MAZOEZI ya kijeshi ya majini yanayoandaliwa kwa pamoja kati ya India na Tanzania, yameanza katika Bahari ya Hindi na kuonyesha jinsi sayansi na teknolojia inavyokuwa kwa kasi na kurahisisha kazi ya ulinzi, usalama na maendeleo ya uchumi wa bluu.
Katika mazoezi hayo ya siku sita yanayofahamika kama Africa-India Key Maritime Exercise (AIKEYME) mataifa mengine 11 ya Afrika yanahusika.
Mataifa haya ni pamoja na Afrika Kusini, Djibouti, Shelisheli, Mauritius, Comoro, Msumbiji, Kenya na Madagascar, ni kwa mujibu wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda.
Ujio wa meli hiyo unakamilisha maandalizi ya zoezi la kijeshi Kamandi ya Jeshi la Wanamaji na Jeshi la Wanamaji la India.
Mazoezi hayo ambayo yanafanyika nchini katika Bahari ya Hindi, yanaambatana na matumizi meli zinazotumia teknolojia ya kisasa, boti za mwendo kasi, ndege zisizo na rubani na zana zingine za kisasa za kivita kutoka India zinazotumika kuondoa tishio linalofanyika kupitia baharini, anasema Waziri wa Ulinzi wa India, Sanjay Seth.
Meli hiyo ikiwasili kwenye bandari ya Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, inakusudia kutumia teknolojia ya kisasa kuimarisha ulinzi kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi, anasema Waziri Seth. .
Ufunguzi wa operesheni hiyo ya majini ulifanywa kwa pamoja na Mawaziri wa Ulinzi wa Tanzania, Dk. Stagomena Tax na India, Sanjay Seth.
Kadhalika wanaoshuhudia kuanza kwa zoezi hilo la kijeshi ni Mkuu ya Majeshi Jenerali Mkunda na Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Majini wa India, Admiro Dimesh Tripath.
Waziri wa Ulinzi, Dk. Stergomena, akizungumzia mazoezi hayo anasema kuwa Tanzania itanufaika kwa kupata ujuzi, uzoefu na uimara katika matumizi ya zana za kisasa za kiulinzi baharini.
Anasema:”Wanajeshi wa nchi zote watajifunza na kubadilishana uzoefu namna ya kupambana na uvuvi haramu, usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya na ugaidi unaofanyika baharini.”
“Wenzetu India wana meli za kisasa zaidi, vifaa, ujuzi na utaalamu kupitia teknolojia yao tutaweza kupata uzoefu katika kuilinda nchi na matukio ya baharini na hivyo kutuwezesha kukuza uchumi wetu wa bluu,” anaongeza Dk. Stergomena.
Anasema mazoezi hayo yanatokana na ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, alipoitembelea India mwaka 2023 na kukubaliana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Narendra Modi, kushirikiana kwa sekta mbalimbali ikiwamo kijeshi.
“Tutahakikisha kama Tanzania tunakuwa wenyeji wa kukumbukwa katika zoezi hili, tunataka kuona kila tunalojifunza na kubadilishana teknlojia linakuwa na faida chanya kwetu,” anasisitiza Waziri Stergomena.
India ni mojawapo ya mataifa yanayonufaika na Bahari ya Hindi anasema Waziri wa Ulinzi Sanjay Seth, akiongeza kuwa nchi yake imeamua kufanya mazoezi hayo na mataifa ya Afrika kutokana na ukaribu wa kiukanda wa bahari na pia utamaduni unaofanana na kushabihiana kwenye uchumi na kihistoria.
Anaeleza kuwa kutokana na dunia kwenda kasi katika teknolojia ya kisasa kuanzia ulinzi, biashara, uchumi , ni jambo jema kuona nchi nyingine zinanufaika hasa katika vifaa na ujuzi wa ulinzi wa baharini.
“Wanajeshi wa nchi zote kupitia AIKEYMA wanabadilishana ujuzi na uzoefu namna ya kupambana na biashara ya dawa ya kulevya, uvuvi haramu na usafirishaji binadamu kwa ajili ya kulinda amani na kuleta maendeleo katika mataifa yetu yanayopakana na Bahari ya Hindi,” anasisitiza Seth.
Anasema kwa washiriki watabadilishana uzoefu katika matumizi ya zana za kisasa kuilinda bahari na hatimaye kila nchi ikanufaika na uchumi wa bluu.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi, Jenerali Mkunda, anawataka wananchi wasiwe na hofu wanapoona vifaa vya kijeshi baharini, akiwaeleza kuwa ni jambo la kawaida na endelevu kufanya shughuli za kiulinzi na usalama eneo hilo.
“Ni jambo la kawaida kwa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania kufanya mazoezui ya pamoja na nchi mbalimbali rafiki.”
“Hili zoezi la AIKEYME, tunataka kuona ni namna gani tunapambana na matukio ya baharini kwa pamoja na wenzetu wa india kwa ufanisi na kwa kisasa zaidi.”
Jenerali Mkunda anaeleza kuwa kufanya mazoezi kama haya na nchi rafiki ni zoezi la kila wakati na kukumbusha kuwa mwaka jana walifanya na China, mwaka huu pia walikuwa na Wamarekani na kwamba yote hayo ni kuona namna Tanzania inavyoweza kupambana na matishio ya kihalifu baharini.
VIFAA
Wakati mazoezi ya zana za kijeshi yanaendelea kufanyika baharini karibu na pwani ya Dar es Salaam, kampuni mbalimbali za India zilifanya maonyesho ya vifaa mbalimbali vya kijeshi ambavyo vinaweza kutumika katika matukio mengi ya kusaidia na kuhudumia raia.
Vifaa vilivyoonyesha ni pamoja ya ndege za kisasa za uchunguzi, ndege zisizo na rubani ‘droni’ na zana zingine za kupambana na matishio ndani ya bahari.
Moja ya zana iliyoonekana kuwavutia wengi ni ndege isiyo na rubani ambayo inafanya kazi mbalimbali ikiwamo matumizi ya kivita, uchunguzi wa baharini na ardhini pia.
‘Droni’ hiyo aina ya ‘Switch UAV’, inatumia mfumo wa kisasa na ina uwezo wa kutumika pia katika shughuli za kirai kama kutafuta na kulinda wanyamapori, kuangalia wingi wa samaki baharini na kutumika katika kupiga picha kwa matumizi ya kuhifadhi data ardhi na rasilimali mbalimbali.
“Ndege hizi zisizo na rubani pamoja na kutumika katika masuala vita au kupambana na matishio ya baharini, ni msaada katika shughuli mbalimbali za kijamii,” Anasema mmoja wa washiriki wa maonyesho hayo Tushar Bidawe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED