Nahimana kinara kuokoa penalti, akunwa na Ahoua

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:08 AM Mar 03 2025
Jonathan Nahimana
Picha: Mtandao
Jonathan Nahimana

GOLIKIPA wa timu ya Namungo FC, Jonathan Nahimana, anaongoza kwa kuokoa michomo ya penalti kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, huku mwenyewe akimsifu Kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua kuwa ni mmoja wa wapigaji hatari anayewahofia.

Kipa huyo raia wa Burundi, ameokoa penalti tatu mpaka sasa kati ya tano ambazo amepigiwa, huku Ahoua akiwa mchezaji pekee Ligi Kuu msimu huu hadi sasa, aliyemgeuza kuokota mpira kambani kwa njia ya matatu.

Nahimana amefungwa penalti mbili ambazo zote ziliwekwa nyavuni na Ahoua kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa, Februari 19, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, Simba ikishinda mabao 3-0.

Kipa huyo amesema Ahoua ni mpigaji penalti mzuri ambaye hata yeye pamoja na umahiri wake wote, anampa tabu kuokoa kwa jinsi anavyopiga.

"Katika mchezo dhidi ya Simba zilipigwa penalti tatu, nilifanikiwa kudaka ile ya Ateba, lakini za Ahoua ilikuwa ngumu sana, ni mchezaji ambaye amenipa wakati mgumu zaidi kwenye ligi, maana amepiga penalti mbili dhidi yangu na zote nimeshindwa kuzizuia, wakati si kawaida," alisema Nahimana.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu Dawati la Michezo, Nipashe (KTDMN), kipa huyo ameokoa michomo mitatu, ambapo mbali na penalti hiyo ya Ateba, ndani ya wiki moja tu aliokoa penalti nyingine ya Feisal Salum wa Azam FC, katika mchezo dhidi ya Azam FC, uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Februari 23, mwaka huu, timu yake ikilazimisha sare ya bao 1-1.

Penalti yake ya kwanza msimu huu, Nahimana kuokoa, ilikuwa ni Desemba 25, mwaka jana, kwenye mchezo kati ya timu yake na Fountain Gate, katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

Penalti hiyo ilipigwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Nicolaus Gyan, lakini aliiokoa na kuifanya Namungo kutoka na ushindi ugenini wa mabao 2-1.

Alitamba kuwa ana uwezo wa kuokoa penalti sita kati ya kumi anazopigiwa, huku akisema ataendelea kujifua zaidi ili aendelee kuokoa penalti, akiamini kuwa mafanikio aliyopata katika michezo hiyo miwili ya karibuni, yamemjenga kisaikolojia na kuongeza kujiamini kwake langoni.

Anayeshika nafasi ya pili ni Ramadhani Chalamanda wa Kagera Sugar, aliyeokoa penalti ya kwanza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Oktoba 29, mwaka jana, wakati timu yake ikicheza dhidi ya Coastal Union, ikipigwa na Maabad Maulid, mechi iliyoisha kwa timu yake kufungwa bao 1-0.

Alifuta penalti nyingine dhidi ya Yanga, mchezo uliochezwa, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Februari Mosi, mwaka huu, iliyopigwa na Stephane Aziz Ki, ingawa alifungwa nyingine iliyopigwa na Pacome Zouzoua, mchezo ambao kwa mara nyingine tena timu yake ilipoteza kwa mabao 4-0.