OFISA Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mansoor Industries Limited, Altaf Hirani, amezishauri nchi za Afrika Mashariki, kutafuta fedha zake wenyewe za kuwekeza katika miradi ya maendeleo, ikiwamo ya mafuta na gesi.
Hirani, alitoa ushauri huo juzi, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya kushiriki katika Mkutano wa 11 wa Maonesho ya Petroli wa Afrika Mashariki(EAPCE’25), uliofanyika kwa siku tatu, jijini Dar es Salaam.
Alisema nchi hizo kuwa na fedha zake wenyewe katika kuwekeza na kuendeleza miradi yake, itaharakisha zaidi maendeleo yake.
“Uwekezaji katika sekta ya mafuta, nafikiri sisi kama Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, inabidi tutafute fedha kutoka kwa wadau na taasisi mbalimbali kutoka kwenye nchi zetu ikiwamo Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), pamoja na taasisi ambazo ziko tayari kutupa fedha, kwa sababu kama tutapata fedha yetu wenyewe, tutafanya mabadilko haraka zaidi,” alisema Hirani.
“Kwa hiyo kwenye miradi yetu yote ikiwamo za miundombinu na ile ya mafuta, inabidi tutafute fedha yetu wenyewe, kwa sababu rasilimali tunayo, hivyo ninaamini tunaweza tukatumia hizo kutafuta fedha na tukafanya maendeleo ya haraka sana kwa sababu tunahitaji maendeleo, tunahitaji nishati lakini tunahitaji fedha kuwekeza.”
Alisema anaamini taasisi hizo zikiungana kwa pamoja na serikali za nchi hizo, fedha za kuendeshea miradi mikubwa ya maendeleo zitapatikana.
“Ninaamini benki ya AfDB na taasisi nyingine zikiungana na serikali zetu, tunaweza kutafuta fedha ya kuleta maendeleo ya haraka sana na inabidi ifanyiwe kazi haraka, lazima tufikirie, tutathimini na tufanye vyote,” alisema Hirani.
Kuhusu miradi ya kimkakati ambayo serikali ya Tanzania inafanya, Hirani alisema hayo ni miongoni mwa maono mazuri ambayo yatawanufaisha Watanzania wote.
“Ni maono mazuri sana serikali yetu kutekeleza hii miradi ya mikubwa ya maendeleo na inahitaji kupongezwa katika hilo, lakini pia nimeona katika sekta ya gesi, serikali yetu iko kwenye mpango wa kuuza vitalu.
“Sasa hiyo inaonyesha iko makini na inaweka mazingira imara ya watu kuwekeza ili Watanzania wote wafaidike, ni maono mazuri na ambayo inabidi tufanyie kazi na kuchangamkia fursa,” alisema Hirani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED