Fadlu aanika mbinu za kuwakaanga Waarabu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:28 PM Apr 02 2025
Nyota wa Simba, Elie Mpanzu (kushoto) na Kibu Denis wakikabana kwenye mazoezi ya mwisho ya timu hiyo jana kuelekea mchezo wao wa leo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry utakaochezwa nchini Misri
Picha: Mtandao
Nyota wa Simba, Elie Mpanzu (kushoto) na Kibu Denis wakikabana kwenye mazoezi ya mwisho ya timu hiyo jana kuelekea mchezo wao wa leo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry utakaochezwa nchini Misri

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameanika mbinu zake zote atakazotumia kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Al Masri, utakaochezwa leo, saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania kwenye uwanja wa New Suez, nchini Misri.

Fadlu amesema yeye na wachezaji wake hawana presha kuelekea kwenye mchezo wa leo, akiweka wazi anataka kuumiliki mchezo wa leo kama alivyofanya kwenye michezo miwili ya hatua za makundi ya michuano hiyo, dhidi ya CS Constantine ya Algeria na Bravo do Maquis ya Angola.

"Nakumbuka michezo miwili tuliocheza ugenini kwenye hatua ya makundi, mmoja tukipoteza na mwingine tulitoa sare, ukiingalia tulimiliki pia mpira tukicheza nje ya uwanja wetu wa nyumbani, tulipiga mashuti mengi kwa wapinzani wetu, tuliwashambulia hasa, nataka na mchezo huu tufanye hivyo, timu hii inazidi kujengeka siku hadi siku na sasa tumeingia kwenye hatua kubwa zaidi, tunatakiwa tuonyeshe nini tunatakiwa kufanya pamoja na kuonyesha ukubwa wetu," alisema Fadlu.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutowapa mwanya wapinzani wao kuwashambulia kwa muda mrefu, lakini pia kupata mabao kwenye mchezo huo wa ugenini ambayo yatarahisisha kazi katika mchezo wa marudiano nyumbani, Jumapili ijayo.

"Lengo letu ni lile lile ambalo nimekuwa nikirudia, kufunga bao moja au zaidi kwenye mchezo huu, hilo ndiyo lengo namba moja kwanza, ni muhimu sana kwenye michuano hii hatua za mtoano,  hata kama ukishinda, sare au kufungwa, lakini unaweza kusonga mbele kwa kuvushwa na bao au mabao ya ugenini, bila shaka tutajaribu kuhakikisha tunalinda lango letu, lakini kupata bao ni muhimu," alisema Fadlu.

Akiwazungumzia wapinzani wao, Al Masry, alisema ni timu nzuri, yenye wachezaji wanyumbulifu, hivyo amewaelekeza wachezaji wake nini cha kufanya.

"Al Masry ni timu nzuri, yenye kiwango kikubwa, wachezaji wao wengi ni wanyumbulifu, wanacheza na mabeki watatu nyuma, wanapenda kushambulia sana, kwa maana hiyo tutalazimika kuwanyima nafasi, lakini pia na sisi kuwashambulia tutakapokuwa tunapata mpira," alisema.

Alisema kipa wake namba moja, Moussa Camara, anaendelea na mazoezi kama kawaida, yupo fiti lakini yeye hawezi kusema kitu chochote mpaka akatakapoletewa jina la kipa atakayekuwa fiti kwa asilimia 100 kwenye mchezo huo kutoka kwa kocha wa makipa.

Ikumbukwe kuwa Camara hakucheza mchezo wowote tangu alipoumia kwenye mechi kati ya Simba dhidi ya Azam FC, uliochezwa, Februari 24, mwaka huu.

Kocha huyo alisema kuwa amefurahia timu yake kufika mapema nchini Misri na kuzoea hali ya hewa ambayo haitowapa tabu kuelekea kwenye mchezo wa leo.