WAKATI kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea Rais mstaafu, Jakaya Kikwete anatabiri kuwa bunge linaloundwa badaye mwezi huu litakuwa na wabunge wanaotoka CCM.
Tena, akiamini kwamba hilo litatimia kwa nchi nzima, si Chalinze peke yake na halitatofautiana na bunge lililomaliza muda wake Julai mwaka huu.
Kiongozi huyo anatoa kauli hiyo Jumapili iliyopita katika mwendelezo wa kampeni za mgombea urais kupitia CCM Samia Suluhu Hassan, kwenye viwanja vya Sabasaba Kibaha mkoani Pwani.
Anakazia kuwa hawapo tayari kuchanganya pumba na mchele, kwa maelezo kwamba wanayajua madhara yake na hawatathubutu kufanya hivyo katika uchaguzi huo.
Baadhi ya wachambuzi na wadau wa siasa wanajadili kauli hiyo wakiiambia Nipashe kuwa maoni hayo yanawakatisha tamaa.
Mwanzilishi wa Chama Cha Kijamii, Constantine Akitanda, anadai kauli hizo zinasikitisa na kukatisha tama kuwa kumbe bado demokrasia ya vyama vingi, haina nafasi.
Anapendekeza kuwa njia ya kumaliza kauli zenye utata kama za mstaafu JK ni kuwapo katiba mpya.
"Ninaamini mwenendo wa uchaguzi huu, umetupatia funzo kubwa kama nchi, bila shaka suala la katiba mpya na hasa inayotokana na maoni ya wananchi ndio uwe mwelekeo wetu," anasema Akitanda.
Anaeleza kuwa amemsikiliza rais mstaafu kwenye mkutano wa hadhara Kibaha mkoani Pwani, na kufafanua kuwa ni wazi CCM inatamani kushinda kwa kishindo kikubwa, lakini akaikumbusha kuwa upinzani upo kikatiba na si pumba au chuya.
"Ila kwa mazingira haya na bila kuzunguka sana, Tanzania inahitaji katiba mpya, ambayo Jaji Warioba na tume yake walituonesha njia ya kupita. Kinyume na hapo, vyama mbadala vitasubiri sana na mwishoni nchi inaweza kuingia kwenye shida kubwa za kisiasa," anasema.
"Msisitizo wangu ni kwamba, CCM, isipuuze maoni au mawazo ya wananchi, kwani Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa 'chama kinachopuuza maoni ya wananchi, kinaweza kulia vibaya na asipatikane wa kukipangusa machozi," anasema.
ATULIE NYUMBANI
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, anasema ni vyema mstaafu akapumzika na kumwachia Rais Samia aendelee kufanya kazi badala ya kumwingilia.
Anasema Kikwete alimaliza zamu yake tangu mwaka 2015, na kwamba anachokifanya ni sawa na kumharibia kiongozi aliyepo madarakani, kwa kauli zenye utata zinazoirudisha nchi kwenye enzi ya chama kimoja.
"Rais Samia alikuja na R4 falsafa ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga upya Taifa (Rebuilding). Hivyo, nitoe wito akumbuke kauli mbiu hiyo na kuifanyia kazi kikamilifu,” anasema
Anakumbusha kuwa Rais Samia, anatangaza falsafa hiyo na kuitisha mkutano na viongozi vyama vya upinzani kwa lengo la kuunganisha Watanzania bila kujali vyama vyao, lakini leo anakuja mtu kumwaribia.
Anasema njia ya nzuri ya kumfanya mstaafu aendelee kuheshimiwa na Watanzania ni kukaa nyumbani na kuacha kujihusisha na siasa, kwa maelezo kwamba anataka kupotosha.
"Hadi sasa ni zaidi ya miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, sasa inakuwaje yeye aseme Watanzania wasichanganye pumba na mchele? Anataka kuwaaminisha kuwa vyama vya upinzani havina lolote katika nchi hii? Anahoji.
Magdalena anasema vyama vya upinzani havikujileta vyenyewe bali vipo kisheria, na kwamba vinapaswa kuheshimiwa na sio kuitwa majina ya aina hiyo kana kwamba havina mchango kwa maendeleo ya nchi.
"CCM inayopigiwa debe haina tena uwezo wa kuongoza nchi, hivyo ikae pembeni na kupisha wengine waweze kuongoza, sio kudanganya wananchi kuwa upinzani ni pumba," anasema.
Mwanasiasa huyo anasema Tanzania bila kuongozwa na CCM inawezekana, huku akiwataka Watanzania waachane na propaganda zinazotolewa na makada wa CCM zinazolenga kudhoofisha upinzani.
HAJASEMA VIBAYA
Mwanasiasa mwingine, Thomas Ngawaiya, anasema kauli hiyo ni ya kawaida katika majukwaa ya siasa na kwamba kila muwamba ngoma huvutia kwake. na kwamba hajakosea kusema hivyo.
"Ingekuwa ni ajabu kama angesema kuwa anatamani mkoa wagombea wote wa ubunge mkoani Pwani wawe wa vyama vya upinzani wakati yeye mwanachama wa CCM," anasema Ngawaiya.
Ngawaiya anasema kilichofanywa na kiongozi huyo mstaafu ni kutimiza wajibu wake wa kukipigia debe chama chake ili ikiwezekana, wagombea wote wa chama hicho washinde katika uchaguzi mkuu.
"Kwanza neno pumba katika siasa ni la kawaida tu la kuvutia mashabiki wa chama na wala lisichukuliwe kama tu, kwani siasa ndivyo ilivyo, tunapigana vijembe kisha baada ya siasa tunakaa pamoja," anasema.
Anafafanua kuwa jambo la msingi katika kauli hiyo ni kutaka wananchi wawe makini na wagombea wote ili kuchagua wale ambao wanafaa, kwa maelezo, na kwamba pumba anaweza kuwa mgombea kutoka CCM au upinzani na kuongeza wapigakura ndio wanaotakiwa kuwa makini.
Ngawaiya anasema sio rahisi kuua upinzani, lakini suala la kila chama kuvutia upande wake ni la muhimu, kwa kuwa haiwezekani akasimama jukwaani na kupigia debe chama ambacho si chake.
"Tanzania ni nchi ya vyama vingi, lakini kila chama kinatakiwa kujipambania chenyewe kwa wananchi kama ambavyo Kikwete anaipigania CCM kwenye majukwaa wakati wa kampeni," anasema.
Anaongeza kuwa safari hii hakuna siasa za mikikimikiki ambazo zinasababisha watu kuonesha mahaba na itikadi za vyama, na kufafanua kuwa hiyo ni ishara kwamba uchaguzi mkuu utafanyika bila kuwa na ushindani mkali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED