Mukwala, Nouma wamvuruga Fadlu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:14 AM Mar 03 2025
Steven Mukwala
Picha: Mtandao
Steven Mukwala

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kikosi chake sasa kiko tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga, unaotarajiwa kuchezwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Jumamosi wiki hii.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi kati ya timu hiyo na Coastal Union, uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha juzi na kushinda mabao 3-0, Fadlu, alisema anaamini itakuwa mechi nzuri, huku akithibitisha kuwa wachezaji wake Fondoh Che Malone na Moussa Camara, watakuwa sehemu ya kikosi baada ya kutokuwapo kwenye mchezo wa juzi kutokana na kuwa majeruhi.

Fadlu pia alifurahia uwezo mkubwa uliooneshwa na wachezaji ambao wamekuwa hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza, akisema wamemfanya kutafakari upya juu ya kupanga kikosi cha kuanza kwenye mchezo huo.

"Steven Mukwala alikuwa bora sana dimbani akicheza kwa faida ya timu huku akikaa kwenye maeneo sahihi ambayo yamemfanya afunge mabao matatu peke yake, 'hat-trick', licha ya kutopata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kwa muda mrefu leo nimempa nafasi na amefanya makubwa dimbani, nimefurahi kwa Salim Ali kuanza na kucheza kwa ustadi wa hali ya juu kiasi cha kumaliza akiwa na 'clean sheet', Kameta (Duchu) pia alitoa 'asisti', Debora Fernandes naye ameonesha kuwa anaitaka namba, viwango vyao vimenichanganya kiasi cha kufikiria upya upangaji wa kikosi kitakachoanza Jumamosi," alisema kocha huyo.

Katika mchezo wa juzi, Simba ilichezesha wachezaji sita ambao hawapati nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza ambapo mbali na Mukwala, Salim na Fernandes, wengine ni David Kameta, Valentin Nouma, na Chamou Karaboue.

Kocha huyo alisema aliamua kuwapumzisha baadhi ya wachezaji baada ya kucheza mechi kubwa, yenye kasi dhidi ya Azam FC, huku wakikabiliwa na mechi nyingine ngumu dhidi ya Yanga.

"Nina wachezaji ambao wanaweza kukupa kitu kile kile, wameonesha kwenye mchezo huu, nina kikosi bora, kwa maana hiyo tuko tayari kwa dabi. Najua wengi wanadhani kutakuwa na kitu tofauti, lakini mpira ni ule ule, tunajua tunakwenda kucheza na timu kubwa kama Simba, lakini tunachohitaji ni pointi tatu, si kwenye mechi hiyo tu, mpango wetu ni kwamba tupate ushindi michezo yote iliyobaki na kuwa mabingwa," alisema Fadlu.

Naye kipa Salim, alisema siri ya kubaki na kiwango bora licha ya kutocheza kwa muda mrefu ni uwezo mkubwa wa ufundishaji wa kocha wao, Wayne Sandlands, ambaye ni kipa wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates za Afrika Kusini.

"Kocha anapenda kuona makipa wake wapo fiti muda wote ili ikitokea changamoto yoyote mwenzake awe na uwezo wa kuziba nafasi yake bila kufanya makosa yoyote yale na kwa uwezo ule ule," alisema kipa huyo ambaye aliokoa hatari tatu kwa ustadi wa hali ya juu huku akishangiliwa na mashabiki waliojazana uwanjani hapo.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mwambusi, alishusha lawama kwa wachezaji wake kwa kile alichokiita uzembe na ukosefu wa umakini.

"Ni uzembe na ukosefu wa umakini, mara nyingi huwa tunawakumbusha wachezaji kwenye viwanja vya mazoezi, mpira unapokuwa kushoto basi ujue kulia kutakuwa na matatizo, ina maana ndipo kuna hatari kuliko ambako kuna mpira, ukiangalia mechi hii ni kwamba tumeitupa sisi wenyewe kwa kuwapa mabao rahisi mawili kipindi cha kwanza, kusema kweli ni masikitiko, lakini nitakwenda kukaa tena na wachezaji wangu kuona nini ambacho tunatakiwa kufanya, lakini kama timu hatukucheza kama vile ambavyo tuliambizana kucheza," alisema Mwambusi.

Baada ya michezo 21, Simba yenye mchezo mmoja mkononi imefikisha pointi 54, ikizidi kuifukuza Yanga juu ya msimamo yenye pointi 58, Coastal Union ikibaki na pointi zake 24 kwenye nafasi ya tisa.