SWALI la kila mwaka ni hili - kuna timu yoyote inayoweza kuizuia Manchester City kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England, EPL?
Kwa msimu wa tisa mfululizo kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola kinapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la Ligi Kuu England.
Wameshinda mataji sita kati ya saba yaliyopita, yakiwamo manne mfululizo.
BBC Sport inazitazama timu saba, wapinzani wa Man City wenye uwezo pia wa kutwaa taji. Timu zimepangwa kulingana na nafasi zao za kumaliza msimu uliopita, twende sasa...
Arsenal
Mwisho wa msimu uliopita, walikuwa nafasi ya pili, pointi mbili nyuma ya City. Wamemaliza washindi wa pili chini ya Man City katika misimu miwili iliyopita.
'Washikabunduki' wa London hao wamefanya mabadiliko makubwa, wamemleta mlinzi wa Italia, Riccardo Calafiori kutoka Bologna kwa ada ya pauni milioni 42. Anaweza kucheza beki wa kushoto au wa kati.
Pia wamegeuza mkataba wa mkopo kuwa wa kudumu kwa kipa wa Hispania, David Raya, ambaye alimpiku Aaron Ramsdale na kuwa namba moja msimu uliopita.
Winga Bukayo Saka ndiye mfungaji wao bora katika misimu miwili iliyopita. Na wanahusishwa kutaka kumnunua mshambuliaji wa Napoli, Victor Osimhen.
"Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard, alisema mwishoni mwa msimu uliopita kwamba, wameibadilisha klabu na anaamini Arsenal watashindania taji kwa muda mrefu," anasema Mwandishi wa Michezo wa BBC, Alex Howell.
Liverpool
Mwisho wa msimu walikuwa nafasi ya tatu, pointi tisa nyuma ya Man City. Liverpool wanaanza msimu bila ya Kocha Jurgen Klopp kwa mara ya kwanza tangu 2015-16.
Klopp alitangaza ataondoka mwishoni mwa msimu, lakini tangazo lake lilikuja katikati ya msimu uliopita - na nafasi yake imechukuliwa na Arne Slot, Mei mwaka huu.
Mholanzi huyo anaonekana kubadilisha mtindo wa uchezaji wa Liverpool kutoka mchezo wa nguvu na haraka hadi ule wa kumiliki mpira.
Liverpool ndio timu pekee mbali na Man City kushinda taji la Ligi Kuu katika kipindi cha miaka saba iliyopita, bado hawajasajili mtu yeyote msimu huu - lakini Slot anatumaini watasajili.
Mwandishi mwandamizi wa soka wa BBC Sport, Nizaar Kinsella, anasema: "Liverpool wanatarajia kuleta ushindani katika msimu wa kwanza wa Slot baada ya enzi nzuri chini ya Jurgen Klopp na kuiacha klabu katika nafasi nzuri.”
Aston Villa
Mwisho wa msimu uliopita walikuwa nafasi ya nne na pointi 23 nyuma ya Man City. Ilifuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita.
Unai Emery ameigeuza klabu hiyo kutoka kugombea kutoteremka daraja hadi timu ambayo inazungumzwa kama mshindania taji msimu uliopita - na hata hajaiongoza kwa miaka miwili bado.
Klabu hiyo inalazimika kuuza wachezaji msimu huu wa majira ya joto ili kutimiza kanuni za faida na kifedha za Ligi Kuu England.
Lakini wameleta sura nyingi mpya - ikiwa ni pamoja na kiungo wa Everton. Amadou Onana, beki wa kushoto wa Chelsea, Ian Maatsen, kiungo wa kati wa Luton, Ross Barkley - na vijana wa akademi Jaden Philogene na Cameron Archer.
Tottenham Hotspur
Mwisho wa msimu uliopita walikuwa watano, wakiwa nyuma ya Man City kwa alama 25. Walianza vema msimu uliopita chini ya Ange Postecoglou na walikuwa nyuma kwa pointi tano kileleni baada ya mechi 10.
Archie Gray, pauni milioni 30 kutoka Leeds, Lucas Bergvall pauni milioni 8.5 kutoka Djurgarden na George Feeney kutoka Glentoran - aliyesajiliwa kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18, ndio pekee waliosajiliwa majira ya haya ya joto hadi sasa.
Winga chipukizi wa Korea Kusini, Yang Min-hyuk, atajiunga na kikosi hicho Januari.
Mikey Moore, mshambuliaji wa akademi mwenye umri wa miaka 16, amevutia katika mechi za kirafiki za kabla ya msimu mpya.
Mwandishi wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: "Kocha Postecoglou ndiye atakayeisukuma Tottenham kushinda taji kwa mara ya kwanza tangu 2008. Hatataka kuweka kikomo katika malengo ya Spurs, lakini kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya litakuwa lengo lao kubwa zaidi."
Chelsea
Mwishoni mwa msimu uliopita ilishika nafasi ya sita na alama 28 nyuma ya Man City. Kocha Enzo Maresca, baada ya kuifundisha Leicester na kupanda daraja, alichukua nafasi ya Mauricio Pochettino katika kiti moto cha 'The Blues'.
Wamesajili wachezaji wengi majira ya kiangazi - Kiernan Dewsbury-Hall, Tosin Adarabioyo na Omari Kellyman wote wana uzoefu wa Ligi Kuu England.
Beki mkongwe wa kati Thiago Silva, pamoja na Hakim Ziyech, Ian Maatsen, Lewis Hall na Omari Hutchinson - wote walikuwa nje kwa mkopo msimu uliopita – wameondoka moja kwa moja. Na Conor Gallagher anatarajiwa kuhamia Atletico Madrid.
Mwandishi wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: "Kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanikiwa kupata mataji mengine yatakuwa ndio matarajio yao, lakini kuna matumaini kwamba kikosi hiki cha vijana kinaweza kukua na kuleta ushindani katika misimu ijayo."
Newcastle United
Mwisho wa msimu uliopita ilishika nafasi ya saba na pointi 31 nyuma ya Man City. Newcastle walifanya vema msimu wa 2022-23 kwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini kumaliza katika nafasi ya saba msimu uliopita kulionekana kama kushuka chini.
Sasa Newcastle wanatumaini watambakiza Kocha Eddie Howe, ambaye anapendekezwa kuwa Kocha wa England.
Mwandishi wa Soka wa BBC Sport, Simon Stone anasema: "Nilifadhaika kuhusu Newcastle kwamba wanaelemewa na sheria za kifedha, ikimaanisha kuwa wanalazimika kuuza wachezaji wakati wanataka kununua.
"Habari njema ni Alexander Isak, Bruno Guimaraes na Anthony Gordon wote bado wako kwenye klabu hiyo."
Manchester United
Mwisho wa msimu walikuwa nafasi ya nane na pointi 31 nyuma ya Man City. Walimaliza vibaya zaidi tangu ligi ya msimu wa 1989-90, walipomaliza katika nafasi ya nane – ingawa msimu huu wameshinda Kombe la FA.
Kocha Erik ten Hag alitarajiwa kupoteza kibarua chake, lakini United waliamua kubaki na Mholanzi huyo baada ya kukaa kwa kipindi cha miaka miwili klabuni hapo.
Man United wametumia fedha kununu vijana wawili msimu huu - mshambuliaji wa Bologna, Joshua Zirkzee kwa pauni milioni 36.5 na mlinzi wa kati wa Lille, Leny Yoro kwa pauni 52.
Hata hivyo, tayari Yoro amejeruhiwa na huenda akakaa nje ya uwanja kwa miezi mingi. Vilevile, wachezaji kadhaa wameondoka kwa uhamisho wa bure akiwamo mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Ufaransa, Raphael Varane na Anthony Martial.
Mwandishi wa BBC Sport, Simon Stone, anasema: "Erik ten Hag lazima aepuke kufanya vibaya msimu huu kwa sababu hawezi kumudu kumaliza nafasi ya nane tena.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED