VIJANA saba wakazi wa Ifakara mkoani Morogoro maarufu 'Tuma pesa katika namba hii' wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, Dar es Salaam wakituhumiwa kwa mashtaka 28 likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na utakatisha wa fedha zaidi ya kiasi cha Sh milioni 1.
Vijana hao ni Yonas Mwombeki (21) Godfrey Kunemba (29 ), Ramadhani Libandika (22), Amdalah Liwewa (22), Nagwa Chonja (22), Dotto Yanila (20) na Aloyce Mwelenga (22).
Walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi na Nura Manja
Ilidaiwa kuwa baadhi ya jumbe ambazo walikuwa wakizituma kwa watu mbalimbali ni kama "TCRA-M-PESA Imefungwa akaunti yako ya M-PESA kwa msaada tembelea ofisi zetu ukiwa na barua kutoka POLICE na kitambulisho chako upate msaada wa laini yako asante"
"Utaingiza hiyo hela kwenye namba hii usajili ni Juma Ally Ramadhani", "TCRA-MPESA Akaunti yako IMEFUNGWA tafadhari tembelea office zetu ukiwa na kitambulisho au namba za NIDA".
Inadaiwa kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa kuongoza genge la uhalifu, kusambaza ujumbe usio rasmi, kutumia laini ya simu ambazo hazijasajiliwa kwa majina yao na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha walizojipatia kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu imedaiwa kuwa kati ya Januri Mosi, 2025 na Februari 10, 2025 mahali pasipo julikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa wote kwa pamoja waliongoza na kusimamia genge ya uhalifu.
Inadaiwa lengo la kutekeleza mipango ya udanganyifu kwa njia ya kuanzisha usambazaji wa ujumbe wa kielektroniki usiotakikana na kujipatia fedha kiasi cha Sh 1,922,000 kutoka watu mbalimbali.
Katika mashtaka ya kusambaza ujumbe usiokuwa rasmi washtakiwa wote kwa nyakati tofauti kati ya Februari 2024 na Februari 2025 maeneo yasiyojulikana washtakiwa kwa nia ya kudanganya, kupitia simu za mkononi zenye namba tofauti walisambaza ujumbe usiorasmi kw watu mbali mbali.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 20, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED