TAKUKURU yaadhimisha Siku Wanawake kwa kuwatembelea waliolazwa hospitali

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 07:40 PM Mar 08 2025
Watumishi wanawake wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU)wakiwa katika picha ya pamoja kujiandaa kupeleka zawadi kwa wanawake waliolazwa wodi ya wazazi ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
PICHA: RENATHA MSUNGU
Watumishi wanawake wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU)wakiwa katika picha ya pamoja kujiandaa kupeleka zawadi kwa wanawake waliolazwa wodi ya wazazi ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

KATIKA kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani,taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU),imetoa bidhaa mbalimbali katika wodi ya wazazi waliojifungua ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa kwa ajili ya matumizi mbalimbali wakiwa hospitalini hapo.

Mbali na wodi ya wazazi pia Takukuru imekabidhi bidhaa nyingine kwenye wodi ya kujifungua ili viweze kuwasaidia pindi wanapojifungua hospitalini hapo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa mambo ya ndani wa Takukuru Leonada Ngaiza wakati akigawa bidhaa hizo kwa akina mama waliojifungua Kwa njia ya upasuaji na wale waliojifungua kwa njia ya kawaida.

"Tumeamua kuadhimisha pamoja siku ya wanawake duniani pamoja na wanawake wenzetu waliopo hospitalini,"amesema Luganzila.

Amesema wao kama Takukuru wameona ni vema kushiriki pamoja na wakinamama hao ili nao waweze kusherekea sikunya wanawake pamoja na kuwa wapo hospitalini.

Ofisa wa Takukuru,Stella Bukuru alisema wametoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 1.5 kama ishara ya upendo kutoka kwa wanawake wafanyakazi wa Takukuru ili kufurahi pamoja na wanawake wenzao waliolazwa katika hospitali hiyo.

Muuguzi Kiongozi kutoka wodi ya wazazi ya hospital ya Rufaa ya mkoa, Henry Mushi amewashukuru Takukuru kutokana na msaada wa bidhaa mbalimbali ambazo zimeletwa kwa wanawake hospitalini hapo.