OFISA Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, amesema mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga maarufu Dabi ya Kariakoo, inayotarajiwa kuchezwa Jumamosi ijayo, saa 1:15, usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, haiwezi kuamua Bingwa wa Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamwe alisema anaamini kuwa bingwa msimu huu atapatikana kwa kuwa na pointi nyingi kuliko timu zingine 15 mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema ingawa kila timu inatamani ishinde mchezo huo kwa kuongeza pointi tatu na sababu ya historia, lakini mshindi katika mchezo huo hawezi kujihesabia kuwa ndiye atakuwa bingwa wa msimu huu.
"Sikubalini kwamba mechi hii ya dabi ndiyo inakwenda kuamua Bingwa wa Tanzania Bara msimu huu, tukicheza dhidi ya Simba tutakuwa tumebakisha michezo saba, kimahesabu Yanga tunatakiwa tupambanie pointi zingine 21, kwa hiyo unaweza kushinda Jumamosi, lakini ukajikuta una mzigo mzito au mlima mkubwa wa kupanda kupata hizo pointi 21, ingawa ni kweli utakuwa mchezo muhimu kushinda, lakini ni jambo la haraka sana kusema inakwenda kuamua bingwa wa msimu," alisema Ofisa Habari huyo.
Aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuipa sapoti timu hiyo kwani katika mchezo huo itakuwa ni mwenyeji, hivyo kujiandaa kuifunga Simba, lakini si kujiandaa na ubingwa.
"Nawaambia mashabiki wa Yanga tujiandae kuifunga Simba ili kupata pointi tatu zituweke vizuri kuelekea huko, tusijiandae kwa ajili ya ubingwa, hakuna bingwa atakayepatikana tu kwa ajili ya kumfunga mtani wake, bingwa atakuwa ni yule mwenye pointi nyingi baada ya michezo 30 kumalizika, au apate pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu zingine," alisema.
Akizungumzia maandalizi, alisema kikosi cha timu hiyo tayari kimeingia kambini kwa ajili ya mchezo huo ambao alitabiri utakuwa mgumu kwani watani zao watakuja kwa nguvu, si tu kutaka kushinda, bali kufuta uteja.
"Tuna rekodi nzuri, wengi wamekuwa wakisema hivyo na ndivyo ilivyo, tumeshinda mara nne mfululizo dhidi ya Simba, hiyo rekodi ndiyo inaongeza ugumu wa mchezo huo, wenzetu watakuja kupambana, si kupambana kushinda mechi, lakini kufuta uteja, tunajiandaa na hilo na tupo tayari na kwa maandalizi tunayoyafanya na viwango vya wachezaji wetu, tunaamini tunakwenda kushinda mchezo huu," Kamwe aliendelea kufunguka.
Akiuzungumzia mchezo huo wa dabi alisema ni mchezo mkubwa, wenye hadhi na thamani ya juu, Afrika kwa sasa.
"Ni mchezo mkubwa, wenye hadhi na thamani ya juu, tafiti mbalimbali zinaitaja dabi hii kuwapo kwenye dabi tano bora Afrika.
"Sisi kama Yanga tunafahamu ugumu wa mchezo huu, ukubwa wake na thamani ya kushinda mchezo huu, kitu ambacho nataka niwaambie wanachama na mashabiki wa Yanga ni kwamba tayari maandalizi ya mchezo huu yameanza, wachezaji wameshaingia kambini kwa ajili ya mchezo huu," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED