RAIS Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuharakisha mpango wa mita za maji ya kulipia kabla ya matumizi, ili kupunguza malalamiko ya kubambikiwa ankra za maji.
Akizungumza Machi 9, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji wa Mwanga, Same hadi Korogwe wa vijiji utakaohudumia vijiji 38, ambao ulikwama kwa miaka 19.
“Tafuta mita ambazo mtu atalipa kwa kadri anavyotumia ili anunue, mkiweka mita za tumia tu wanatumia tu wanamwagilia mbogamboga ukimpelekea ankara anasema umembambikia, jitahidi upate mita za kulipia kwanza itasaidia,”alisema.
Alisema: “Mamilioni ya fedha yamelala hapa fedha za mkopo mbali ya ambazo serikali imeweka, ndio maana hatuhamaisishi sekta binafsi kuingia kwenye miradi ya maji kwa sababu malipo yake ni makubwa, serikali tunatoa ruzuku kubwa, ili wananchi wapate maji. Nawaomba sana wanaotumia maji walipie ili tupate fedha tulipe mikopo.”
Aidha, alisema awamu ya pili itawafikia wananchi wa Korogwe huku akiwataka wananchi kulinda vyanzo vya maji na miundombinu kwasababu unahudumia wananchi wengi na umetumia fedha za serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED