Namna mapigano ya koo yalivyodhibitiwa Tarime

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 03:22 PM Mar 09 2025
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele
Picha: Mtandao
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele

JESHI la Polisi wilayani ya Tarime limelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya wananchi wa Koo za Wakira na Waanchari waliokuwa wameanzisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe wakigombea ardhi.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele alifika katika eneo la mapigano hayo juzi na kufanikiwa kuyasitisha kwa kukutanisha viongozi wa pande zote mbili katika mpaka unaotenganisha koo hizo katika Vijiji vya Nyabichune na Kototambe.

Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walionekana kubeba silaha za jadi yakiwemo mapanga na mishale, lakini serikali imedhibitisha hakuna mtu yeyote alijeruhiwa wala kupoteza maisha.

Hadi kufikia jumapili jioni mali yakiwemo mashamba na nyumba kadhaa ambazo thamani yake bado hakijajulikana vilikuwa vimeharibiwa ambapo Mkuu wa Wilaya, Gowele aliagiza Mkuu wa upelelezi Sirari kuwasaka na kuwakamata wahusika.

Viongozi wa maeneo hayo wanadai matukio ya mapigano hayo mapya yameibuka baada ya baadhi ya wananchi kukaidi maagizo ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kuzuia mtu yoyote kufanya kazi yoyote maeneo yenye mgogoro.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza viongozi wa vijiji husika kuzuia wananchi wao kuvamia upande wowote na kuendesha kilimo hadi pale serikali itakapoleta mipaka halali inayotambuliwa.

Amesema serikali hivi karibuni baada ya kukamilika kazi ya kamati ndogo aliyounda na Mkuu wa Mkoa wa Mara inatarajia kuja na matokeo ya kamati hiyo sambamba na uhamuzi wa mipaka halali ya eneo hilo linalogombaniwa.

Diwani wa Kata ya Regicheri, John Bosco amesema baadhi ya wananchi walivamia na kuharibu mazao na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa wananchi wanaogopa kuishi na kushughulikia kilimo.

"Tunamshukuru DC (Mkuu wa wilaya) kwa kuzima mapigano haya kabla hayajaleta mauaji na uharibifu zaidi kama miaka ya nyuma ambapo wananchi waliuawa na bila sababu," amesema Bosco.

Mkuu wa Upelelezi Sirari, Aaron Mihayo amesema jeshi la polisi wanaendelea kuimarisha doria na kuhakikisha hakuna uharibifu unafanyika tena katika maeneo hayo.

Amesema walifanikiwa kuzuia ugomvi wa kutumia silaha za jadi na kutahadharisha kuwa kila raia wa Tanzania ana haki ya kukutana na kwenda popote ilimradi havunji sheria.