Simba SC yaziota pointi 30 Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:05 AM Feb 28 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

WAKATI akili na nguvu za wachezaji na benchi la ufundi la Simba zimeelekezwa katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union inayotarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Wekundu wa Msimbazi 'wanaziota' pointi 30 zilizobakia msimu huu.

Kauli hiyo inamaanisha kwa sasa Simba imeipotezea na haitaki kuzungumzia mechi dhidi ya watani wao, Yanga itakayopigwa Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, huenda Simba ikawakosa  wachezaji wake wa kikosi cha kwanza akiwamo kipa, Moussa Camara na beki wa kati, Che Fondoh Malone, ambao ni majeruhi.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameliambia gazeti hili amewataka wachezaji wake kuupa umuhimu mchezo huo wa kesho na si kuwaza mechi nyingine tofauti na hiyo.

Fadlu alisema kwa sasa hana mawazo ya  kukutana na Yanga na badala yake anaifikiria zaidi Coastal Union, kwa sababu ni timu ambayo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ililazimisha kupata sare ya mabao 2-2.

"Siiwazi dabi kwa sasa, naiwaza Coastal Union, tulipoteza pointi mbili tukicheza nao kwenye Uwanja wa KMC Complex, wakati tunaongoza mabao 2-0, walirudisha yote kwa namna ambayo haielezeki, tunataka kusawazisha hilo kwenye mchezo wa Jumamosi.

Coastal wanacheza kitimu, wana wachezaji wazuri, tunajua watatupa tena wakati mgumu tutakapokutana," alisema Fadlu.

Aliongeza katika mchezo wa kesho atabadilisha staili ya uchezaji kutokana na aina ya uwanja wanaotarajia kuutumia.

"Kama kawaida tutabadilisha aina ya uchezaji kama tunavyofanya tukicheza kwenye viwanja vya ugenini, kama tulivyofanya dhidi ya Tabora United, Singida Black Stars na Fountain Gate.

Kuhusu Camara na Che Malone sina wasiwasi na hilo kwa sababu timu yangu ina kikosi kipana, chenye wachezaji ambao wanaweza kuziba nafasi hizo bila wasiwasi wowote," Fadlu aliongeza.

Winga wa timu hiyo, Kibu Denis, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kusahau matokeo ya sare ya mabao 2-2, ambayo waliyapata Jumatatu iliyopita walipokutana na Azam FC, na badala yake wawasapoti katika mchezo wa kesho ili kusaidiana kupata pointi tatu.

"Sare ilituumiza, lakini imeisha tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Coastal Union, sipo hapa kuzungumzia mechi dhidi ya Yanga, kwa sababu upo mchezo mwingine kabla ya huo na ni dhidi ya Coastal Union ambao ni muhimu sana," alisema Kibu.

Aliongeza anapuuza maneno ya baadhi ya mashabiki kuhusiana na kutofunga mabao kwenye Ligi Kuu, akisema yeye (Kibu), anachojali ni kuisaidia timu yake, haijalishi kama anafunga mabao au la.

"Mimi sizungumzii mabao, mimi naangalia mchango wangu kwenye timu, ningekuwa siyo muhimu singekuwa napangwa, kocha anaona umuhimu wangu ananipanga, goli litakuja tu, na mimi siangalii sana kuhusu bao, au watu wanasema nini, naangalia mchango kwa timu yangu, mabao yatakuja tu," aliongeza.

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema tayari wameanzisha kampeni ya kuhakikisha wanapata pointi zote 30 katika michezo yao 10 iliyosalia kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Matokeo ya mwanzo dhidi ya Coastal yanatuongezea umakini kuelekea kwenye mchezo huu, kwa jinsi ilivyo kwa sasa kila timu inacheza kwa malengo, hakuna timu inayocheza ili kukamilisha ratiba,  tunaanza kampeni ya kukusanya pointi 30 katika michezo 10," alisema Ahmed.