Wanasayansi wanavyokuna kichwa kufupisha muda wa matibabu ya TB

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:15 PM Sep 18 2025
Mgonjwa wa TB
Picha: Mtandao
Mgonjwa wa TB

JUHUDI za kufupisha muda wa matibabu ya kifua kikuu (TB), zinaelezwa kupiga hatua katika miaka ya karibuni, lakini matokeo mapya yanaonesha kuwa njia hiyo mpya bado imejaa changamoto.

Kwa miaka mingi, wagonjwa wenye kifua kikuu sugu dhidi ya dawa wamekuwa wakitibiwa kwa mpango wa kawaida wa dawa za kila siku kwa muda wa miezi sita.

Wanasayansi wamekuwa wakitafuta njia fupi zaidi ya tiba, ili kupunguza mzigo kwa wagonjwa, kuongeza ufuasi wa matibabu na kupunguza gharama kwenye mifumo ya afya.

Hata hivyo, katika makala ya maoni yaliyochapishwa kwenye jarida maarufu la kitabibu la ‘The Lancet Infectious Diseases’, inapendekeza kwamba kupunguza muda wa matibabu ni jambo tata zaidi kuliko inavyotarajiwa.

Makala hiyo inazingatia jaribio la kitabibu liitwalo “Clo-Fast trial”, ambalo lilichunguza usalama na ufanisi wa mpango wa dawa wa miezi mitatu wenye dawa tano ambazo ni isoniazid, rifapentine, pyrazinamide, ethambutol, na clofazimine.

Hiyo ni pale inapolinganishwa na matibabu ya kawaida ya miezi sita kwa wagonjwa wenye kifua kikuu.

Matokeo hayakuonesha ishara ya tija zaidi, kwani mpango mfupi wa dawa haukufanya kazi vizuri, huku kukiwapo viwango vya juu vya kifua kikuu kuendelea au kurudia.

Wanasayansi wanaeleza kuwa zaidi ya nusu, kwa maana ya asilimia 52 ya wagonjwa waliokuwa kwenye mpango wa miezi mitatu walipata matokeo yasiyoridhisha, ikilinganishwa na 27 waliokuwa kwenye mpango wa kawaida wa miezi sita.

Jaribio hilo lilikatishwa mapema, kwa kuwa washiriki wengi walikuwa na kifua kikuu kikali na viwango vya juu vya bakteria, jambo lililofanya matibabu mafupi kubeba tafsiri ya kutokuwa na ufanisi.

Wataaluma hao, pia wakafanya jaribio lingine liitwalo ‘TRUNCATE-TB’, la mipango ya wiki nane hadi 12, kwa wagonjwa wa kifua kikuu isiyo kali, ambalo nalo halikusonga katika tija iliyotarajiwa.

Inatajwa kwamba, ikaoonesha kuwa washiriki wachache walihitaji matibabu ya nyongeza, jambo linaloonesha kwamba ukali wa ugonjwa kifua kikuu, unaathiri sana matokeo.

Watafiti pia wakabainisha changamoto katika kufuatilia madhara. Wagonjwa mara nyingi huanza tiba ya kifua kikuu, wakiwa na afya dhaifu na ilikuwa vigumu kutofautisha kati ya dalili za kawaida za kupona na athari halisi za dawa.

Watafiti wanapendekeza kwamba, majaribio yajayo yatahitaji vigezo maalum vya usalama na zana sahihi zaidi za kupima madhara na mafanikio ya matibabu.

WATAALAMU WANENA

Tanzania nayo haiko nyuma, kwani mwanasayansi wa Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Beno Mbeya, akachangia maoni kwenye makala hayo, yakilenga kusaidia kukuza uelewa kimataifa kuhusu mikakati ya matibabu ya kifua kikuu.

Hapo inajumuisha maneo kama ya kutoa mbinu muhimu za ufuatiliaji wagonjwa, uvumilivu wa dawa na usanifu wa majaribio.

Maoni mengine ya kitaalamu nchini yanatoka kwa Mtanzania, Ombeni Chimbee kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa – Kituo cha Utafiti Mbeya (NIMR-MMRC), Tanzania.

Pia, kuna raia wa kigeni: Joanitah Nalunjogi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya cha Makerere, Uganda; na Ivan Noreña na Norbert Heinrich kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza na Tiba ya Kitropiki katika Chuo Kikuu cha LMU, Ujerumani.

Wataalamu wanaeleza umuhimu wa kuboresha matibabu ya kifua kikuu, wakieleza mipango mifupi inabakia kuwa lengo kuu, matokeo ya Clo-Fast yanaonesha kwamba mtazamo wa “njia moja kwa wote” unaweza kuwa si salama wala wenye ufanisi. 

Aidha, wanapendekeza tiba ya miezi sita inabakia kuwa chaguo la kuaminika zaidi.

Katika matokeo mengine ya utafiti wa karibuni, wanasayansi wanaeleza kuwa kifua kikuu kinalazimu kutibiwa kwa muda mrefu zaidi kwa kuwa kinga za mwili inasaidia bakteria aina ya Mycobacterium tuberculosis, anayesababisha maradhi hayo kujificha.

“Hatari kubwa ya ugonjwa huu ni uwezo wake wa kuingia katika hali ya “usingizi” anaeleza mtaalamu. Katika hali hiyo ya ukimya, bakteria hawatoi dalili zozote, lakini husalia wakipinga dawa nyingi zilizopo. 

Baadaye, kinga ya mwili inapodhoofika, wanaweza ‘kuamka’ na kusababisha ugonjwa hai, ambao wakati mwingine huwa hatari kwa maisha.

Ili kuchunguza namna kifua kikuu inavyoingia katika hali ya usingizi, watafiti walitengeneza makundi ya chembechembe za kinga zinazozunguka bakteria wa maabara chuo kikuu, wakitumia sampuli za damu kutoka kwa wagonjwa wa kifua kikuu waliojitolea kwenye afya nchini Tanzania. 

Wakabaini kwamba, walipotumia chembechembe za wagonjwa, bakteria waliingia usingizini haraka zaidi.

Mhusika mkuu akabainika kuwa na ‘molekyuli’ inayoitwa granulysin, protini inayozalishwa na chembe za kinga mwilini na inafanya kazi kama ‘molekyuli muuaji’ kuharibu bakteria, ikiwamo wanaosababisha shida hiyo inayojadiliwa.

Ufunikaji bakteria kwa ‘granulysin’, hata ukiwa katika kiwango cha chini kisichotosha kuwaua, inatajwa kuwasukuma kuingia kwenye usingizi, hali inayowawezesha kuishi.

“Katika utafiti huu, tumefafanua jukumu la granulysin katika kusababisha usingizi wa bakteria hawa,” wanaeleza wataalamu.

Wanaendelea: “Matokeo yetu yanaonesha kuwa shughuli za ‘granulysin’ ni sehemu muhimu ya kinga ndani ya granuloma, zinazolazimisha ‘Mycobacterium Tuberculosis’ kujibu kwa kuingia usingizini, kisha kuamka pale mwenyeji anapodhoofika kinga,” 

“Mfumo wa kinga unajaribu kupambana, lakini katika kufanya hivyo, unaweza pia kuwasaidia bakteria kujificha na kuendelea kuishi,” inafafanuliwa

Hali hiyo inatajwa kuwa vita ya siri kati ya kifua kikuu na kinga ya mwili, inaeleza kwanini tiba huhitaji miezi mingi na kurudia kwa maambukizi ni jambo la kawaida.

Wanaeleza kuwa, mara nyingi dawa za kifua kikuu hushindwa kuwaangamiza bakteria waliolala kwa sababu hawakui wala kugawanyika. 

Utafiti huo unaweza kufungua njia ya tiba mpya zinazozuia kifua kikuu kisiingie katika hali hiyo ya usingizi kuanzia mwanzo.

Pia, utafiti uliochapishwa katika jarida la European Journal of Immunology, uliofanywa na timu kubwa ya watafiti kutoka taasisi mashuhuri, zikiwamo:

Taasisi ya Uswisi ya Afya ya Kitropiki na Umma (Swiss TPH), Chuo Kikuu cha Basel nchini nchini humo, Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) nchini Tanzania, pamoja na washirika kutoka Ulaya na Marekani.

Taasisi ya Afya Ifakara, ilishiriki kwa kiasi kikubwa katika utafiti huu, kupitia wanasayansi akiwamo Max Mpina, Anneth Tumbo, Elirehema Mfinanga, Frederick Haraka, Hellen Hiza, Mohamed Sasamalo na Jerry Hella.

Wakahusika kwa ukaribu katika kukusanya sampuli za wagonjwa, kufanya majaribio ya chembeza kinga na kuchambua data. Mchango wao ulikuwa wa msingi katika mapambano dhidi ya kifua kikuu.