JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu, tuliangalia namna wanawake wanaopenya na kufanikiwa kushika nafasi za uongozi, wanavyoonesha uwezo mkubwa katika usuluhishi wa migogoro ya kifamilia au ya kijamii kwa njia ya amani na maelewano.
Tuliona pia uelewa wao wa changamoto zinazoendelea katika jamii, unavyowasaidia kupendekeza njia endelevu za kutatua changamoto kila zinazopojitokeza. Katika safu yetu leo, tutaangalia kwa nini viongozi wanawake wana nafasi kubwa ya kufanya ushawishi wa mabadiliko yenye tija. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira.
Viongozi wanawake wana nafasi kubwa ya kufanya ushawishi wa mabadiliko yenye tija, dunia inashuhudia mabadiliko makubwa kwenye siasa, nafasi ya mwanamke katika uongozi imeendelea kupata msukumo mkubwa.
Ingawa kwa muda mrefu wanawake wamekabiliwa na changamoto nyingi katika kupata nafasi za uongozi na ushawishi, leo hii wanawake wengi wameonesha uwezo mkubwa wa kuongoza, kushawishi, na kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.
Ukifuatilia kwa makini, utabaini kuwa wanawake wanapopewa uongozi, kwa kutumia nafasi zao katika vyombo vya maamuzi iwe ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa, taifa na hata kwenye taasisi ziwe za umma, binafsi ama vikundi vya kijamii, hutumia uzoefu wao na uelewa mkubwa walionao katika changamoto zilizoko katika jamii zao, kufanya ushawishi unaolenga katika kuleta mabadiliko yenye tija kwa jamii nzima.
Ingawa wengine wanaingia kwenye nafasi za maamuzi kuwakilisha makundi fulani, kiuhalisia wamekuwa wakibeba sauti za jamii nzima. Kwa kuangalia mifano ya baadhi ya wanawake waliofanikiwa kufanya ushawishi ulioleta mabadiliko makubwa katika jamii na taifa, ni wazi kuwa jamii inaweza kuwa na mabadiko makubwa iwapo wanawake wengi zaidi watapata nafasi za kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali.
Miongoni mwa masuala ambayo wanawake viongozi wana uwezo mkubwa wa kuyashikia bango na kushawishi mabadiliko ni pamoja na kupinga mila na desturi kandamizi dhidi ya wanawake na wasichana. Kwa kutumia nafasi zao, wanaweza kujenga uelewa kwa jamii kuhusu usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na madhara ya mila kandamizi.
Eneo kubwa ambalo wanawake wamefanikiwa kufanya mabadiliko ya fikra ni eneo la uchumi ambapo hivi sasa kila mahali wameamka, wameanzisha vikundi, wanafanya biashara na kutunza fedha zao kuendeleza familia zao. Hii imewawezesha kujitegemea kiuchumi na kupunguza utegemezi wa kifedha ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa unachochea ukatili wa majumbani.
Ili kuleta kushawishi mkubwa katika nyanja ya uchumi, tumeshuhudia wengi wameanzisha miradi ya kiuchumi inayolenga wanawake na vijana kama vile vikundi vya ujasiriamali, kilimo cha kisasa, au elimu ya stadi za maisha. Wengine wametoa ajira kwa wanawake wengine, hivyo kuimarisha hali ya maisha na kuongeza ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Wapo wanaoongoza vikundi hivyo kwa mafanikio makubwa, iwapo wakipata nafasi ya uongozi wa kisiasa, ni wazi watafanya ushawishi mkubwa kwenye jamii.
Njia nyingine ambayo wanaitumia kuleta ushawishi wa mabadiliko yenye tija ni kwa kushiriki kwenye mijadala mbalimbali na kupaza sauti juu dhidi ya masuala kama ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, mimba za mapema, ukosefu wa huduma za afya. Kupitia ushiriki wao, pia wanawake kushinikiza serikali na taasisi kuchukua hatua madhubuti kwa kupitia kampeni na harakati za kijamii.
Kushiriki katika mijadala ya kijamii ni moja ya njia zenye nguvu kubwa sana ya kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii. Kwa wanawake, kushiriki kwenye mijadala hii na kutumia sauti zao kwa ujasiri ni hatua muhimu ya kuondoa ukimya uliodumu kwa karne nyingi kutokana na mfumo dume, mila kandamizi, na ubaguzi wa kijinsia.
Majukwaa haya yanaweza kuwa kupitia mikutano ya kijiji, semina, makongamano, midahalo ya vyombo vya habari, mijadala ya mitandaoni, au hata majadiliano katika vikundi vya kijamii kama makanisa, misikiti, vikundi vya kina mama.
Kushiriki katika mijadala ya kijamii na kupaza sauti siyo tu haki ya wanawake bali ni wajibu muhimu wa kijamii. Wanawake wanapojitokeza na kuzungumza, wanaleta mtazamo mpya, wa kweli na wa kuleta matumaini. Sauti zao huchochea mabadiliko, hutoa mwanga kwa wanaonyimwa haki, na kuibua majadiliano ya kuleta jamii yenye usawa, haki, na maendeleo. Ni muhimu kuendelea kuwahamasisha, kuwawezesha, na kuwalinda wanawake wanaotumia sauti zao kwa ajili ya manufaa ya jamii nzima.
Matumizi sahihi na yenye tija ya mitandao ya kijamii ni njia nyingine ambayo inaweza kutumiwa na wanawake viongozi kufanya ushawishi. Hivi sasa wanawake wengi wamejiunga na vikundi vya kuinuana, kusaidiana na kufanya biashara pamoja. Ili kurahisisha mawasiliano, wanatumia mitandao ya kijamii na njia hii imewasaidia sana kuwafikia kwa haraka hata wale wanaoishi pembezoni.
Licha ya vikundi hivyo kuwa na malengo mengine lakini uzoefu umeonesha kuwa vikundi hivyo ni fursa nzuri kwa wanawake kuelimishana na kupashana taarifa kuhusu masuala mengine muhimu yanayoendelea katika maeneo yao. Mfano mzuri ni wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024, ambapo wanawake walitumia vikundi vyao vya kuinuana kuhamasishana na kupashana taarifa juu ya uchaguzi.
Uzoefu huo unaonesha kwamba wanawake wana nafasi kubwa ya kufanya ushawishi kutumia mitandao waliyonayo, kwa sababu njia hiyo tayari imeonyesha mafanikio makubwa.
Kwa ujumla, wanawake viongozi wanaweza kuwa mawakala wa mabadiliko katika jamii kwa kutumia nafasi zao kushawishi sera, kuelimisha jamii, kuanzisha miradi ya maendeleo, na kuvunja mila na mitazamo potofu. Hata hivyo, ili haya yote yafanikiwe, ni muhimu pia kwa jamii kuwapa wanawake nafasi, usaidizi na mazingira wezeshi ya kuendeleza jitihada zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED