Yanga, Ihefu mechi ya kisasi leo

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:16 AM May 19 2024
Yanga, Ihefu mechi ya kisasi.
Picha: Maktaba
Yanga, Ihefu mechi ya kisasi.

YANGA leo inashuka kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini kusaka tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la FA itakapoumana na Ihefu kwenye mchezo wa nusu fainali.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akizungumzia mchezo huo wa leo, amesema wamejiandaa vizuri lakini angependa vijana wake wamalize kazi ndani ya dakika 90.

Gamondi amesema hatarajii mchezo mwepesi na hivyo wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi utakaowapeleka hatua ya fainali watakayocheza na Azam ambao jana walifanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kuifunga Coastal Union.

Gamondi, amesema malengo yao msimu huu ni kutwaa makombe yote ya ndani na wanahitaji ushindi leo kuweka hai malengo yao ya kuchukua vikombe vyote.

"Tulikuwa na melngo yetu tangu kuanza kwa msimu huu, asilimia kubwa tumefanikiwa, tumecheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sisi malengo yetu yalikuwa kufika hatua ya makundi, tumetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, sasa kazi imebaki kwenye michuano hii ya kombe la FA, tunalitaka," amesema Gamondi.

Amesema wanatarajia upinzani kutoka kwa Ihefu lakini amewataka wachezaji wake wapambane kuhakikish wanapata alama tatu na kwenda fainali ya michuano hiyo.

Kwa upande wake, Kocha wa Ihefu, Mecky Mexime, amesema vijana wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo wa nusu fainali.

Amesema wanafahamu ugumu wa wapinzani wao lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo wa nusu fainali.

"Tunawaheshimu yanga kwa ubora wao, wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu, lakini na sisi tumejiandaa kuhakikisha tunapata ushindi, litakuwa jambo zuri kama tutaingia fainali, tumejipanga kukabiliana nao," amesema Mexime.

Katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza jana uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Azam FC walifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 3-0.

Katika mchezo huo, Coastal Union licha ya kuonyesha upinzani mkubwa walishindwa kuzima ndoto za Azam za kutinga fainali ya pili ya michuano hiyo inayodhaminiwa na benki ya CRDB.

Azam sasa wanasubiri mshindi wa mchezo wa leo kucheza nao fainali itakayofanyika Juni 2 mkoani Manyara.

Mabao ya Azam jana yalifungwa na Abdul Suleiman 'Sopu' aliyefunga mabaomawili katika kila kipindi na Feisal Salum 'Fei Toto' aliyefunga kipindi cha pili.