Mwanamke kuwa kiongozi pekee, haitoshi, yawepo mazingira wezeshi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:54 PM Sep 24 2025
Mbunge wa zamani ( Viti Maalum CCM), Al -Shaimaa Kweigyir, ameonesha kuwa mazingira wezeshi kama kuwaibua, kuwapa nafasi wenye mahitaji maalumu na kutumia vipawa vyao kunaibadilisha jamii
Picha; Mtandao
Mbunge wa zamani ( Viti Maalum CCM), Al -Shaimaa Kweigyir, ameonesha kuwa mazingira wezeshi kama kuwaibua, kuwapa nafasi wenye mahitaji maalumu na kutumia vipawa vyao kunaibadilisha jamii

JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu, tuliona jinsi ambavyo wanawake wanaochukua nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali wanavyotumia uzoefu na uelewa mkubwa walionao katika changamoto zilizoko katika jamii zao, kufanya ushawishi unaolenga katika kuleta mabadiliko yenye tija kwa jamii nzima.

Katika safu yetu leo, tutaangalia mazingira wezeshi kwa wanawake viongozi kufanya ushawishi wenye matokeo chanya na endelevu. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira.

Kuchukua uongozi peke yake haitoshi, wanawake wanahitaji mazingira wezeshi kushawishi mabadiliko ya kweli na endelevu 

Uhusiano kati ya ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi na uwezo wao wa kushawishi mabadiliko yenye tija si jambo geni masikioni mwa wengi.

Watu wengi wamewahi kusikia, na wanakubaliana na dhana kwamba mtu anapopata nafasi ya kuwa sehemu ya chombo cha maamuzi, ni fursa kubwa ya kuibua changamoto zinazowakabili wananchi na kutoa hoja zenye uzito kwa ajili ya kuhimiza mabadiliko ya sera, sheria au mifumo ya kijamii.

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba uwapo wa wanawake katika vyombo vya maamuzi pekee hakutoshi kuhakikisha ushawishi wenye tija.

Mafanikio yao katika nafasi hizo hayawezi kupatikana moja kwa moja bila juhudi maalum. Badala yake, yanahitaji kuwepo kwa mazingira mahsusi na ya kuwezesha ambayo yataimarishwa kwa makusudi ili kuhakikisha ushiriki wao unazaa matokeo ya kweli, yenye maana na endelevu kwa jamii nzima.

Ili uwapo wa wanawake katika vyombo vya maamuzi uweze kuleta ushawishi wenye tija, ni lazima kuwe na mchanganyiko wa mazingira ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yanayowawezesha kushiriki kwa usawa na ufanisi.

Katika mazingira ya kisiasa na kijamii, mwanamke hahitaji tu nafasi ya kuongoza anahitaji mazingira rafiki, uelewa wa kijinsia, na msaada wa kimfumo ili aweze kufanya ushawishi wenye maana. 

Ushawishi wa mwanamke haujengwi tu kwa kauli au cheo, bali kwa mchanganyiko wa vitu kadhaa muhimu vinavyomwezesha kusikika, kueleweka, na kuheshimiwa.

Kadhalika, ili mwanamke aliye kwenye nafasi ya uongozi aweze kuwa na ushawishi wenye tija, anatakiwa awe na uelewa wa kina kuhusu masuala anayoyasimamia, pamoja na ujasiri wa kusimama na kutoa hoja zenye uzito, zinazojengwa juu ya maarifa, uzoefu na uhalisia wa maisha ya jamii anayoiwakilisha. Uwezo huu wa kutoa hoja zenye mashiko ndio msingi wa kuaminika, kusikilizwa, na kuleta mabadiliko ya kweli katika vyombo vya maamuzi.

Pia ni lazima awe na nguvu ya kijamii inayoendana na dhamana ya nafasi hiyo.Hii inajumuisha uungwaji mkono wa jamii inayomzunguka pamoja na kuwapo kwa mitandao ya wanawake wengine viongozi au watetezi wa haki za wanawake. Msaada huu wa kijamii humpa mwanamke ujasiri wa kusimama imara katika mijadala ya sera na maamuzi, huku akijua kuwa hana mzigo wa kupambana peke yake, bali ana jamii inayomtazama kama mwakilishi wa matumaini ya pamoja.

Kufanya kazi kwenye mazingira rafiki ya kijamii na kimaadili ni suala lingine linalompa mwanamke amani na ari ya kufanya kazi kwa bidii. Mazingira yaliyo rafiki kwa mwanamke hayana mitazamo hasi, hayana kubezwa na kushambuliwa kwa misingi ya jinjia.

Badala yake wanawake wanathaminiwa na wanaheshimiwa, hali ambayo huwapa nguvu ya kujiamini na kusimamia agenda zao bila hofu. Hali hiyo pia huwapa vijana wa kike mifano mizuri ya kuiga, kitu ambacho hukuza kizazi kijacho cha wanawake viongozi.

Kuwapo kwa usawa wa fursa kati ya viongozi wa kike na wa kiume, hasa katika maeneo muhimu kama upatikanaji wa taarifa, rasilimali, na majukwaa ya kutoa maoni, ni suala lingine muhimu katika kumwezesha mwanamke kiongozi kufanya ushawishi wenye tija.

Mara nyingi wanawake hushindwa kuibua na kutoa hoja za nguvu kuhusu jambo fulani si kwa sababu hawana uwezo, bali kwa sababu wanakosa taarifa sahihi kwa wakati, rasilimali za kutekeleza majukumu yao ipasavyo na pia wengine wanabaki nje ya `majukwaa’ rasmi na yasiyo rasmi ambayo mijadala na maamuzi makubwa hufanyika.

Kuwapo kwa mazingira mazuri ya kisera na kisheria yanayolinda haki za wanawake huwapa ujasiri wa kusimamia hoja bila hofu wala mashaka. Misingi hii ya kisheria ni muhimu kwa kumhakikishia usalama wa kimazingira, uhuru wa kujieleza na ulinzi dhidi ya vitisho, unyanyasaji au ukandamizaji wa kijinsia unaoweza kujitokeza anapotekeleza majukumu yake.

Bila sera madhubuti zinazolinda haki za wanawake katika uongozi, wanawake wengi hujikuta wakinyamazishwa au kuwekewa vizingiti visivyo rasmi vinavyowazuia kuleta mabadiliko. Kwa mfano, ukosefu wa sheria kali dhidi ya lugha za matusi na udhalilishaji kwa wanawake kwenye majukwaa ya siasa na mitandaoni huchochea hofu na kuua ujasiri wa wanawake wengi wenye nia ya kushiriki kwenye maamuzi ya umma.

Kwa hiyo, kuwepo kwa mfumo thabiti wa kisera na kisheria ni zaidi ya kulinda heshima ya mwanamke ni msingi wa kumuwezesha kuwa kiongozi jasiri, mwenye sauti, na anayeweza kutetea ajenda za kijamii kwa uhuru na kwa tija.

Kwa kuzingatia haya yote, mwanamke kiongozi anakuwa na nafasi bora ya kushiriki katika maamuzi ya kitaifa na kijamii, kuibua mijadala ya msingi, na kusukuma mbele ajenda zenye manufaa kwa wanawake, vijana, na jamii kwa ujumla.

Ndiyo maana inabidi tuelewe kuwa wanawake kuchukua uongozi na kuwa kwenye vyombo vya maamuzi, peke yake haitoshi kuwawezesha kufanya ushawishi wenye tija. Lazima waungwe mkono na kuwekewa mazingira yanayofanikisha mipango yao.