Pacha wa Mandela tangu 1941 hawakuachana hadi kifo 2003

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:12 PM Apr 10 2025
Walter Sisulu (kushoto) na Nelson Mandela
Picha: Mtandao
Walter Sisulu (kushoto) na Nelson Mandela

WATANZANIA wanamfahamu vizuri mwanahakarakati wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika, Shujaa Nelson Mandela. Daima katika harakati zake chini ya kofia ya chama chao cha wa Chama cha African National Congress (ANC), alikuwa na pacha wake kiharakati, Mzee Walter Sisulu.

Hata alipokuja nchini mara kadhaa, ikiwamo safari ya mwisho walipotaka kustaafu siasa, mwanzoni mwa miaka ya 1990 kukutana na umati katika Uwanja wa Mnazi Mmoja Dar es Salaam, alikuwa mmoja wa vivutio vikubwa

Marehemu Mzee Walter Sisulu, mpole kimaumbile, ila matendo yake kisiasa yamezaa mengi kwa wananchi Afrika Kusini, dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi, akiwa sehemu ya kila matendo ya Mandela.

Walter Max Ulyate Sisulu, ni mwanaharakati aliyepinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Mwanachama wa Chama cha African National Congress (ANC), alizaliwa Mei 18, mwaka 1912.

Miongoni mwa nyadhifa zake kichama ni Katibu Mkuu wa ANC kuanzia mwaka 1949 hadi 1954 na pia Makamu wa Rais wa ANC tangu 1991 hadi 1994.

Misimamo yake na harakati zake, zilimsababiahia kuingia kifungoni.

Sisulu, alikuwa mshtakiwa Na. 2 katika Kesi ya Rivonia na alifungwa kwenye Kisiwa cha Robben, akitumikia kifungo cha zaidi ya miaka 25, kwa sababu ya kupinga ubaguzi wa rangi. 

Ni mashirika wa karibu na muungaji mkono wa falsafa za wenye taswira kama yake kifikra, alikuwa na ushirikiano na Oliver Tambo na Nelson Mandela.

Hao wote kw pamoja walihusika kwa kiasi kikubwa katika kuandaa Kampeni ya Uasi wa 1952 na kuanzisha Ligi ya Vijana ya ANC pamoja na ‘Umkhonto we Sizwe’. 

Pia alikuwa Sisulu,  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini.

FAMILIA YAKE

Sisulu alizaliwa katika mji wa Ngcobo, ndani ya Muungano wa Afrika Kusini, sehemu ambayo sasa ni Jimbo la Eastern Cape (wakati huo ilikuwa Transkei). 

Kama ilivyokuwa kawaida kwa kizazi chake, hakuwa na uhakika wa tarehe ya kuzaliwa, lakini alikuwa akiadhimisha siku hiyo tarehe 18 Mei.

Mama yake, Alice Mase Sisulu, alikuwa mfanyakazi wa ndani wa kabila la Xhosa na baba yake, Albert Victor Dickinson, alikuwa mtumishi wa serikali ya mzungu na hakimu. 

Dickinson, hakuhusika katika malezi yake kabisa ya mwanawe, inasemekana Sisulu alikutana naye mara moja tu, miaka ya 1940, kabla hajafariki miaka ya 1970.

Sisulu na dada yake, Rosabella, walilelewa na familia ya mama yao, ‘ujombani’, ukoo wa Thembu. 

Alikuwa na uhusiano wa karibu na mjomba wake, Dyantyi Hlakula, ambaye alipenda sana utamaduni wa Xhosa na ndiye aliyesimamia sherehe za kumwingiza utu uzima. 

Ingawa kitaalamu alikuwa wa mchanganyiko wa damu, Sisulu alijitambulisha kama Mwafrika mweusi na Mxhosa.

Katika ujana wake, aliacha shule, ilikuwa shule ya misheni ya Anglikana na kuamua kutafuta kazi. 

Alifanya kazi mbalimbali mjini Johannesburg, zikiwamo za kuwa mtunza fedha benki, mfanyakazi wa migodi ya dhahabu, mfanyakazi wa ndani, na mpishi wa mikate. 

Harakati zake damuni hazikujificha, huko nako alifukuzwa kazi kwa kujaribu kuwaunganisha wafanyakazi wenzake.

Mwaka 1939, alianzisha kampuni ya Sitha Investments, iliyokuwa katika jengo la Barclay Arcade, kati ya Barabara ya West na Commissioner katika kitovu cha biashara cha Johannesburg. 

Lengo lake, lilikuwa kusaidia Waafrika na Wahindi kununua nyumba. Wakati huo, Sitha ilikuwa kampuni pekee ya biashara ya mali isiyohamishika inayomilikiwa na Mwafrika.

MAISHA YA KISIASA

Harusi ya Sisulu na Albertina, ilifanyika mwaka 1944. Evelyn Mase alikuwa kushoto kwa bwana harusi na Nelson Mandela alikuwa mbali kushoto. 

Anton Lembede, alikuwa kulia kwa bibi harusi. Dada wa Walter, Rosabella, alikuwa akiwatazama wanandoa hao.

Sisulu, alikuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa ANC waliopigania ushirikiano usio na ubaguzi wa rangi, hatua iliyopelekea ushirikiano na wanaharakati Weupe na Wahindi kama Joe Slovo na Ahmed Kathrada. 

Kazi yake iliweka msingi wa wazo la "Rainbow Nation." Alijiunga na ANC mwaka 1940. Mwaka mmoja baadaye, Mandela alihamia Johannesburg na kutambulishwa kwa Sisulu. 

Sisulu alisema, "Sikusita hata kidogo, nilipokutana naye nilijua kuwa huyu ndiye mtu ninayemhitaji" mtu wa kuwaongoza Waafrika.

Alimshauri Mandela kujiunga na ANC, alimsaidia kidogo ada ya shule ya sheria na alimtambulisha kwa mke wake wa kwanza, Evelyn Mase, ambaye alikuwa ndugu wa mama yake Sisulu.

SISULU, MANDELA MICHEZONI

Mwaka 1943, Sisulu akiwa na Mandela na Tambo, walijiunga na Ligi ya Vijana ya ANC, iliyoanzishwa na Anton Lembede.

Sisulu alikuwa Mweka Hazina wa kwanza. Alijitenga na Lembede, baada ya Lembede kumkejeli kuhusu ukoo wake.

Ushindi wa Chama cha National Party (NP) mwaka 1948, kilichokuza sera za ubaguzi, uliongeza hamasa ya harakati za kisiasa.

Desemba 1949, katika Mkutano wa 38 wa Kitaifa wa ANC, Ligi ya Vijana ilifanya "mapinduzi ya kushangaza", na kuwafanya vijana wakakamavu kuchukua nafasi ndani ya Kamati Kuu ya Chama, akiwamo Sisulu aliyechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa ANC.

Ligi pia ilileta Mpango wa Harakati uliosisitiza utaifa wa Waafrika na mbinu za uhamasishaji wa umma. Kilele chake kilikuwa Kampeni ya Uasi ya 1952. 

Sisulu alikuwa katika kamati ya kupanga na alikamatwa kwa kushiriki. Alihukumiwa na wengine kwa "ukomunisti wa kisheria" lakini adhabu yao ilisitishwa kwa miaka miwili.

Hakuchoka, mwaka 1953, Sisulu aliongoza ujumbe wa ANC katika mkutano wa Vijana wa Kidemokrasia duniani huko Romania. 

Pia walitembelea Poland, London, Israeli na China. Mwaka 1955, Sisulu, Mandela na Kathrada walitazama Mkutano wa Watu, ulioidhinisha Katiba ya Uhuru kutoka juu ya paa kwa kuwa walikuwa wamepigwa marufuku kuhudhuria.

UMKHONTO WE SIZWE

Mwanahistoria Paul Landau, alisema kuwa Sisulu na Mandela walikuwa nguvu kuu nyuma ya mabadiliko ya ANC ya kuingia katika mapambano ya silaha. Sisulu alikuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Umkhonto we Sizwe ulioanzishwa 1961.

Alihukumiwa mara saba kati ya 1952 na 1962, akazuiliwa nyumbani mwaka 1962. Katika Kesi ya Uasi (1956–1961) alihukumiwa miaka sita lakini aliachiwa kwa dhamana akisubiri rufaa.

KESI YA RIVONIA

Alijificha mwaka 1963, na mkewe Albertina kuwa mwanamke wa kwanza kutiwa mbaroni kwa Sheria ya Siku 90. Alikamatwa Rivonia tarehe 11 Julai. Alifungwa kifungo cha maisha tarehe 12 Juni 1964. 

“Ninaapa kwa dhati nikitambua matokeo ya kiapo hili. Mradi bado ninaaminiwa na watu wangu, na kadri bado nina uhai, nitapigania kwa ujasiri na msimamo kufutwa kwa sheria za kibaguzi na uhuru wa Waafrika Kusini wote, bila kujali rangi wala imani.”

GEREZANI

Alihudumu sehemu kubwa ya kifungo chake kwenye Kisiwa cha Robben, baadaye akahamishiwa Gereza la Pollsmoor. Mkewe aliwekewa marufuku ya kusafiri mara kadhaa.

Aliachiliwa huru tarehe 15 Oktoba 1989 akiwa na miaka 77. Aliungana na Mandela katika mazungumzo yaliyopelekea Minute ya Groote Schuur. Mwaka 1991 alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa ANC, kwa lengo la kuepusha migogoro kati ya viongozi vijana.

Baada ya 1994, Sisulu alichagua kutohudumu serikalini. Alibaki kuwa mshauri na msaidizi.

KUSTAAFU NA KIFO

Mwaka 1994, ANC ilishinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia, lakini Sisulu alikataa kushiriki serikali kutokana na afya yake. Alifariki tarehe 5 Mei 2003, karibu na siku yake ya kuzaliwa. Alizikwa rasmi kwa heshima kubwa tarehe 17 Mei 2003. 

Mandela alisema: “Tangu tulipokutana 1941, maisha yetu yamefungamana. Tuliishi pamoja, tuliteseka pamoja. Alikuwa rafiki yangu, kaka yangu, mlinzi wangu, na mzalendo mwenzangu.”

Baada ya kifo cha Mandela 2013, Mac Maharaj alifichua kuwa Sisulu na Mandela waliandikiana nekrolijia kabla ya 2003.

HAIBA, TASWIRA YA UMMA

Sisulu alisifiwa kwa unyenyekevu wake. Waliokuwa naye gerezani walimpongeza kwa utulivu na uvumilivu wake. Mandela alisema, “Mara nyingi alikuwa kimya wakati wengine walikuwa wakipiga kelele.” Kathrada alisema:

“Huwezi kumzungumzia Mandela bila kumtaja Sisulu. Walikamilishana... Mandela aliheshimiwa sana, lakini Sisulu alipendwa zaidi. Tofauti ya baba na kiongozi – hiyo ndiyo tofauti yao.”