Katambi akabidhi milioni 2.6/- vikundi michezo ya jadi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:39 PM May 19 2025
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Samweli Jackson akikabidhi kiasi cha fedha sh.milioni 2.6 kwa viongozi wa michezo ya Jadi wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kugawiwa vikundi 26 ambapo kila kikundi kitapewa sh. 100,000
Picha: Marco Maduhu
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Samweli Jackson akikabidhi kiasi cha fedha sh.milioni 2.6 kwa viongozi wa michezo ya Jadi wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kugawiwa vikundi 26 ambapo kila kikundi kitapewa sh. 100,000

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, amekabidhi vikundi vya michezo ya jadi, kwa kutoa Sh. milioni 2.6 kama zawadi kwa washiriki wa mashindano hayo.

Fedha hizo zimekabidhiwa leo Mei 19, 2025 na Katibu wa wake Samweli Jackson, kwa niaba ya Mbunge Katambi, katika hafla fupi iliyofanyika Ofisi ya Mbunge.

Samweli akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo amesema  kuwa Mbunge Katambi ametoa ahadi hiyo Mei 16, mwaka huu, wakati wa fainali ya michezo jadi iliyofanyika katika viwanja vya CCM Kambarage, akiahidi zawadi ya Sh. 100,000 kwa kila kikundi kilichoshiriki.

“Mbunge Katambi ndiyo mdhamini wa mashindano haya ya michezo ya jadi na alitoa zaidi ya Sh. milioni sita, na kama sehemu ya kuthamini ushiriki wa vikundi vyote, aliahidi kuwapa zawadi ya Sh. 100,000 kwa kila kikundi, leo ametimiza ahadi hiyo kwa vikundi 26,na nimekabidhi Sh. milioni 2.6,” amesema Samweli.

Amesema kuwa, Katambi ameahidi kuendelea kuunga mkono michezo hiyo ya jadi, kwa lengo la kuenzi na kudumisha mila na desturi za kitanzania.

Katibu wa Michezo ya Jadi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fabiani Francis, amempongeza Mbunge huyo pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zao za kufufua michezo hiyo ambayo ilikuwa imesahaulika kwa muda mrefu.

“Michezo ya jadi ni muhimu katika jamii, sababu ni kielelezo cha Taifa na urithi wetu,” amesema Fabiani.

Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Janeth Seseja, amemshukuru Katambi kwa moyo wake wa kujitolea na kusaidia kuendeleza michezo ya jadi.

Baadhi ya wawakilishi wa vikundi vilivyopokea zawadi hizo, akiwamo Shoka Binkisu, wamemshukuru Katambi kwa kuwa karibu na wananchi na kuonyesha kuguswa na matukio ya kijamii, huku wakimpongeza kwa moyo wake wa kutoa.