Miloud ataja siku ya mwisho kwa wasugua benchi Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:20 AM Mar 03 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, amesema hadi kufikia Mei mwaka huu, hakuna mchezaji yeyote wa Yanga aliyesajiliwa msimu huu ambaye hatapata nafasi ya kucheza kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo amesema anataka wachezaji wote waliosajiliwa wacheze na waipe mafanikio klabu, kuwafurahisha mashabiki na wao wenyewe kutengeneza wasifu wao kwa maisha yao ya baadaye kwenye soka.

Miloud aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, huku akifafanua kwamba amekuwa akifanya mabadiliko ya wachezaji wengi kipindi cha pili kwenye kikosi cha Yanga tangu aanze kukinoa kwani anahitaji awaone wachezaji wote, viwango vyao, ili aweze kuchukua maamuzi sahihi mwishoni mwa msimu.

Alisema anawaheshimu wachezaji wote aliowakuta, hivyo atawapa nafasi wamwoneshe walichonacho, huku akisema hapendi wachezaji ambao wanaridhika na kukaa benchi.

"Nataka hadi kufika Mei, wachezaji wote waliosajiliwa Yanga wawe wamecheza mechi za Ligi Kuu na Kombe la FA.

"Nimeanza kuwatengeneza wachezaji wote wawe wana uwezo wa kuisaidia timu kwani hawakusajiliwa Yanga kwa ajili ya mafunzo, bali kuja kufanya kazi, kuisaidia klabu kwenye malengo yake, kuwafurahisha mashabiki na wao wenyewe wasonge mbele kwenye maisha yao ya soka," alisema kocha huyo.

Miloud, alipewa mikoba ya kuifundisha Yanga baada ya kuondoka kwa Sead Ramovic, ambaye ametimkia CR Belouizdad ya Algeria.

Kabla ya kutua Yanga, alikuwa kocha wa Singida Black Stars, ambako hakuwahi kuiongoza timu hiyo kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu.

Kocha huyo ameiongoza Yanga kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu, akishinda minne na kutoka sare mmoja.

Alianza na mguu mbaya, timu yake ikitoka suluhu dhidi ya JKT Tanzania, Februari 10, mwaka huu, lakini baada ya hapo, alipata ushindi wa michezo minne mfululizo, akiiongoza Yanga kushinda mabao 6-1 dhidi ya KMC, 2-1 dhidi ya Singida Black Stars, 5-0 dhidi ya Mashujaa FC na 3-0 dhidi ya Pamba Jiji.

Akiwa Kocha Mkuu, ameiwezesha Yanga kuvuna pointi 13, mabao 16, ikiruhusu nyavuni kwake mabao matatu pekee.