TUTAENDELEZA vipigo, hizo ndio tambo za Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, kuelekea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji inayotarajiwa kuchezwa leo kuanzia saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Yanga itashuka dimbani katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Mashujaa FC mabao 5-0, mechi iliyochezwa Jumapili iliyopita mkoani Kigoma.
Akizungumza na gazeti hili jana, Miloud, amesema amekiandaa kikosi chake kwa mbinu na nguvu ile ile aliyoiandaa kabla ya kuwakabili Mashujaa FC, hivyo ana matumaini ya kufanya kama ilivyokuwa mchezo uliopita na kuvuna pointi tatu.
Miloud alisema wamejipanga kuendelea kutoa 'dozi kubwa' kwa wapinzani ili kujiimarisha zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Nimeiandaa timu yangu kama nilivyoiandaa katika mechi dhidi ya Mashujaa, kwa hiyo tutafanya kila kitu ili kufanya kama kile kile tulichokifanya kwenye mchezo uliopita ili kuchukua tena pointi nyingine tatu muhimu za ugenini," alitamba Miloud.
Kocha huyo alisema pia wataingia na mbinu ile ile waliyoitumia kuwamaliza Mashujaa na wanaweza kubadilika kutokana na namna wapinzani wao watakavyokuwa.
"Tuna mipango mikakati mingi katika mchezo huu, tunaweza kubadilika kadri mpinzani wetu anavyobadilika pia, lakini hapa siwezi kusema tutabadilika vipi, ni siri, ila mtaona katika mchezo wenyewe, ila kwanza kabisa tunaanza na mfumo tuliocheza dhidi ya Mashujaa," Miloud alisema.
Hata hivyo, kocha huyo alisema Pamba Jiji si timu mbaya kwa sababu ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Singida Black Stars, Jumapili iliyopita, lakini alibainisha tatizo la timu nyingi na makocha wa timu za daraja la kati ni uoga wa kufanya mashambulizi wanapokutana na timu kubwa.
"Ningekuwa Kocha wa Pamba nisingeingia kwa mbinu za kujilinda kwa sababu nao wanahitaji pointi, hivyo wanapaswa kucheza mpira, imetoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Singida Black Stars, timu nzuri, yenye wachezaji bora, kwa maana hiyo kama wakiamua wanaweza kushambulia na kufunga mabao pia," alisema kocha huyo.
Naye Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Minziro, alisema wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo wa mzunguko wa pili.
"Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata matokeo ya ushindi, tunakutana na timu nzuri, yenye wachezaji wenye viwango vya hali ya juu, ila na sisi kipindi hiki cha dirisha dogo tumeongeza nyota wazuri tu, kwa hiyo tunaamini itakuwa ni mechi ya aina yake.
Unapokutana na timu bora lazima uwe na mbinu mbadala ambazo zitakufanya uendane na jinsi mechi ilivyo, safari hii tuna wachezaji wazuri na wenye viwango vinavyokaribiana, kila namba ina wachezaji wawili wazuri," Minziro alisema.
Yanga itashuka katika mchezo huo ikiwa kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 55, ikicheza michezo 21 wakati Pamba Jiji iliyoanza msimu kwa kusuasua sasa imejikusanyia pointi 22 na wako katika nafasi ya 12.
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo ni kati ya Tabora United dhidi ya Dodoma Jiji.
Tabora United yenye pointi 34 iko katika nafasi ya tano kwenye msimamo wakati Dodoma Jiji yenye pointi 26 inahitaji kuvuna pointi tatu muhimu ili kujiweka mahali salama ili isikutane na janga la kushuka daraja.
Kagera Sugar ya Bukoba mkoani, Kagera yenye pointi 16 na KenGold ya jijini, Mbeya yenye pointi 14, zinaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED