Kibu: Mechi Simba, Yanga ndizo zangu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:07 AM Mar 05 2025
Kibu Denis
Picha: Mtandao
Kibu Denis

KLABU ya Simba imesema mchezo wa Jumamosi dhidi ya Yanga umebeba hatma, mustakabali na heshima yao, huku winga, Kibu Denis, akibainisha kuwa katika mechi ambazo hucheza kwa ufanisi na kujituma zaidi ni dhidi ya Yanga.

Kibu ambaye mara kwa mara huwasumbua sana mabeki wa Yanga, kiasi cha kumfanya baadhi ya mechi kufanyiwa madhambi, wakati mwingine kushindwa kuendelea na mchezo, jana jijini Dar es Salaam alisema yeye hupenda kucheza mechi za aina hiyo.

"Mimi katika mechi ambazo napenda sana kuzicheza kwa ufanisi, nguvu na kujituma zaidi ni dhidi ya Yanga, ila kwa sasa sitaki kusema mengi kwa sababu ndiyo tunakwenda kujiandaa na mchezo wenyewe," alisema Kibu.

Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, jana jijini Dar es Salaam, alisema kikosi cha timu hiyo kimeingia kambini tangu Jumatatu jioni wiki hii, kwa ajili ya mchezo huo wa dabi, huku akisema wachezaji wao Fondoh Che Malone na Moussa Camara ambao hawakucheza mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union, wameshapona na watakuwapo kwenye mchezo huo.

"Mechi ya Jumamosi imebeba vitu vingi sana, hatma, mustakabali na heshima yetu, kikosi imeingia kambini tangu Jumatatu kuanza rasmi mazoezi na maandalizi ya mchezo huo.

"Kwa sasa sitosema chochote kwa sababu wachezaji ndiyo wana siku ya pili leo kwenye maadalizi, tusubiri kwanza mazoezi yachanganye, ila cha kuwaambia wanachama na mashabiki wa Simba ni kwamba tunakwenda kucheza mechi yenye umuhimu mkubwa na ngumu Jumamosi, kifupi tu niwaambie wale jamaa, ubingwa wetu msimu huu wanao wao," alisema Ahmed.

Simba itaingia kwenye mchezo wa Jumamosi ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo minne mfululizo, mitatu ikiwa ni ya Ligi Kuu, mmoja wa Ngao ya Jamii.

Novemba 5, 2023, ilichakazwa mabao 5-1, katika mchezo wa mzunguko wa kwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, kabla kuchapwa mabao 2-1, mchezo wa mzunguko wa pili uliopigwa Aprili 20, 2023.

Kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii, kuashiria kuanza kwa msimu mpya, Simba ilipoteza tena kwa bao 1-0, Agosti 8, kabla ya kupokea kipigo kama hicho, mchezo wa mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, mechi ikipigwa Oktoba 19, mwaka huu.

Mechi zote hizo zilichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo ya Oktoba 19, ndiyo mchezo pekee ambao Simba ipoteza kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, ikiwa chini ya kocha Fadlu David, raia wa Afrika Kusini, aliyeichukua timu hiyo kutoka kwenye mikono ya Juma Mgunda, ambaye alikaimu baada ya kuondoka kwa kocha raia wa Algeria, Abdelhak Benchikha.