Mwinyi atangaza mkakati kuirejeshea karafuu heshima

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:01 PM Oct 01 2025
Wananchi Pemba wakianika karafuu.
Picha: Rahma Suleiman
Wananchi Pemba wakianika karafuu.

KARAFUU inabaki kuwa uti wa mgongo wa uchumi na utambulisho wa Pemba, ambako familia nyingi hutegemea kilimo hicho kwa maisha ya kila siku.

Ni zao linaloipa jina kubwa kimataifa, zikisafirishwa hadi Ulaya, Mashariki ya Kati na Asia na kutumika kuzalisha manukato, tiba ya binadamu na viungo vya vyakula.

Zanzibar inatambulika duniani kama “nyumba ya karafuu”, Pemba ikiubeba umaarufu wa kipekee kwa ubora na wingi wa zao hilo.

Kwa vizazi vingi, karafuu imekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa familia na serikali, kugharamia elimu, afya, makazi na hata shughuli za kijamii.

Hata hivyo, kwa muda mrefu wakulima wa karafuu wamekuwa wakilima kwenye mashamba yasiyo na hatimiliki rasmi, kukosa usalama wa ardhi na fursa za kifedha.

Katika kampeni zake, mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anaahidi mabadiliko makubwa katika zao hilo akianza na hatimiliki za mashamba ya karafuu kwa wananchi.

Kwenye mikutano yake ya kampeni kisiwani Pemba Dk Mwinyi anasema wakulima wa karafuu wamekuwa uti wa mgongo wa uchumi Zanzibar kwa muda mrefu, lakini mara nyingi wanakabiliwa na changamoto za kutokuwa na usalama wa umiliki wa mashamba yao.

“Kila mkulima atapatiwa hatimiliki ya shamba lake. Hili litawaongezea heshima, usalama na uwezo wa kutumia mashamba kama dhamana ya kupata mikopo ya maendeleo,” anaahidi Dk. Mwinyi

Aidha, atatoa hatimiliki kwa wananchi wote waliopewa mashamba ya karafuu na serikali ili wayatunze.

“Baada ya kupewa hatimiliki yatakuwa yenu na hata urithi kwa watoto wenu ndiyo njia pekee ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo,”anasema mgombea wa urais wa Zanzibar.

Dk. Mwinyi anaongeza kuwa serikali yake ikichaguliwa, itaimarisha pia upatikanaji miche bora ya karafuu, kuanzisha viwanda vya usindikaji na kusaka masoko mapya ya kimataifa.

Kwa wakulima wa karafuu Pemba, kauli ya mgombea imeibua matumaini mapya ya kuimarisha urithi wao na kuendeleza Zanzibar kama kitovu cha karafuu duniani.

Wakizungumza na Nipashe baadhi ya wakulima wanasema wakipatiwa hatimiliki itakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto wanazokabiliana nazo kwa miaka mingi.

Mkulima Mohammed Ali Kombo mkazi wa Kalani shehia ya Mgagadu Mkoani Pemba, anasema wanalima zao hilo lakini hawana uhakika wa kesho yake hivyo kupewa hatimiliki na nguvu ya kweli kulinda mashamba yao na kuendeleza maisha.

hHatua hiyo itawasaidia vijana kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha karafuu. “Hii ni nafasi ya vijana kuingia kwa nguvu kwenye kilimo. Tukipata mikopo kwa dhamana ya mashamba, tunaongeza uzalishaji na kutengeneza ajira mpya.” 

Anasifu kuwa itafanikisha kupanga mipango bora ya matumizi ya ardhi na kulinda mashamba ya karafuu dhidi ya uingizaji wa shughuli zisizo rasmi zinazoharibu mazingira.

Aidha, hatua hiyo ya serikali imeonesha dhamira ya kuwatambua wakulima wadogo kama mhimili muhimu wa maendeleo ya kilimo na uchumi wa Zanzibar.

Anasema kwa sasa uzalishaji umepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na athari za mabadiliko ya tabiayanchi.

"Hivi sasa kuna upungufu wa mvua hivyo uzalishaji ni mdogo na kutokana na hali ya hewa ya jua kali karafuu zinasinyaa zikiwa changa na hazistawi,” anasema mkulima huyo.

Juma Ayoub Khamis, mkulima anayeishi Kalani Pemba anasema ni hatua ya kuungwa mkono jitihada za serikali  kwa kulipa kipaumbele zao hilo ambalo lina mafanikio makubwa katika maisha ya kila siku.

Ikiwa serikali italiangalia upya zao hilo kwa kuliongezea thamani zaidi ili lizidi kuwanufaisha, kuanzia kuwapatia hatimiliki ya mashamba ni jambo jema, akisema wapo baadhi ya wanaoingia kwenye mashamba yasiyo yao.

Anadai wapo wanaotengeneza nyaraka za kughushi hasa katika mashamba ya serikali na kuyakodisha wakulima na kuchukua fedha bila wenyewe kujua.

Anashauri serikali kuweka utaratibu wa kuwa na mfumo wa kuandaa hatimiliki ya karafuu ili kuondosha changamoto ya watu kuvamia mashamba hayo hasa msimu wa mavuno.

"Kutoa hatimiliki ni jambo jema na litaepusha watu kuvamia mashamba ambayo sio yao hasa wakati kama huu wa mavuno”anasema.

Talib Mohammed Bakar mkazi wa Shemkani anaona kupewa hatimiliki ya mashamba kutaondosha vitendo vya dhulma.

Aidha, anashauri serikali kufanya utafiti wa mashamba ya karafuu na kila mwenye shamba la asili la kurithi kufahamu wa kukabidhiwa nyaraka halali za umiliki.

Wataalamu wa kilimo wanasema kutoa hatimiliki kwa wakulima kutaimarisha sekta ya karafuu na utaratibu huo utapunguza migogoro ya ardhi, kuongeza uwekezaji wa wakulima na kuweka mazingira ya uzalishaji wenye tija.

Ali Khamis Juma Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, anazitaja faida za hatimiliki ya mashamba ya karafuu kuwa ni usalama wa umiliki ambao mkulima atakuwa na uhakika kuwa shamba ni mali yake halali, jambo linalopunguza migogoro ya ardhi.

Anasema pia itarahisisha upatikanaji wa mikopo kwa sababu inatumika kama dhamana ya kupata mikopo kutoka benki na taasisi za kifedha, jambo litakalowawezesha wakulima kuongeza uwekezaji wao.

Aidha, kutaongeza uzalishaji wa zao hilo ambapo wakulima wenye uhakika wa umiliki huwa na motisha zaidi kupanda miche mipya, kutumia mbolea na mbinu za kisasa.

“Umiliki wa hatimiliki ni urithi wa vizazi, jambo linaloongeza thamani ya mali ya familia”anakumbusha Juma.

Kama mpango huu utafanikiwa, sekta ya karafuu inaweza kuleta mageuzi makubwa kiuchumi, wakulima wakiwekeza zaidi, uzalishaji utaongezeka na Zanzibar itaendelea kuongoza duniani kwa ubora wa karafuu lakini pia serikali itaongeza mapato kupitia kodi na mauzo ya karafuu na bidhaa zake.

Ajira mpya zitaibuka kupitia viwanda vya usindikaji na biashara za ndani na nje ya nchi.

Ahadi ya Dk. Mwinyi ya kutoa hatimiliki kwa wakulima ni hatua ya kihistoria ya kulinda urithi na kubadili maisha ya Wazanzibari ikiwa utekelezaji utasimamiwa kwa umakini.

Pemba na Unguja zinaweza kuibuka upya kuwa kitovu cha karafuu duniani na wakulima kufaidika kulingana na jasho lao.