WENGI sasa wanaufahamu ugonjwa wa Mpox, baadhi wakizama hata kwa chanzo chake, jinsi unavyoenea, virusi vyake kusambaa kutoka kwa wanyama hadi binadamu na mengine mengi.
Mpox inapatikana zaidi katika nchi zilizo karibu na misitu ya mvua ya kitropiki. Katika maeneo hayo, kuna maelfu ya wagonjwa na mamia ya vifo kutokana na ugonjwa huo kila mwaka na watoto chini ya umri wa miaka 15 wameathirika zaidi. Nikirejea tovuti ya kihabari, ina ufafanuzi na elimu, kuna aina mbili kuu za virusi zinazojulikana kuwapo. Hali mbaya zaidi ilisababisha mlipuko wa kimataifa mnamo 2022 ambao ulienea kwa karibu nchi 100 ambazo hazikuwahi kukumbwa na virusi hivyo.
Shida ya pili, hatari ni ya kawaida katika Afrika ya Kati. Aina hizi mbili hubeba hatari tofauti za ugonjwa na vifo. Ni hivi karibuni tu, nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kukatangazwa aina hizo mbili, zikibeba hatari tofauti za ugonjwa na vifo. Dalili za ugonjwa wa Mpox, mtu kupata homa, maumivu ya kichwa, misuli na baadaye kupata vipele wa kufikia vidonda, ikianzia na vipele vikubwa.
Mnamo tarehe 7 mwezi uliopita, Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji habari, ikapokea taarifa juu za kuwapo dalili za Mpox katika jamii yetu.
Kati ya wanaohisiwa, ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi hiyo. Hiyo ni baada ya kupokea taarifa za wanaohisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa Maabara Kuu ya Taifa, kwa uchunguzi.
Mnamo Machi 9, uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili, wamethibitika kuwa na ugonjwa huo nchini na kutangaza rasmi taarifa hiyo mnamo tarehe 10 ya mwezi uliopita.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na vituo vyote vya kutoa huduma za afya, zinaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wanaohisiwa wengine, ili waweze kupatiwa huduma stahiki. Chanzo cha ugonjwa huo kinatajwa kuwa ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu huweza kuupata kutokana na shughuli zake.
Hiyo ni kupitia maji, nyama na endapo binadamu akipata maambukizi hayo, anaweza kumwambukiza mtu mwingine kwa kugusana. Kwa taarifa hiyo, Wizara ya Afya, inawahakikishia wananchi kuwa serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huu na hasa kutokana na uzoefu tulionao wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Serikali inasema inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa watu wanaoingia na kutoka kupitia mipaka ya nchi, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya. Kwa kupitia hilo, jamii inatakiwa ijifunze madhara ya mambo kama kuazimana nguo na kuepuka msongamano usio wa lazima.
Ni kwa kiasi kikubwa watu wajiepushe na magonjwa ya namna hiyo. Bila shaka, watu wanatakiwa kuzingatia kunawa kila wakati, kujiepusha na maambukizi ya namna hiyo. Wito ni kwa madereva na makondakta kujiepusha kubeba abiria wengi kupita kiasi, kwa sababu ya kipato badala yake wawe na abiria wanaopeana nafasi, kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Japokuwa serikali yetu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imejizatiti kuweka mikakati ya udhibiti, kuzama kwa umma, mwamko ni muhimu tukajitambua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED