JUMAMOSI wiki hii, nchi inakwenda kushuhudia kwa mara nyingine tena mchezo wa 'Dabi' ya Kariakoo, kati ya timu mbili kubwa na kongwe nchini Tanzania, Simba na Yanga ambazo zitavaana vikali kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:15 usiku.
Ni moja ya mechi ambazo husimamisha nchi kwa dakika 90 ikifuatiliwa na watu wengi, si hapa Tanzania pekee, bali nchi mbalimbali ambazo wachezaji wao wanakipiga kwenye klabu hizo na hata nje ya Bara la Afrika.
Hata hivyo, kwa siku za karibuni, mechi za dabi zimeonekana kukosa mvuto ndani ya uwanja kutokana na ubovu wa uchezeshaji wa waamuzi.
Dakika 90 zinapomalizika, waamuzi hususan ni mwamuzi wa kati ndiye huwa 'Mchezaji Bora wa Mchezo' kutokana na kuzungumzwa zaidi kuliko mchezo na wachezaji wenyewe.
Mfano mdogo tu, hadi leo hii jina la Ramadhani Kayoko, mwamuzi aliyechezesha dabi ya mzunguko wa kwanza, ndilo jina linalozungumzwa zaidi tangu ulipomalizika mchezo huo Oktoba 19, mwaka jana.
Jina la mwamuzi huyo limekuwa likizungumzwa kwa mabaya kutokana na jinsi alivyouchezesha mchezo huo na kuonekana wazi kutoutendea haki kwa kutofuata sheria 17 za soka.
Zamani unapomalizika mchezo wa Simba na Yanga, mashabiki wanakuwa wamekaa vikundi vikundi wakizungumza juu ya uwezo wa timu hizo, mchezaji mmoja mmoja, nani alifanya vizuri, nani aliibeba timu na nani alikuwa nyota wa mchezo na mengine mechi.
Wachambuzi nao hawakupata tabu kuuchambua, tofauti na sasa, anayetamba ni mwamuzi aliyeamua mechi itaisha vipi kutokana na kuwa na matokeo yake mkononi.
Hivyo, tunachoshauri kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), sambamba na Bodi ya Ligi nchini (TPLB) na hata Kamati ya Waamuzi, kuchagua waamuzi waadilifu, ambao si waoga, wenye uwezi wa kusimamia sheria 17 bila kupindisha, kumwonea mtu, kutaka 'kubalansi' mchezo, na kufanya maamuzi magumu bila kupepesa macho, ili mradi tu yawe sahihi.
Hiki ndicho kinachokosekana kwa sasa kwa waamuzi wetu wakichezesha dabi. Hawana maamuzi magumu. Wanaruhusu kutawaliwa na wachezaji, kusukumwa, kufokewa na kudharauliwa. Huwa tunashangazwa inafika hatua hadi mchezaji anamsukuma mwamuzi, halafu hata kadi hatoi. Wakati akijua mwamuzi ni kama baba nyumbani, au hakimu mahakamani, hivyo unapoona wachezaji wanammudu basi jua kuna namna, si bure.
Wenye mamlaka ya soka wanatakiwa kuteua mwamuzi ambaye atakwenda kuwarejeshea heshima, kwani tayari kuna maneno mengi yamekuwa yakizungumzwa mitaani kuhusu 'mahakimu' hao wa mechi.
Na hata kama wakiwateua, wanatakiwa kukaa na waamuzi wastaafu kuwaelekeza nini cha kufanya kwenye mchezo huo wa dabi.
Kwa miaka ya karibuni mechi za dabi nchini zimekuwa zikijicheza zenyewe, si kama za vurumai kama miaka ya nyuma. Na hii imetokana na kuwapo kwa wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa hapa nchini, hivyo ufundi unakuwa mwingi zaidi.
Mwamuzi anachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wachezaji wanacheza soka kwa uhuru, hakuna rafu za kipuuzi, na kila kosa linaadhibiwa bila kufumbiwa macho, kwani tunaamini kama mwamuzi akifanya hivyo, mchezo utachezwa kwa heshima na nidhamu ya hali ya juu, kitu ambacho mashabiki wanatamani kukiona.
Kama kosa ni la penalti hata kama ni nne zitolewe, kama kadi nyekundu hata kama dakika ya kwanza ya mchezo itoke tu. Tumeshaona huko nyuma, kuna miaka fulani kila mchezo Simba ilikuwa inapata kadi nyekundu, ingawa mechi nyingi za aina hiyo ilikuwa ikishinda, lakini kwa sasa utaona kuna rafu nyingi za kuumizana, lakini waamuzi wamekuwa wakishindwa hata kutoa kadi ya njano na kuanza kujipa ugumu wao wenyewe mwingine anaporudishia.
Tunataka mchezo ukimalizika, wawapo watu ambao hawatofahamu hata jina la mwamuzi, badala yake kuizungumzia mechi, wachezaji na ufundi wa makocha jinsi walivyovitengeneza vikosi vyao.
Mashabiki kwa sasa wamechoka kuwazungumzia waamuzi kuwa nyota wa mchezo kwenye michezo ya dabi, jambo ambalo hatutamani kuliona likitokea tena katika mchezo huo wa Jumamosi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED