Olengurumwa ataka waasisi haki za wanawake waenziwe

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 01:08 PM Mar 08 2025
MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa
PICHA: MPIGAPICHA WETU
MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa

MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa ameomba katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kukumbukwa kwa wanawake watetezi waasisi walioweza kufikisha lengo la kuleta usawa kwa wanawake nchini.

Maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka THRDC inaomba Serikali, jamii na  wadau mbalimbali kuenzi na kutambua mchango wa wanawake waliojitoa kupambania haki za wanawake hadi kufika sasa.

Amesema juhudi zilizofanywa na waasisi hao watetezi wa wanawake katika nchi hii ni kubwa sana na leo wanawake wanajivunia ukombozi wa mwanamke kupitia waasisi hao na wengine wakafuata nyayo.

Kutambua jitihada za waasisi hao katika kuleta usawa  kwa wanawake katika elimu, siasa, kiuchumi pamoja na kuwawezesha wanawake kutambua haki zao katika  kuzingatia utawala bora, sheria na haki za wanawake wasimame kidete.

“Hata  maazimio 12 yanayosherehekewa sasa ya miaka 30 ya Beijing huwezi kuacha kuwataja wanawake hao, hata kizazi cha pili cha watetezi wa haki za wanawake na hiki kilichopo sasa yametokana na waasisi hao” alisema

Ametaja baadhi ya wanawake hao waasisi wa watetezi wanaotakiwa kuenziwa kwa juhudi zote ni pamoja na Bibi Titi Mohamed, Getrud Mongela, Anna Tibaijuka, Hellen Kijo Bisimba na wengine wengi ni watu wa kukumbukwa kutokana na mchango wao.

Aidha amewashauri kupitia maadhimisho hayo yanayofanyika duniani kote watetezi wa haki za wanawake wanatakiwa kuchakata na kutathimini  changamoto zote zinazowakuta wanawake bila kusahau haki za watoto na makundi mengine.