UMEME ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kuanzia uchumi kwenye viwanda, biashara na kilimo mashambani.
Ni nguzo upatikanaji na utoaji huduma zote kuanzia mawasiliano, elimu, afya, usafirishaji na maji katika maeneo yote mijini na vijijini ambako shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na kutoa huduma zinafanyika.
Tanzania imevisambazia umeme vijiji vyote 12,318 na vitongoji kadhaa. Aidha, inatazamia kuongeza uwezo wa taifa wa kuzalisha umeme zaidi ufikie megawati 4,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kwenye Mto Rufiji linatarajiwa kuzalisha megawati 2,100 na mwaka jana ilishuhudiwa mitambo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1,400 ikifanya kazi.
Katika mkutano wa siku mbili wa 'Nishati Afrika' uliomalizika jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, anataja mafanikio mengi yaliyopatikana kitaifa.
Ni kusanyiko linawakutanisha marais kutoka nchi 24, mawaziri na wadau wa taasisi za fedha za kimataifa.
Anayesema hayo katika mkutano huo na kutaja maendeleo yaliyofikiwa na mataifa ya Afrika tangu mwaka 1960.
Katika ufafanuzi wake anasema Tanzania imeongeza uzalishaji wa nishati hiyo kutoka megawati 21 wakati wa uhuru hadi 3,160 na sasa imepiga hatua zaidi hadi kila kijiji kuwa na umeme.
Hiyo ni hatua ya kupongeza ambayo nchi imefikia ila ombi langu ni kwamba kasi ya kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo iongezeke, kwani kumekuwapo na tatizo la katizo la umeme kila mara.
Tanzania ina vyanzo mbalimbali vya nishati, vingezidi kuimarishwa ili kuwa na umeme wa uhakika ambao hauna changamoto utakaoweza kuuzwa nchi jirani na kuliongezea taifa mapato.
Kwa sasa Tanzania inaimarisha muunganiko wa Afrika au gridi ya Afrika, kwa miundombinu ya umeme inayounganisha Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda, ikiwa mbioni kuiunganisha na Zambia.
Hayo yakifanyika, nchi itakuwa na umeme wa kutosha, kwani hata Naibu Waziri Mkuu anakiri kwamba pamoja na maendeleo ya nishati taifa linayo ya kujivunia, bado inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati.
Ni wazi matarajio ya kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda, madini na huduma nyingine ni jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati kama anavyosema.
Umeme unahitajika kila mahali kuanzia hospitalini, uzalishaji viwandani, miundombinu ya usafiri na mawasiliano, darasani kufundisha wanafunzi, mashambani kwenye kilimo na jikoni kuandaa vyakula.
Ni hatua muhimu kwa nchi za Afrika Kusini ya Jangwa la Sahara kuweka mikakati ya kuhakikisha watu wake wanapata nishati hiyo.
Katika mkutano huo uliomalizika jana, imeelezwa kuwa wananchi
wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo na takribani Waafrika milioni 600 haujawafikia.
Wapo wengine wamegeukia nishati mbadala ikiwamo ya mionzi ya jua au sola kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
Afrika inatamani ifikapo mwaka 2030, watu milioni 300 wawe na nishati hiyo, huku njia mojawapo inayotajwa ya kufanikisha hilo ni kuunganisha nguvu na kushirikiana kupitia sekta ya nishati ili bara lifikie lengo hilo na kubadili sura yake.
Inaelezwa kuwa maendeleo yaliyofikiwa na mataifa ya Afrika tangu mwaka 1960, ni pamoja na Tanzania kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kutoka megawati 21 wakati wa uhuru hadi megawati 3,160.
Kimsingi, hiyo ni hatua ya kujipongeza hasa baada ya kufikisha umeme kila kijiji ili wakazi wa huko waweze kutumia umeme kujiletea maendeleo badala ya kuendelea kubaki nyuma.
Wanaoishi vijijini, wanaweza kutumia nishati hiyo kwa kuanzisha viwanda vidogo hata vya kusindika matunda, kuwa na mashine ya za kusaga nafaka, saluni za wanawake kwa wanaume, kuchomelea vyuma na migahawa ya vyakula na vinywaji kwa kutumia jokofu.
Jambo la muhimu ni kuombea malengo ya mkutano huo yafanikiwe ili idadi hiyo ya watu milioni 300 iweze kupata umeme ifikapo mwaka 2030 ambayo ni miaka mitano ijayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED