Misitu inapokuwa kinara mchango wa pato la taifa

By Dk. Felician Kilahama , Nipashe
Published at 05:14 PM Sep 23 2025
Misitu inapokuwa kinara mchango wa pato la taifa
Picha: Mtandao
Misitu inapokuwa kinara mchango wa pato la taifa

MISITU kwa kiasi kikubwa, huhifadhi mazingira na kuimarisha hali ya hewa na zaidi kuchangia kufanikisha uzalishaji mali kwenye sekta nyingine za uchumi. Kwa mfano, kilimo, chakula, nishati, mifugo, uvuvi, wanyamapori, maji, utalii, afya na elimu.

Hata hivyo, huduma za kiikolojia zitokanazo na rasilimali misitu, kwa miongo kadhaa, zimekuwa hazithaminishwi kifedha kwenye uchumi ngazi za kitaifa.

Uzoefu unaonesha kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imekuwa ikitoa taarifa kila mwaka kuhusu mchango wa rasilimali misitu kwenye pato la taifa lakini kwa kutumia asilimia ndogo, huduma za mifumo ikolojia sekta ya misitu ambazo haziko kibiashara zimekuwa hazijumuishwi kama sehemu ya mchango wa misitu katika pato la jumla la taifa yaani `Gross Domestic Product’ (GDP).

Hata hivyo, misitu, kwa miaka mingi, imekuwa ikionekana kama haina umuhimu unaaonekana licha ya kwamba inategemewa kama chanzo muhimu kuyamudu maisha ya wananchi wengi vijijini na mjini. 

Hivyo, mfumo wa NBS kuweka bayana thamani michango ya sekta mbalimbali kwenye pato la jumla (GDP), umekuwa ukizingatia zaidi mapato ya misitu kutokana na mazao ya bidhaa zilizouzwa. 

Utaratibu huo umekuwa hautilii maanani huduma ikolojia misitu. Kwa miaka kadhaa, wataalamu wa misitu wamekuwa wakieleza kukosekana uthamanishwaji ikolojia misitu ili thamani yake iwe sehemu ya mchango kwenye GDP. Hata hivyo, sauti hizo hazipenyi kutokana na kutofautiana kimitazamo kitaaluma na kisiasa.

Hoja kuu kuhusu michakato ya huduma ikolojia ambazo haziko rasimu kibiashara; inahusisha masuala kama vile misitu na virutubisha ardhi au udongo, kuhifadhi vyanzo vya maji, kudumisha bayoanuwai na hifadhi ya kaboni.

Mathalani, katika mazingira yenye misitu asilia inakuwa rahisi kudhibiti mvua na kuwezesha maji yasipotee bali yaweze kuingia ardhini na wakati huo, misitu ikirutubisha udongo pamoja na kuhifadhi viumbehai pia kutunza makazi ya wanyamapori na kupunguza kaboni angani hivyo kupunguza athari za mabadiriko tabianchi. 

Hata baharini sehemu zenye misitu ya mikandaa au mikoko hakuna athari mbaya za mawimbi makubwa, wala tsunami pia ni mazalio ya samaki ambao ni chanzo cha mapato na kukua uchumi.

Kadhalika, rasilimali bioanuwai zilizomo kwenye msitu mfano nyuki huweza kufanya uchavushaji ipasavyo na kuimarisha uzalishaji mazao shambani wakati wanapotafuta nekta’ kutengeneza asali. Isitoshe, bioanuwai huweza kudhibiti wadudu, kusambaza mbegu ikiwa pia ni vivutio kwa utalii ikolojia. 

Kwa mazingira yenye misitu asilia inayosimamia vizuri kuna uwezekano mkubwa kutoa huduma kamili za ikolojia ikilinganishwa na misitu isiyosimamiwa ipasavyo. 

Huduma ikolojia zitokanazo na misitu ni muhimu mathalani, asilimia 80 ya uzalishaji umeme ni kwa kutumia maji kupitia mabwawa ya Kidatu, Mtera (Mto Ruaha Mkuu) na bwawa Nyerere, kwenye Mto Rufiji.

Masuala mengine muhimu ni kama misitu kuhifadhi udongo, kupunguza kaboni hewani; kuwezesha upatikanaji maji kwenye mito mwaka mzima kwa ajili ya umwagiliaji mazao shambani na uchavushaji.

Huduma hizi muhimu kutokana na ikolojia misitu zinanufaisha sekta karibu zote mfano kilimo, nishati, uvuvi, na ufugaji. Kwa kuwa mbinu za sasa zinazotumika kubainisha mchango wa misitu katika GDP zinategemea zaidi bidhaa zinazouzwa; ikaonekana kuna ulazima wa kuhakikisha huduma ikolojia misitu zinawekwa bayana kwa faida za kiuchumi. 

Kwa mujibu wa NBS (2023), mchango wa sekta ya misitu katika pato la jumla, kati ya 2010 na 2023, ulikadiriwa kuwa kati ya asilimia 2.2 na 4.0.

Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT) kuanzia 2019 hadi 2021), iligharamia utafiti kuhusu mchango wa misitu kwenye uchumi bila kuhusisha huduma ikolojia misitu na kuripoti mchango wa asilimia 3.3 katika pato la jumla la taifa. 

Kwa hiyo, ripoti za NBS na MNRT zilithaminisha mchango wa misitu kwa kutumia viashiria vya kawaida vya kiuchumi kama vile ajira na mapato yanayotokana na bidhaa misitu zilizouzwa. 

Kwa kuwa mbinu za kawaida hazizingatii huduma za mifumo ikolojia katika hesabu za pato la taifa; iliilazimu serikali kupitia MNRT kufanya utafiti zaidi ili kubaini uhalali wa huduma-ikolojia katika kuthaminisha mchango halisi wa misitu kwenye pato la jumla la taifa (GDP).

Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ilifanya utafiti kuweka bayana mchango wa huduma ikolojia zitokanazo na uwepo wa misitu asilia maeneo mbalimbali nchini. Kadhalika, uthaminishwaji huduma ikolojia ulilenga kupata thamani yake kifedha ili kupata msingi wa uhakika kitaaluma kuweza kuwashawishi watumiaji rasilimali misitu na au wafanya maamuzi watambue kikamilifu thamani yake na hatimaye waweze kufanya maamuzi yenye uelewa wa kutosha mtazamo chanya pia kuweza kutoa kipaumbele kudumisha uhifadhi misitu asilia kwa manufaa ya wengi.

Kwa ujumla, utafiti ulitumia utaratibu wa kuthaminisha uhifadhi mazingira unaofahamika kama uhasibu kijani au green accounting. Takwimu zilikusanywa kutoka mikoa 17 ikiwa ni asilimia 65 ya mikoa ya Bara yenye rasilimali misitu na huduma ikolojia toshelezi ya Arusha, Dodoma, Dar-Es-Salaam, Iringa, Katavi, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mbeya, Njombe, Morogoro, Pwani, Ruvuma, Singida, Tabora, na Tanga.

Utafiti ulijikita katika maeneo saba muhimu ya huduma za mifumo ikolojia misitu mathalani, kubainisha uhifadhi wa kaboni; uhifadhi ardhi na kurutubisha udongo; uhifadhi viumbehai misituni; mchango wa kiuchumi kupitia uhifadhi maji (kupitia misitulindimaji); mchango kiuchumi kupitia kuondoa kaboni hewani; mchango kiuchumi kupitia utalii ikolojia na faida kitamaduni pamoja na mchango kiuchumi kupitia huduma uchavushaji mazao sekta ya kilimo.

Matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Misitu (NAFAC) ya MNRT wakati wa mkutano wa Bodi ya TAFORI Juni mwaka huu, watafiti kutokavyuo vikuu vya SUA na UDSM; waliwasilisha matokeo ambayo kwa kupitia taratibu za uhasibu kijani; kwa mara ya kwanza tangu uhuru waliweka bayana uhalisia wa mchango wa huduma zitokanazo na ikolojia-misitu katika pato la jumla la taifa.

Inatia moyo kwamba kupitia utafiti uliofanyika tumeweza kuthibitisha thamani yake hivyo kubainisha huduma ikolojia misitu kuchangia asilimia 16.73 kwenye pato la jumla la taifa. Hakika, ni mchango mkubwa ambao hauonekani kifedha lakini muhimu kwenye maendeleo ya uchumi nchini. Haya ni matokeo ya ‘mbinu za uthaminishaji kijani’ utaratibu ambao haujawahi kutumiwa nchini, ingawa umekuwa ukitumiwa na nchi nyingine kama China. 

Hivyo, takwimu hizo zikijumuishwa pamoja na asilimia 3.3 kama mchango wa misitu wa sasa kwenye pato la jumla; inafanya mchango halisi wa misitu kufikia asilimia 20.03 hivyo, kuweka bayana thamani na umuhimu wa rasilimali misitu nchini.

Matokeo kuhusu thamani ya ikolojia misitu kwa kutumia uthamanishaji kijani yanapaswa kuwawezesha watunga sera na wafanya maamuzi kutafakari kwa kina kuhusu huduma ikolojia misitu ili kuimarisha uendelevu wa rasilimali misitu.

Kutokana na matokeo haya na kuweza kufikia mwafaka kitaifa, inashauriwa serikali na wadau  kukomesha mara moja, shughuli zinazosababisha huduma ikolojia misitu kuzorota. Kwa mfano, ukataji miti,uharibifu wa misitu kupitia kilimo cha kuhamahama, ukataji, ufyekaji miti, misitu ovyo na uchomaji misitu, mapori nyakati za kiangazi, inabidi masuala haya yadhibitiwe ipasavyo. 

Kulingana na takwimu zilizopo, kiwango cha upotevu wa rasilimali misitu ni takriban hekta 470,000 kila mwaka, jambo ambalo linatishia huduma za misitu ikolojia.

Thamani ikolojia kupitia rasilimali misitu katika pato la jumla la taifa, inathibitisha umuhimu wa kuhifadhi misitu asilia kuliko kuibadilisha kwa matumizi mengine. Wizara zinapaswa kubuni mifumo inayoweza kutumika kuwezesha walengwa wote kuchangia katika uhifadhi-misitu. 

Kwa mfano, kuanzisha malipo ya huduma ikolojia (PESS) kwa kuzingatia faida kiuchumi na mitazamo chanya ikiwemo utashi-kisiasa. Pamoja na hayo, wizara inapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha NBS, kila mwaka inapata takwimu sahihi kuhusu mchango wa misitu kwenye uchumi nchini kwa kujumuisha mchango huduma ikolojia misitu kupitia takwimu za uthaminishaji kijani na nyinginezo. Kwa sasa thamani iliyotokana na utafiti huu, ichukuliwe kwa uzito wake kama msingi wa kuanzia na kuendeleza kazi hiyo.