“TUMEFANYA yote kwa sababu tumeenzi na kulinda Muungano wetu. Wengine walijaribu hawakuweza. Sisi tumeulinda kwa miaka 61. Kama ni kuporomoka au kufaidika ni wote. Watanzania tuendelee kuenzi na kuulinda, ndio msingi wa amani, umoja, maendeleo na mustakabali wa taifa letu."
Ni moja ya kauli za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan, anazotoa katika mikutano ya kampeni visiwani Zanzibar, akiwa kwenye viwanja vya nyumbani alikozaliwa Makunduchi.
Akiendelea kujinadi kwa wananchi ili kumchagua Oktoba 29, 2025, anasisitiza dhamira ya chama chake na serikali kuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Anawahakikishia wananchi wa visiwani Unguja na Pemba kwamba amani, mshikamano na maendeleo vitabaki kuwa dira ya taifa.
Katika mikutano hiyo, Samia anatumia muda mwingi kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali ya awamu yake, akionesha kwamba, Muungano umekuwa chanzo kikuu cha amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.
Anasema kwa miongo sita sasa, Tanzania imeendelea kuishi kwa umoja kwa sababu ya kuenzi Muungano, jambo ambalo wengine walijaribu lakini walishindwa.
Katika mikutano yake, Samia anabainisha kuwa Muungano umekuwa na faida kubwa kwa wananchi wote wa pande mbili za Muungano. Amewataka wananchi wasidanganywe na hoja zinazopotosha zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani.
“CCM tunaamini Muungano umekuwa na manufaa makubwa.
Tunatofautiana na wenzetu wanaobeza na kupotosha umma kuhusu Muungano. Ukweli ni kwamba umetoa fursa ya maendeleo katika sekta nyingi,” anasisitiza kwenye moja mkutano unayofanyika wiki iliyopita visiwani humo.
Anatoa mfano sekta ya uchumi wa buluu, hususan uvuvi wa bahari kuu, usafirishaji kupitia Bahari ya Hindi na rasilimali za mafuta na gesi, akisema zimekuwa zikisimamiwa kwa pamoja na zikinufaisha Watanzania wote.
KUNYANYUA WANANCHI
Akieleza jitihada za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, Samia anautaja Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambavyo umesaidia familia nyingi kutoka katika umasikini wa kupindukia.
“Mradi wa TASAF umefanya vizuri. Wengi wamemaliza na sasa wanajitegemea, wengine wameingizwa na wanaendelea kuandaliwa awamu nyingine ili kunyanyua walio chini,” anaahidi Watanzania.
Anaweka wazi kuwa programu za mikopo isiyo na riba na urasimishaji wa biashara ndogo ni sehemu ya Muungano, na zitaendelea kufanikishwa kote nchini.
DIPLOMASIA KIMATAIFA
Rais Samia anasifu kuwa Tanzania imepata heshima kubwa kimataifa kutokana na mshikamano na umoja wa taifa, jambo lililoimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kukuza jina la nchi.
“Heshima tunayoipata duniani ni kwa sababu ya mshikamano wetu.Tumekuza uhusiano na kuimarisha jina la Tanzania kimataifa,” anasema.
AMANI UCHAGUZI
Katika mikutano yake, Rais Samia anasisitiza kuwa kudumisha amani, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ni jambo la lazima sana.
Anasema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha kila Mtanzania anapiga kura kwa utulivu.
“Hamjasikia pepepe ndani ya nchi. Mkisikia labda ni ajali au mtu mmoja amevunja amani, lakini hamjasikia vurugu. Hata waliovuka mipaka kutaka kuleta vurugu tumewashughulikia na hawajathubutu kurudi tena.
“Niwaombe sana ndugu zangu, kipindi hiki ni cha uchaguzi na wengine wanakitumia kuchokozana. Msichokozeke. Kuweni kama mimi, mama yenu, dada yenu, bibi yenu. Nachokozwa sana lakini sichokozeki. Tusivunje amani kwa sababu ya uchaguzi, maana akiumia mmoja ni familia nzima itahangaika,” anasema.
Mgombea urais wa CCMA anaguswa na mshikamano wa kijamii, akisisitiza kwamba haoni tofauti ya makabila au mikoa.
“Mimi nikiwa Makunduchi, nitasema ni Mmakunduchi. Nikiwa Kizimkazi, nitasema ni Mkizimkazi.
“Lakini hapa pia niwaambie mimi ni Mpemba pia. Sitafurahi kuona ndugu yangu wa Makunduchi au wa Pemba amepigwa au ameumizwa. Niwaombe sana tutunze amani na utulivu.”
Aidha, anawahimiza wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura, akibainisha kuwa hakuna vurugu zitakazotokea kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara.
“Tumejipanga vyema kulinda nchi hii. Hakutakuwa na ninyi wala nyinyinyi. Watu tokeni, amshakeni kapigeni kura. Msijemkawa wengi kwenye mikutano halafu kwenye boksi la kura mkawa wachache,” akahamaisha.
Rais Samia analitumia jukwaa hilo kumwaga sifa kwa mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwaeleza Wazanzibari kuwa ndiye mgombea sahihi atakayewavusha salama.
“ Kazi aliyoifanya katika miaka mitano iliyopita imethibitisha kuwa yeye ni kiongozi makini, mtulivu na mzalendo,” anasema.
Kwa ujumla mikutano ya kampeni aliyofanya Unguja na Pemba, amesisitiza misingi mitatu ambayo chama chake na serikali wanayoingoza wanataka iendelee kusimama kama nguzo ya taifa: kuenzi Muungano, kudumisha amani na mshikamano, na kuhakikisha maendeleo kwa kila Mtanzania.
Kwa kauli zake zenye msisitizo, anahamasisha siyo tu wafuasi wa CCM, bali Watanzania kwa ujumla kudumisha umoja na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao.
Msisitizo wake ni kuwa Muungano ndiyo msingi wa nguvu ya taifa, na kwamba bila amani na mshikamano hakuna maendeleo yatakayoweza kufanikishwa.
Kwa upande wa mgombea urais Zanzibar, Dk. Mwinyi anahimiza amani, umoja, mshikamano na maridhiano, akiweka bayana kwamba, ndizo sera za CCM, kufanyika kinyume chake ni kutoitakia mema nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED