofanyika wakati huu ni uandaaji wa bajeti; uandikishaji wa wapiga kura;ununuzi wa vifaa;uandaaji wa kalenda na mpango wa utekelezaji;marekebisho ya sheria na maelekezo ya watendaji na wadau wa uchaguzi;mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi; kutoa elimu ya mpiga kura; na wakati wa uchaguzi.
Katika hatua hii kinachofanyika ni Katika awamu hii, uteuzi wa wagombea; uratibu wa kampeni za wagombea, utekelezaji wa kamati za maadili;usajili wa watazamaji wa uchaguzi;kuchapa na kusambaza karatasi za kura;kusambaza vifaa vya uchaguzi;upigaji kura; kuhesabu kura; na kutangaza matokeo.
Aidha, katika hatua hiii kinachofanyika ni tathmini baada ya uchaguzi mkuu;kushughulikia kesi za uchaguzi; na kuandaa taarifa ya uchaguzi mkuu, marekebisho ya sheria za uchaguzi;kupitia na kuboresha Daftari la Wapiga Kura;kupitia na kuboresha mifumo ya uchaguzi.
Mengine ni kupitia na kuboresha mipaka ya majimbo ya uchaguzi;kupitia na kuboresha muundo wa tume;ukaguzi wa matumizi ya fedha na vifaa vilivyotumika katika uchaguzi mkuu;kupitia mpango mkakati; na kuandaa mpango kazi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata.
Kwa upande wa Zanzibar chini ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wanachagua Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na madiwani wa kwenye wadi. Huku INEC ikiratibu na kusimamia uchaguzi wa Rais na wabunge kutoka Kisiwani humo kwenda Bunge la Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED