Rais Samia : Tanzania ni msimamizi mpango wa Nishati Safi Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:42 AM Mar 09 2025
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania ni Msimamizi wa Mpango Maalum wa Nishati Safi Afrika

Amesema hayo wakati akizungumza  katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Kitaifa kwa  Tanzania yamefanyika Jijini Arusha, Tarehe 8 Machi, 2025 katika Uwanja wa Shekhe Amri Abeid Karuta.

Amefafanua kuwa Mpango wa Nishati Safi kuwepo nchini, kumeifanya Tanzania kuwa Msimamizi wa Mpango huo Maalum kwa Afrika.

" Katika Nishati Safi hii tunampango maalumu kama Tanzania, na kwa kuwa Tanzania ni msimamizi wa mpango huu kwa Afrika, hivyo nishati safi ya kupikia ni ajenda yetu kama nchi na tunaisimania Afrika", alisema Dk. Samia

Alisisitiza kuwa suala la nishati lipo katika mpango wa saba wa maendeleo endelevu katika nchi ya Tanzania hivyo Tanzania imefanya kazi nzuri katika kuhakikisha nishati safi inatumika.

"Sio nishati tu bali ni nishati safi tumefanya kazi nzuri ya kujenga bwawa la Mwalimu Nyerere na linatoa Megawati 2115 pamoja na bwawa hilo kuna mabwawa mengine madogo  sita ambayo yanatoa umeme katika maeneo mengine" 

Kuhusu usambazaji wa Umeme nchini, Dk. Samia  amesendelea kusema kuwa umeme kwa sasa Vijiji vyote 12,300 nchini tayari vimesambaziwa umeme na kazi hiyo inaendelea  katika Vitongoji.

" Suala la nishati tumepiga hatua kubwa tulikuwa tunafaidi umeme katika baadhi ya Vijiji na Minim sasa Serikali imeweza kusambaza umeme katika vijiji vyote 12300, Na tunavyoongea sasa Vitongoji  kadhaa tayari vimeunganishwa na kazi inaendelea," alisisitiza Rais.


Vilevile Dk. Samia Suluhu Hassan alieleza namna Tanzania ilivyobarikiwa kwa uwepo wa Gesi Asilia ambayo kama Taifa inaendelea kuichakata huku akieleza kuwa sasa  nchi  imetoka katika Umeme wa kutumia mafuta na kuelekeza nguvu Gesi Asilia na Maji ili kupata  nishati safi.

 Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na baadhi ya  watumishi kutoka Wizara ya Nishati.