Aziz Ki tishio mabao mguu wa kushoto

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:39 PM Mar 23 2025
Aziz Ki tishio mabao mguu wa kushoto
Picha: Mtandao
Aziz Ki tishio mabao mguu wa kushoto

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, anaongoza kwa kufunga mabao mengi kwa kutumia mguu wa kushoto mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.

Mchezaji huyo raia wa Burkina Faso, amepachika jumla ya mabao sita, akitumia mguu huo, katika mabao yake saba aliyofunga mpaka sasa.

Bao moja lililobaki alilifunga kwa kichwa, ambalo alilifunga Februari 28, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya timu yake dhidi ya Pamba Jiji uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kushinda mabao 3-0.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na Bodi ya Ligi, jumla ya wachezaji wanne wanashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao matano kila mmoja kwa mguu wa kushoto.

Wachezaji hao ni Gilbril Sillah wa Azam FC ambaye amefunga jumla ya mabao saba, Offen Chikola wa Tabora United ambaye pia amepachika jumla ya mabao saba, Nassor Saadun wa Azam FC ambaye mabao yake yote matano aliyoyafunga kwenye ligi ameyafunga kwa mguu wa kushoto pamoja na Selemani Bwezi wa KenGold, ambaye amepachika mabao yote matano kwa mguu huo.

Nafasi ya tatu inachulikuwa na Joshua Ibrahim ambaye kwa sasa anaichezea Namungo FC, lakini mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu alikuwa akikipiga kwenye klabu ya KenGold.

Mchezaji huyo amefunga jumla ya mabao matano hivyo ni moja tu ambalo hakufunga kwa mguu wa kushoto.

Wakati huo huo kikosi cha Yanga kilitarajia kuondoka jana jijini Dar es Salaam na treni ya kisasa, SGR, kuelekea Dodoma, ambapo kitakuwa njiani kwenda Singida, kucheza na Singida Black Stars mchezo maalum wa kirafiki utakaopigwa kesho kwa ajili ya kuzindua uwanja mpya.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kikosi hicho ni cha wachezaji ambao hawakuitwa kwenye timu za taifa ambao watakwenda kutoa burudani safi kwa wakazi wa Singida.

"Wachezaji wote ambao hawajakwenda kwenye majukumu ya timu ya taifa ndiyo tutakaokwenda nao, maana yake tuna kina Pacome Zouzoua, Aziz Ki na wengine ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa," alisema.

Hata hivyo, Yanga itamkosa Aziz Ki, ambaye pamoja na kwamba hajachaguliwa na kikosi cha timu ya taifa ya Burkina Faso, lakini anasumbuliwa na majeraha ya mgongo, kwa mujibu wa meneja wa timu hiyo, Walter Harrison.

"Aziz Ki, ana shida ya mgongo unamsumbua, hayupo kwenye mazoezi ya hapa, madaktari wanamtibia na kuangalia ni jinsi gani anaweza kurejea haraka iwezekanavyo, waliobaki wote wapo, isipokuwa wale ambao wapo kwenye majukumu ya timu za taifa," alisema meneja huyo.

Mgeni rasmi katika mchezo wa kesho ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, maarufu kama MwanaFA, ambaye ataufungua uwanja huo uliopo maeneo ya Mtipa mjijni Singida unaomilikiwa na klabu hiyo ya Singida Black Stars.