Wahudumu 60 wa Afya Ngazi ya Jamii (WAJA) wamepatiwa mafunzo maalum ya namna ya kuelimisha jamii kuhusu saratani ya matiti na mlango wa kizazi, pamoja na kuhamasisha umuhimu wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi (HPV).
Akizindua mafunzo hayo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk.Jesca Lebba, amesema mradi huo unalenga kupambana na saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti. alibainisha kuwa, kwa kiwango cha dunia, saratani hizo mbili ndizo zinazoongoza kwa kusababisha vifo vitokanavyo na saratani kwa wanawake, ikiwemo Tanzania.
Ametoa wito kwa jamii kuzingatia chanjo inayotolewa mara moja kwa wasichana wa umri wa miaka tisa na husaidia kuwalinda dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Amesema serikali na wadau mbalimbali wanaendesha kampeni za uchunguzi wa awali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, hatua inayosaidia kubaini saratani mapema na kuchukua hatua stahiki kabla haijawa mbaya zaidi.
Akizungumzia mshikamano wa wadau, anasema kuwa Aga Khan Foundation wanashirikiana na watoa huduma wa serikali pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika kutoa elimu kwa wananchi, ili wanawake na wasichana waweze kufika kwenye vituo vya kutolea huduma na kupata huduma hizo muhimu.
"Changamoto kubwa katika Kanda ya Ziwa ni kuenea kwa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti ambazo pia zinaongoza duniani kote kwa kuathiri wanawake, takwimu kutoka hospitali zinazohusika na tiba ya saratani, kama Ocean Road na nyinginezo, zinaonyesha kuwa hali bado ni ya kutia wasiwasi na kwamba saratani hizi ndizo zinazoongoza kwa vifo vya akinamama."anaeleza.
Amesema Mkoa wa Mwanza bado unakabiliwa na changamoto ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi. Hivyo, alihimiza jamii kuwekeza zaidi kwenye afya kinga, badala ya kusubiri madhara yatokee, Pia wanahimiza akinamama kufanyiwa uchunguzi wa awali kwenye vituo vya afya ili kubaini saratani mapema kwa sabanu inatibika ikigunduliwa mapema.
Naye Meneja wa Mradi wa EA-Cwcp kutoka Aga Khan Foundation , Rester Boniface, amesema mradi huo wa miaka minne (2025–2029) unatekelezwa nchini Tanzania na Kenya, ambapo kwa Tanzania utahusisha mikoa sita Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam, pamoja na Zanzibar.
Amesema mradi huo unalenga kuwafikia wananchi zaidi ya milioni tatu kwa elimu ya afya, kuwachanja wasichana zaidi ya milioni moja dhidi ya virusi vya HPV, na kuwafanyia uchunguzi akinamama zaidi ya laki nne pia wahudumu wa afya 400 watajengewa uwezo ili wawe mabalozi wa kueneza elimu katika kaya na vijiji vyao.
“Tunataka jamii ielewe kuwa saratani inatibika endapo itagundulika mapema. Ndiyo maana tunaanza na mafunzo haya, ili WAJA wawe mabalozi wa elimu, watoe hamasa kwa akinamama kufanya uchunguzi na kuwashawishi wazazi kuruhusu watoto wao wa kike wa miaka tisa wachanjwe chanjo ya HPV,” anasema.
Kwa sasa mafunzo hayo yameanza katika mkoa wa Mwanza, yakihusisha halmashauri za Misungwi, Sengerema na Kwimba, maeneo ambayo kiwango cha chanjo ya HPV bado hakijafikia malengo ya kitaifa.
Amesema malengo ya mradi ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu saratani ya wanawake,kuboresha miundombinu katika baadhi ya hospitali zinazotoa huduma za saratani, kuwajengea uwezo watoa huduma wa afya, ikiwemo WAJA pamoja na kuufanya tafiti mbalimbali kuhusu saratani.
" Mradi unatekelezwa na mtandao wa maendeleo wa Aga Khan( AKDN ) kupitia taasisi zake ambazo ni Aga Khan hospital,Aga Khan foundation,Chuo kikuu cha Aga Khan Kwa kushirikiana na wizara ya afya na Tamisemi ,ukifadhiliwa na shirika la maendeleo la Ufaransa ( AFD) , Gates Foundation na Aga Khan foundation" anaeleza.
Amesema pia watashirikiana na viongozi wa dini, ili kuhakikisha jamii inaondokana mitazamo potofu inayohusisha saratani na ushirikina au laana.
Kalugulu Bundala ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mhudumu wa afya ngazi ya jamii, alisema mafunzo hayo yata msaidia kupeleka ujumbe sahihi kwa jamii yake ambayo mara nyingi huamini saratani ni laana au kurogwa.
"Nitakuwa balozi wa elimu na kuwahamasisha watu kufanya uchunguzi mapema.”
Rebeca Nyamsingi aliongeza kuwa ataitumia elimu hiyo kuvunja dhana potofu kwa sababu jamii hudhani saratani ni ugonjwa wa kishirikina, lakini watawaelimisha kuwa ni ugonjwa kama mengine na unatibika iwapo utagunduliwa mapema.
Matina Igembesabo aliahidi kushirikiana na jamii yake kwa karibu na kupita kaya kwa kaya kutoa elimu hiyo ,imani potofu bado zipo, lakini tutaendelea kuelimisha watu wakapate uchunguzi na matibabu kwa wakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED