Rais Samia: Tumepiga hatua kubwa lakini hatuwezi kuwa sawa katika kila kitu

By Enock Charles , Nipashe
Published at 03:01 PM Mar 08 2025
Rais Samia Suluhu
PICHA: MTANDAO
Rais Samia Suluhu

RAIS Samia Suluhu amesema suala la kupigania usawa wa kijinsia haliwezi kufanyika katika majukumu ya asili katika uumbaji na kuomba kusaidiana kati ya wanaume na wanawake.

Akizungumza na wananchi Jijini Arusha jana katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani , Rais Samia alisema kwamba Tanzania imepiga hatua mbalimbali katika masuala ya usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali za uongozi lakini kuna mambo ambayo hata hivyo hayahitaji usawa.  

“Kuna mambo ambayo mpaka dunia itakwisha wanawake na wanaume hatutakuwa sawa, mimi kama Mwanamke Mungu amenipa kazi ya kubeba mtoto tumboni kwangu na kumtoa kwenye mwili wangu kazi ambayo mwanaume hutaifanya  hata siku moja hata maendeleo gani yafanyike” amesema Rais Samia

“Lakini la pili Mwanaume umepewa jukumu la kuniwekea mbegu ili nibebe hiyo mimba na nimlee huyo mtoto kazi ambayo mimi Mwanamke siwezi kuifanya hapo hakuna cha usawa ,tunaenda kama Mungu alivyotuumba”-amesema Rais Samia

“Hali ilivyokuwa huko nyuma katika taasisi za kufanya maamuzi haikuwa ikiridhisha sana lakini sasa ni tofauti, sasa tunaona asilimia ya wabunge haipungui asilimia 33 katika madiwani kuna namba kisheria inayotakiwa ifikiwe lakini pia katika mawaziri tunajitahidi”-Samia